24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JAFO AANZA KUKUNJUA MAKUCHA TAMISEMI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


WAZIRI wa Tamisemi, Selemani Jafo, amezitaka halmashauri 12 ambazo ni wadaiwa sugu wa fedha walizokopa katika Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, kurejesha fedha hizo.

Ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa haraka, Jafo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Richard Mfugale, kufuatilia wadaiwa wote ili wawasilishe fedha zao kabla ya Desemba 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Jafo, halmashauri hizo zinadaiwa zaidi ya Sh bilioni 2, zikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambayo ina deni kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jafo alizitaja halmashauri zingine kuwa ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mbeya, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Singida, Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Karatu, Pangani, Igunga, Kongwa na Halmashauri ya Mji Mbinga.

 “Kitendo cha namna hii katika urejeshaji mikopo kinanyima fursa halmashauri nyingine kupata mikopo. Kwa hiyo, naagiza bodi ifanye ufuatiliaji kwa wadaiwa wote kwa sababu madeni hayo ni ya muda mrefu.

“Siwezi kuridhika hata kidogo na utendaji wa chombo hiki kilichopo chini ya ofisi yangu, kiwe kinalegalega.

“Pamoja na madeni hayo, bodi yetu hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu, imefanikiwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 9.7 kwa halmashauri 54.

“Lakini, hadi sasa shilingi bilioni 6.57 ndizo zimesharejeshwa, jambo ambalo linanifanya nichukue hatua kwa wadaiwa sugu.

“Pamoja na kwamba baadhi ya halmashauri zinajitahidi kurejesha mikopo yao, halmashauri 12 zina usugu uliopitiliza kwenye urejeshaji mikopo,” alisema Jafo.

Kutokana na hali hiyo, waziri huyo aliitaka bodi hiyo kuangalia utaratibu wa kupitisha mikopo inayolenga katika ujenzi wa viwanda na uwekezaji katika halmashauri ili kukuza ajira na uchumi wa viwanda.

“Bodi iache kubweteka ijipange katika mkakati wa kujenga uwezo wa kutoa mikopo kwa halmshauri zilizo makini katika mapinduzi ya viwanda.

“Mtendaji mkuu wa bodi, tutapima utendaji wako wa kazi katika kusimamia bodi hii, sasa nataka bodi hii iwe chombo imara kitakacholeta tija kwa nchi.

Kwa upande wake, Mfugale alisema wameanza kuwasiliana na wahusika kuwajulisha juu ya mikopo yao kwa kuwa kila wanapochelewa kulipa, riba inapanda.

Pia, alisema bodi yake imeanza kuandikishiana mikataba mipya na wakurugenzi wa halmashauri hizo ili makusanyo yao ya ndani yaweze kulipa madeni yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles