KITANZI CHA TWAWEZA NA UHAKIKA WA TAFITI HURU SIKU ZIJAZO

0
457

Na, ANDREW MSECHU                |                      


MATOKEO ya utafiti wa Twaweza mwaka 2016, mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Urais mwaka 2015 yalionesha umaarufu wa Rais John Magufuli umepanda na kufikia asilimia 96.

Matokeo ya utafiti uliofanyika mwaka mmoja baadaye na kutolewa Juni 2017 yalionesha kushuka kwa umaarufu wa Rais kutoka asilimia 96 hadi asilimia 71, japokuwa wananchi waliendelea kuridhishwa na utendaji wake.

Mwaka mmoja baadaye, Julai 2018 Twaweza katika matokeo yake ya utafiti uliopewa jina la Sauti za Wananchi, Kuwawajibisha Viongozi na Nahodha wa Meli Yetu Wenyewe, imeingia matatani baada ya kuonesha matokeo kuwa umaarufu wa Rais umeshuka kutoka asilimia 71 mwaka 2017 hadi asilimia 55 mwaka 2018.

Ukilinganisha matokeo hayo na yale ya mwaka 2016, kutoka asilimia 96 hadi asilimia 55 mwaka 2018 inaakisi kuwapo kwa matatizo yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi ili kurejea katika kiwango cha awali cha umaarufu kwa siku zijazo.

Awali, Twaweza ambayo imeeleza pia kushuka kwa umaarufu wa baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani ilionekana kuwa taasisi inayofanya kazi zake kwa weledi, kupongezwa na kupewa nafasi nzuri, ikiwamo kuonekana kwa uthabiti wa viongozi wake, akiwamo Mkurugenzi Aidan Eyakuze.

Utafiti huo haukupokelewa vizuri, hasa katika kipengele kilichoonesha kushuka kwa umaarufu wa Rais, ambacho kimeleta taharuki miongoni mwa wanasiasa na watendaji wa Serikali.

Mara tu baada ya matokeo ya utafiti huo kutolewa, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) haikuchukua muda kuiandikia barua Twaweza kutaka waeleze kuhusu matokeo ya utafiti huo na kwanini wasichukuliwe hatua.

Kwa mara ya kwanza, uraia wa Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze ukaanza kutiliwa shaka na Idara ya Uhamiaji kuamua kushikilia pasi yake ya kusafiria kama sehemu ya uchunguzi kuhusu uraia wake.

Hatua hii inaweza kuingiwa woga wa aidha kuchukuliwa hatua kwa taasisi hiyo na kupoteza uhuru wake katika kufanya tafiti na kutoa matokeo chanya kwa mujibu wa uhalisia wa matokeo ya tafiti zao.

Uhuru wa Twaweza

Katika mahojiano, Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema kuna wasiwasi kutoka kwa jamii na washirika wa tafiti za Twaweza kwamba huenda uhuru wao katika kufanya tafiti za namna hiyo ukapungua, lakini hali sivyo ilivyo.

Alisema Twaweza itaendelea kuhakikisha kwamba ina uhuru wa kutangaza matokeo ya tafiti zake kama yanavyojitokeza na wanavyoyabaini kwa kutumia njia za kitaalamu.

Alisema katika tafiti zao, suala la uhuru wa kutangaza kile wanachokipata halitaingiliwa na watahakikisha kwamba katika kufanya hivyo, methodolojia zinazotumika kupata taarifa za kitafiti zinaainishwa, matokeo yanaainishwa na uchambuzi wao unaainishwa ili watu waelewe namna hitimisho linalotolewa kwa umma lilivyofikiwa.

“Kwa hiyo uhuru huo kwetu sisi ni suala la msingi na tutahakikisha tinashirikiana na Serikali na wananchi tunaulinda na kuukuza uhuru huo na kuonesha kwa umma na Serikali manufaa ya kupata mawazo mbadala na mawazo chanya na mtazamo unaoweza kuchangia kuwapa maono tofauti na changamoto ambazo wao wakiwa vitani kila siku wanazipata,” alisema.

