LIBERIA WAPIGA KURA KUCHAGUA RAIS MPYA

0
5

MONROVIA: Liberia


WANANCHI wa Liberia walipiga kura jana kuchagua rais ambaye atakuwa badala ya rais wa sasa  mwanamke na mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel,   Ellen Johnson Sirleaf.

Mwanasoka wa zamani,  George Weah (51) na Makamu wa Rais,  Joseph Boakai ndiyo washindani wakubwa wa urais katika uchaguzi huo.

Liberia, ambayo ilianzishwa katika Karne ya 19 na waafrika waliokuwa watumwa Marekani  haijawa na mabadiliko ya amani ya madaraka ya urais kwa miaka 73.

Sirleaf aliwataka wananchi kushiriki katika uchaguzi huo kwa amani katika nchi hiyo ambayo iliwahi kukabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 14.

“Kura yako ni kuhusu wewe na familia yako – siyo chama, ukabila,” alisema katika hotuba yake kwa taifa.

Watu wapatao 20 wanagombea urais katika uchaguzi huo.

Hao ni pamoja na  Alex Cummings, ofisa mkuu wa zamani wa Kampuni ya   Coca-Cola, na MacDella Cooper, mwanamitindo wa zamani na rafiki wa zamani wa kike wa   Weah.

Sirleaf (78), hagombei tena baada ya kumaliza uongozi wake wa mihula miwili.

Alishika madaraka mwaka 2006 baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo,   Charles Taylor, kulazimishwa kuachia madaraka mwaka 2003 na waasi waliokuwa wanaipinga serikali yake.

 

Hivi sasa Taylor anatumikia kifungo cha miaka 50 Uingereza kwa makosa ya vita yanayohusiana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here