KIVUMBI LIGI KUU BARA KUANZA LEO

0
540

NA WINIFRIDA MTOI         |                


PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/2019, linatarajia kufunguliwa leo huku ikiwa haina mdhamini mkuu baada ya Kampuni ya simu ya Vodacom kumaliza mkataba wake.

Mbali na kutokuwa na mdhamini, msimu huu idadi ya timu imeongezeka kutoka 16 hadi 20, hivyo kuna uwezekano mkubwa timu nyingi kushindwa kufika vituoni kutokana na kukosa fedha.

Wadhamini waliojitokeza hadi sasa ni Kampuni ya Azam na Benki ya KCB ya Kenya.

Ligi hiyo itaanza kwa mechi sita kupigwa leo katika viwanja tofauti lakini kati ya hizo mchezo unaotarajia kuvuta hisia za wapenzi wengi wa soka ni ule unaohusisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba watakaowakaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Uhuru,  jijini Dar es Salaam.

Simba watashuka dimbani wakiwa ni mabingwa wa Ngao ya Jamii kwa mwaka huu wakitwaa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, katika mechi iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Wekundu wa Msimbazi, watavaana na Prisons 1:00 usiku badala ya saa 10:00 kama ilivyopangwa awali kutokana na Sikukuu ya Idd Alhaj.

Hamu kubwa ya mashabiki wa kikosi hicho ni kutaka kuona ubora wa timu yao katika mechi za Ligi Kuu kama itaendeleza ubabe baada ya kufanya vizuri kwenye mechi za kirafiki, Simba Day dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar.

Tofauti na hilo, pia Wanasimba wengi wanahamu ya kuona matunda ya kambi ya timu yao waliyokuwa wameweka nchini Uturuki pamoja na ubora wa wachezaji wapya.

Simba iliweka kambi ya wiki mbili Uturuki kwa lengo la kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ambako walifanikiwa kucheza mechi tatu za kirafiki.

Ikumbukwe kuwa baada ya kumalizika kwa ligi ya msimu uliopita, Simba walifanya usajili mkubwa kwa kuchukua wachezaji walioonyesha viwango vya juu katika timu mbalimbali, ndani na nje ya Tanzania.

Tayari wachezaji; Meddie Kagere,  Cletus Chama, Adam Salamba, wameonekana kuwateka wapenzi wa Simba kutokana na kiwango walichokionyesha katika mechi kadhaa,  lakini bado ubora wao utadhihirika pale watakapoonyesha makali yao kwenye ligi hiyo.

Hassani Dilunga naye baada ya kuwakosha mashabiki wa Wekundu hao,  alipofunga bao la ushidi dhidi ya timu yake ya zamani Mtibwa  Sugar katika mechi ya Ngao ya Jamii, wakimsubiri kumwona akifanya vizuri kwenye mchezo wa leo, ni wazi atawaaminisha wadau wa kikosi hicho kuwa hakubahatisha.

Katika mechi za hivi karibuni tumeona pacha ya washambuliaji wa Simba, Kagere na Emmanuel Okwi, ikiwa na mafanikio makubwa, je, kwenye ligi itaendelea hivyo? Picha kamili itaanza kuonekana leo.

Kwa upande wa Kocha Mkuu Mbelgiji, Patrick Aussems, atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha anapata matokeo mazuri kwa sababu utakuwa ni mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu tangu akabidhiwe kikosi hicho.

Ukiangalia kikosi cha Prisons wanachokutana nacho Simba, ni moja ya timu ngumu katika ligi hiyo, hivyo haitakuwa mechi rahisi ya kujiaminisha kupata matokeo mazuri bila kupambana.

Katika kudhihirisha hilo, kocha wa Simba, Aussems, baada ya mechi na Mtibwa Sugar alisema ugumu walioupata kuifunga timu hiyo, inaonyesha jinsi atakavyokwenda kukabiliana na upinzani mkali kwenye ligi.

“Tanzania kuna timu nzuri si Simba pekee, lazima tujipange ili kutetea ubingwa wetu, tunaanza ligi tukijua tunakwenda kukabiliana na wapinzani wenye timu nzuri,” alisema Aussems.

Nao Prisons wanaingia katika mchezo huo wakiwa wametokea kambini visiwani Zanzibar walikokaa kwa wiki mbili na kucheza mechi nne za kirafiki.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons,  Abdallah Mohammed, alisema wamejipanga kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo kutokana na  maandalizi bora ya timu yao.

“Siwezi kujua wapinzani wangu wamejiandaa vipi, kila kocha ana mbinu zake za kukabiliana na mchezo muhimu kama huu, kwa sisi lengo letu ni matokeo mazuri,” alisema Mohammed.

Michezo mingine inayotarajiwa kupigwa leo, Singida United watawakaribisha Biashara United kutoka mkoani Mara katika Uwanja wa Namfua, Singida.

Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC, Uwanja wa Mabatini, uliopo Mlandizi, Pwani, wakati Lipuli ya Iringa watakuwa wageni wa Coastal Union katika dimba la Mkwakwani, Tanga.

Mechi nyingine Alliance na Mbao zote za jijini Mwanza, zitamenyana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza huku Kagera Sugar wakiwakaribisha Mwadui FC katika Uwanja wa Kaitaba,  mjini Bukoba, mechi zote zikichezwa saa 10:00 jioni.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo minne ambapo Yanga watacheza dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Azam FC watawakaribisha Mbeya City,  Uwanja wa Azam Complex, Chamazi,  Stand United watachuana na African Lyon, Uwanja wa Kambarage,  Shinyanga, wakati JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa KMC kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here