Kimenuka mabasi mwendokasi

0
596

*Mwendeshaji  akwama, abiria waingia barabarani

*Makonda aingilia kati, JPM ampa onyo Mtendaji DART

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAKATI abiria wa mabasi ya mwendokasi wakijikuta wakikwama vituoni jana kwa kukosa usafiri, madudu kadhaa yamefichuka huku ikielezwa kuwa  mmiliki wa kituo cha mafuta kwa ajili ya mabasi hayo amegoma kutoa kutoa huduma hiyo  kwa Kampuni   ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart).

Taarifa za ndani ziliiambia MTANZANIA jana kuwa baada ya kuzuka  kwa vurugu hizo, serikali iliingilia kati suala hilo lilosababisha usumbufu kwa abiria wa mabasi hayo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ilibainika kuwa  Kampuni   Camel Oil ambayo hutoa mafuta kwa mabasi ya Udart kupitia kituo chake   cha mauzo cha Kurasini jana ilikataa kutoa huduma hiyo.

Ilielezwa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa  Camel Oil alitoa  agizo mabasi hayo yasipewe mafuta jana kwa vile hadi sasa  Udart inadaiwa mamilioni ya fedha na kampuni hiyo.

“Tumefuatilia kwa kina kuna ubabaishaji mkubwa kwenye huu mradi hasa  mwendeshaji anadaiwa madeni na watu ambao wanatoa huduma kwake yakiwamo makampuni ya mafuta… sasa vinageuzwa viswahili na kuonekana kuna hila.

“Na   kama Camel Oil anadai mamilioni ya fedha na amefikia hatua ya kusimamisha kutoa huduma kwa mwendeshaji, je kwa hatua hii serikali inalaumiwa vipi?

“Ni lazima huyu mwendeshaji ifike mahali ajitafakari mwenendo wake kama anaweza kwenda na kasi inayotakiwa… na kwa hali hii kuna kila sababu ya kuwa na waendeshaji zaidi ya mmoja.

“… kama tungekuwa na mfumo wa kuwa na mwendeshaji zaidi ya mmoja, mfano kama huyo ambaye amekwama leo (jana) kutoa huduma na kusingizia mambo mengine, abiria wasingekwama hata sekunde,”  alisema mmoja wa vigogo wa serikali ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini.

MTANZANIA ilipomtafuta Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Udart, Deus Bugaywa, alisema  si kweli kwamba kamouni hiyo inadaiwa.

Alisema kama kampuni hiyo ingekuwa inadaiwa,  mabasi yangewezaje kutembea.

“Si kweli, kama ndivyo je mabasi yangewezaje kutembea?” alisema Deus na kukata simu.

HALI  ILIVYOKUWA VITUONI

Jana asubuhi ilikuwa ni mateso kwa abiria wanaotumia usafiri wa mabasi ya mwendokasi ambako umati wa watu ulijazana  vituoni kwa muda mrefu.

MTANZANIA ilishuhudia mamia ya wananchi wakiwa wamejazana vituoni kuanzia saa 12 asubuhi na kadri muda ulivyokuwa unakwenda hali ilizidi kuwa mbaya.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili walisema sasa umefika wakati serikali kumwangalia mwendeshaji wa mabasi hayo na ikiwezekana itafute mbia mwingine.

“Unajua haya ni mateso tangu saa 12 asubuhi hadi sasa bado nipo hapa na sijui la kufanya, kazini nimechelewa, niambie muda huu saa 2:30 bado nimekwama!

“Ninafiki ipo haja kwa Rais Magufuli kuangalia… anadondoshwa na watendaji wake kupitia huyu mwendeshaji ambaye amekuwa mbabaishaji sana,” alisema John Masii mkazi wa Kimara.

Naye Rehema Said, alisema kukwama kituoni hapo kumekuwa ni mateso makubwa huku akiomba mamlaka za juu kuingilia kati suala hilo.

“Unaona kaka yangu hapa tangu asubuhi tumekwama, ona wanafunzi wanavyohangaika na sasa watu wameamua kuingia barabarani katika vituo vyote… kile cha pale Korogwe na hapa Kimara mwisho.

“Wamekuwa polisi lakini hakuna msaada tuliopata  na watu wengine wameamua kutoka nje na kutafuta usafiri mbadala huku nauli   wanasamehe,” alisema Rehema.

