KAMPUNI ZINAVYOPAMBANA KUNUSURU UGUMU WA MAISHA KWA WATEJA

0
901

Na MWANDISHI WETU


AGOSTI mwaka huu, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo, kupitia huduma yake ya Tigopesa, walitoa gawio la Sh bilioni 2.35 za faida kwa wateja wao wanaotumia huduma hiyo kupitia simu za mkononi.

Hii ni robo ya malipo ambayo kampuni imechangia kwa wateja wake, ambapo inakamilisha jumla ya Sh bilioni 81.8 tangu kampuni hii ilipoanza kugawa faida kwa wateja wake mwaka 2014.

Suala hili linapotazamwa kwa mtazamo wa kibiashara, utoaji wa faida kwa wateja unaweza kuonekana kama gharama katika biashara hivyo kuwa ni jambo linalopaswa kuepukwa. Wakati huo huo, ni sawa kwamba mteja aliyeridhika ambaye pia kimsingi ndio uti wa mgongo wa biashara anapaswa kuzawadiwa. Mteja yuko katika msingi wa mapato, riba na uvumbuzi unaopatikana katika ngazi ya mabadilliko.

Kwa hiyo mteja anapaswa si tu azawadiwe kwa kuamini huduma anazotumia, lakini pia anapaswa kujihisi kuwa yeye ni sehemu ya kampuni kwa kupitia juhudi za kampuni za kutambua mchango wao, na zaidi kwa kujenga kipengele muhimu kinachotakiwa zaidi cha uaminifu wa mteja na kuthamini nembo ya kampuni. Pia inajenga mazingira ya faida ya pande zote ambazo ni kampuni na mteja. Mara nyingi ni tumaini la kampuni nyingi kuongeza uzalishaji, pia wakiwa wanatoa mapato yao kwa njia sahihi na inayoeleweka.

Akitangaza riba ya robo mwaka jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari, anasema:  “Riba ya robo mwaka inadhihirisha zaidi kwamba Tigopesa ni zaidi ya pesa – Tigopesa ‘ni zaidi ya pesa’. Kila robo ya mwaka tunatoa riba ya robo mwaka kwa wateja kwa kutegemea salio lao la kila siku katika akaunti zao za simu za mkononi.”

Kwa sasa Tigo wanajivunia mtandao unaokua kwa kasi zaidi nchini wenye zaidi ya wateja milioni 12 waliosajiliwa, zaidi ya wateja milioni saba wanaotumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, Tigopesa, pamoja na mtandao wa zaidi ya wafanyabiashara 40,000 na ina mawakala 85,000 wa huduma za fedha kupitia simu za mkononi.

“Tigo imekuwa ni kampuni ya kwanza ya simu za mkononi duniani kutoa faida yake inayopatikana kutoka katika akaunti ya fedha kupitia simu za mkononi. Tangu mwaka 2014 kampuni imeweza kutoa zaidi ya Sh bilioni 81.8 katika riba ya robo mwaka kwa wateja wake,” anasema Karikari na kuongeza: “Hii ni mara ya 17 mfululizo ambapo Tigo imechangia riba kwa wateja. Ambao kila mmoja anapokea malipo kutegemeana na thamani ya fedha za kielektroniki walizozihifadhi katika akaunti zao za Tigopesa kuendana na matakwa ya Benki Kuu ya Tanzania.”

Anasema: “Utoaji huu wa faida ni kwa watumiaji wote wa huduma ya Tigopesa ikiwamo wateja binafsi, mawakala wa rejareja na washirika wetu wa kibiashara wote kwa kutegemeana na thamani ya fedha za kielektroniki zilizoko katika akaunti zao za Tigopesa.”

Wakati wote huo, kampuni imeweza kutoa jumla ya malipo yanayokaribia kufika thamani ya bilioni 50 kwa watumiaji wa huduma ya fedha kupitia simu za mkononi na kampuni haitaacha kuhakikisha mapato hayo yanawakilisha hali ya faida kwa wote.

Tigo Tanzania imeamua kuhusu utaratibu utakaotumika kutoa faida miongoni mwa wateja kutoka kwenye utoaji wa faida kutegemeana na salio la kila siku la wateja wa Tigopesa kuendana na waraka wa Benki Kuu ya Tanzania iliyotolewa Februari 2014.

“Tunashauku kubwa ya kutangaza ongezeko hili la gawio la faida kwa mara ya tisa mfululizo. Jambo hili linadhihirisha utayari wetu wa kutoa nafasi ya kufikia huduma za kifedha kwa wateja wetu nchi nzima kwa ujumla kupitia huduma zetu za Tigopesa,” anasema Karikari.

Hali ya soko iliyoboreshwa na ongezeko imara la idadi ya watumiaji wa Tigopesa ni sehemu ya vichocheo vya ongezeko la gawio la faida hususani kutoka kwenye sekta ya wafanyabiashara. Kwa sasa Tigopesa inamtandao mkubwa zaidi wa wafanyabiashara na mawakala nchi nzima.

Karikari anabainisha kwamba uwekezaji mkubwa wa Tigo katika upanuzi, uvumbuzi unaolenga mteja, teknolojia ya kidigitali ya kisasa na huduma nzuri kwa wateja imekuwa ni kichocheo kikubwa cha ongezeko la watumiaji na kutumia huduma ya fedha kwa njia ya simu za mkononi.

“Tigopesa imeweka juhudu katika agenda ya ushirikishwaji wa kifedha ya Serikali na inatengeneza zana mpya za kibiashara za kidigitali na kuandaa mazingira kuelekea katika mtindo wa maisha usiotumia fedha taslimu, kwa kupanua mfumo wake wa kifedha na kiuchumi, kuboresha ubora wa huduma zake na kutambulisha njia za kibunifu, zenye ufanisi kwa ajili ya wateja kufurahia huduma bora zaidi,” anaongeza Karikari.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here