Alisema katika kutekeleza hilo, wanahakikisha wanashirikiana na taasisi zinazowapa ruhusa kukusanya takwimu, wanafuata taratibu zilizowekwa kisheria na wanapata ushirikiano wa watendaji katika maeneo wanayofika, ikiwamo kupata maelekezo na ramani za maeneo ya kuhesabia kutoka kwa Serikali za Mitaa na maeneo kama hayo.

Eyakuze alisema mwaka 2015 walitembelea kila wilaya za Tanzania na kuzungumza na kaya 600, pia kuwahoji watoto zaidi ya 150,000 kwa hiyo huwezi kufanya kazi hiyo bila kuwa na ushirikiano wa mamlaka husika.

Eyakuze alisema pamoja na matukio yote ya hivi karibuni yaliyosababisha Twaweza kutajwa na kujadiliwa katika vyombo vya habari na mijadala ya umma, taasisi hiyo imepitia kipindi chenye changamoto za mashirikiano baina yake na baadhi ya taasisi za Serikali kufuatia uzinduzi wa taarifa za ripoti mbili za Sauti za Wananchi mnamo Julai 5, zenye vichwa vya habari; Kuwapasha Viongozi? Na Nahodha wa Meli yetu wenyewe?

Alisema hata baada ya kupokea barua mbili kutoka Costech zilizohoji uhalali wa programu ya Sauti za Wananchi na kuwataka wafafanue kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao, ambazo wamezijibu, kisha Idara ya Uhamiaji kushikilia pasi ya kusafiria ya Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza tangu Julai 24 na kumfanya ashindwe kusafiri nje ya nchi, misingi ya Twaweza itabaki kama ilivyo.

Alisema Twaweza ni shirika lenye kuamini katika uwazi na linashirikiana kwa ukaribu na wadau muhimu katika jitihada zake za kuchangia katika ukuaji wa demokrasia na maendeleo nchini Tanzania na mara kadhaa wamefanya kazi na Serikali na kuchangia jitihada za Serikali kwa kufanya tafiti zinazoleta takwimu muhimu katika kuibua mawazo na habari zenye kutoa mwangaza na uhalisia wa mambo katika kujaribu kutafuta ufumbuzi wa masuala muhimu.

Shirika la Twaweza lilianzishwa mwaka 2009 na Mwanaharakati Mtanzania, Rakesh Rajani ikifanya kazi zake nchini Kenya, Tanzania na Uganda kwa lengo la kuhamasisha uwepo wa raia makini (watu kufanya kazi ya kutatua matatizo yao wenyewe na kushirikiana na Serikali; mamlaka zenye kuwajibika (Serikali sikivu na yenye kuchukua hatua kwa umakini hoja na mawazo ya wananchi); na watoto kujifunza ili waweze kukua na kuwa raia wenye tija na ushiriki.

Kutikiswa

Pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi yake na dhidi ya Twaweza kama taasisi, Eyakuze alisema hawezi kukiri kwamba kwa wakati huu wametikiswa, kwa kuwa si mara ya kwanza kutakiwa kutoa maelezo kuhusu matokeo ya tafiti zao.

Alisema mwaka 2015 walitoa tafiti zinazofanana na hizi walizozitoa hivi karibuni, ambazo zilizua mjadala mpana na kufikia hatua ya Twaweza kuhojiwa.

Alisema hatua kama hizo zinapochukuliwa wanachukulia kama sehemu ya kazi yao, kwa kuwa hawatarajii mapokeo chanya pekee kwa sababu tafiti zilizo huru lazima ziibue mijadala, hivyo uhusiano unaendelea kujengwa kwa hatua kama hizo za kuandikiwa barua, kuhojiwa na kutoa majibu.

“Suala la kubadilishana barua, kuelezana na kuelekezana na kuhakikisha kwamba kwa kuwa sisi ni taasisi inayosimamia uwazi tunalinda uhuru wa mijadala na kujieleza, hivyo sisi pia tunapoombwa kujieleza tunatimiza wajibu wetu wa kujieleza, tuko tayari kabisa kutekeleza,” alisema.