KAULI YA UDART

Jana ilipofika mchana, Kampuni ya UDART kupitia Meneja wa Idara ta Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Deus Bugaywa, ilisema kazi ya kuyatoa mabasi ndani ya ofisi na karakana zao zilizopo   Jangwani kwenda kuanza kazi hufanyika kuanzia saa 9:45 alfajiri   kuwezesha huduma kuanza saa 10:30 alfajiri.

Hata hivyo alisema jana baada ya mabasi matano ya kwanza kutoka ndani, dereva mmoja alichukua basi kubwa lenye urefu wa mita 18 na kuliegesha eneo la ndani ya lango kuu la kutokea upande wa mbele hivyo likaziba njia.

“Na wakati huo huo dereva mwingine aliziba lango la nyuma kwa basi lenye ukubwa kama huo. Madereva wote wawili waliondoa funguo kwenye mabasi hayo na kukimbilia nje ya uzio wa karakana yetu huku juhudi za walinzi kuwafuatilia zikishindwa kuzaa matunda,” alisema Bugaywa.

Alisema hali hiyo ilisababisha kazi ya ziada kufanywa na mafundi kuyaondoa mabasi hayo na kuwezesha mabasi mengi zaidi yaliyokuwa bado ndani ya uzio kutoka kwenda barabarani kuanza kazi.

Alisema kazi hiyo ilifanikiwa lakini tayari ratiba ilikuwa imevurugika na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria.

MASWALI UTATA

Pamoja na taarifa hiyo, taarifa za uhakika ni kwamba mabasi hayo huwa na funguo tatu ambako dereva wa gari hupewa moja na nyingine mbili hubaki ofisini.

MAKONDA AINGILIA KATI

Kutokana na kashehe hiyo, jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwaagiza watendaji wote wanaosimamia UDART kukutana naye leo saa 12:30 asubuhi Kituo cha Mabasi Kimara .

Makondaa alisema l  anataka kufahamu kwa nini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa  kumaliza kero kwa wananchi.

Alisema hafurahishwi hata kidogo na namna mradi wa mabasi hayo unavyoendeshwa .

Alisema hata matarajio ya Rais Dk. John Magufuli ya  kuona changamoto ya muda mrefu ya usafiri inageuzwa kuwa  historia kupitia mradi huo,  yamekuwa tofauti.

“Hatuwezi kuvumilia kuona wananchi wanateseka wakati Serikali yao ipo kwa ajili yao.

“Kesho lazima hili liishe ili wananchi  wasafiri pasipo usumbufu kama Serikali yao inavyotaka.

“Na nitumie fursa hii kuwaomba radhi wananchi,” alisema Makonda katika taarifa yake kwenye mtandao wa jamii wa Instagram.

 ATUMBULIWA, ARUDISHWA

Dakika 10 zilitumika kumpa nafasi ya Utendaji Mkuu wa UDART    Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad)  Mkoa wa Singida,  Leonard Kapongo,  lakini baada Rais Dk. John Magufuli alitengua uteuzi huo na kumrudishia   Donald Lwakatare

Hali hiyo ilijitokeza  jana wakati Waziri Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),  Selemani Jafo  alipowaambia waandishi wa habari kuhusu kutenguliwa kwa  Lwekatare kutokana na maelekezo ya Rais Dk. Magufuli.

Hata hivyo, baada ya kama dakika 10  waandishi wa habari kuondoka ofisini kwa Jafo, aliwaita tena na kueleza yalikuwapo mabadiliko kuhusu taarifa hiyo.

Jafo alisema alipewa tena maelekezo kwamba  Lwakatare   ataendelea na cheo chake kama mtendaji mkuu wa UDART   ila anatakiwa kujitathmini.

“Kama mmeshuhudia leo (jana) watu wengine wamepita katika madirisha (Dar es Salaam) na nikiwa kama Waziri wa Tamisemi siridhiki na mwenendo huu, namuagiza mtendaji mkuu anipe nini kinachoendelea,  kwa nini kuna hali ya kusuasua?”alisema.

Jafo  alisema yamekuwapo  malalamiko ya wafanyakazi kuhusiana na mtoa huduma wa Udart  lakini amekuwa  hashughulikiwi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here