Alisema kwa sasa kazi za Twaweza zitaendelea kama kawaida, bila kupoa na bila kujibana, ila katika mazingira ya kuheshimu sheria na taratibu za nchi.

Akifafanua hilo, alisema tayari uongozi umeshakaa na Bodi ya Wakurugenzi na wadau na wamekubaliana kuwa wataendelea kufanya kazi zao kama kawaida na hawatojibana wala kujiwekea mipaka, ila wataendelea kufanya kazi zao za utafiti za ushirikiano wa karibu kabisa na Serikali na wadau kama ambavyo wamekuwa wakifanya tangu mwaka 2009.

“Tuna imani tutaendelea kupata ushirikiano wa taasisi za Serikali ambako tunaenda kuomba kibali, kuomba ushirikiano kwa wataalamu wao kuja kutusaidia kuainisha au kutunga methodolojia zetu, kwa kuwa yapo maeneo mengi tu ambayo bado yanahitaji kazi za takwimu.

“Lakini hapa, tuwe wazi pia kwamba tutaendelea kusimamia malengo yetu, mojawapo ikiwa ni kuona ushirikiano wa Serikali na Umma unakuwa wenye tija na manufaa kwa umma, kwa kuwapo uwazi, ushiriki wa pamoja na uwajibikaji,” alisema.

Kuhusu kuhojiwa methodolojia ya Sauti za Wananchi, alisema methodolojia hiyo imewekwa wazi kabisa kwa kuandikiwa kitabu na katika tafiti zozote ni jambo zuri kuhojiwa na wamekuwa wakijibu, ikiwamo maswali kadha ambayo yaliwahi kuibuka ikiwamo kwanini wamewapa watu simu kama sehemu ya kuwezesha utafiti wao unaofanyika kwa njia ya simu.

Alisema wapo watu waliohoji kwa hoja kuwa wamewapa watu simu ili wapate majibu wanayoyataka katika tafiti zao, lakini jibu la msingi ni kwamba walikuwa bado wanatafuta uwakilishi wa kitaifa, kwa kuwa Watanzania wengi sasa wana simu za mkononi, lakini ukiwatumia hao tu unapata maoni angalau ya asilimia 80 ya Watazania, kwa hiyo unakosa uwakilishi wa kitaifa kwa kuacha asilimia 20 ya wasio na simu.

“Kwa hiyo, tunataka uwakilishi wa kitaifa kwa kuwapata wale asilimia 20 ambao hawana simu kwa kuwapa simu na chaja zake. Katika kuwapata hao, tunatafuta maeneo 200 ya kuhesabia na kutafuta kaya 10 kwa kuanza nyumba moja na kupiga hatua 50 kufika nyumba nyingine na wanaokubali wanapokea simu na mkataba wa kuwa tayari kuhojiwa kwa muda tutakaokubaliana, lakini zaidi lazima wawe na umri usiopungua miaka 18,” alisema.

Alisema kwa wanaohoji kwamba hawajapigiwa simu ni kwa sababu hawakuwapo miongoni mwa Watanzania 2000 waliochanguliwa kuwakilisha zaidi ya Watanzania watu wazima milioni 30, watoaji wa maoni, ambayo ni sampuli sahihi inayotumika kupata uwakilishi wa watu waliopo nchini.

Eyakuze alisema huko mbele ya safari, kwenye mipango yao kama walivyofanya miaka minne iliyopita, kila mwaka wamekuwa wakifanya tafiti za namna hiyo hivyo wataendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia sheria na mipaka ya nchi husika.

Programu za Twaweza

Eyakuze alisema tangu kuanzishwa kwa Twaweza imesimamia programu zake kubwa tatu, ambazo ni Uwezo, Kiu-Funza na Sauti za Wananchi ambazo zimeonesha mafanikio makubwa katika kuibua matatizo yanayolalamikiwa na wananchi na mamlaka husika kuwajibika na kuyatafutia ufumbuzi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here