IGP SIRRO: SITAKI KUZOZANA NA FAMILIA YA LISSU

0
2

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, amesema hataki malumbano na familia ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) anayeendelea na matibabu Nairobi Kenya, kwani jeshi hilo linafanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote na si kikundi cha watu fulani.

Kauli hiyo ya IGP Sirro imekuja siku chache baada ya familia yake kucharuka na kuwajibu viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Mkuu  huyo wa Polisi  na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita, familia ya mwanasheria huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ilionyesha kushangazwa na kauli za viongozi hao, huku wakitaka ndugu yao asifanywe kama mpira wa kona.

Kaka mkubwa wa Lissu, Alute Mughwa na mdogo wake, Vincent, walishangazwa pia kwa kitendo cha kuona mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na badala yake wanadai kumsubiri dereva wa Mbunge huyo, Simon  Bakari ambaye naye yupo Nairobi kwa matibabu ya kisaikolojia.

Walishangaa pia polisi kushindwa kumhoji dereva huyo akiwa Nairobi, ambapo Tanzania ina ubalozi ama kumhakikishia usalama wake ili aje kuhojiwa sehemu salama na si mahabusu kama mhalifu.

Akizungumza mjini Mbeya jana, IGP Sirro baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu jeshi hilo kushindwa kuwakamata watuhumiwa waliomshambulia mbunge huyo, alisema kwa sasa hana jibu na hayuko tayari kuingia kwenye malumbano na familia ya Lissu.

“Kwa hili sina jibu kwa sababu sitaki malumbano, jeshi lipo kwa ajili ya Watanzania wote na ndio maana nchi ipo shwari, kama kuna mtu anafikiria hivyo.

“… na mimi ndio mkuu wa jeshi la polisi nawajibika kwa raia na mali zao kwa kuhakikisha zinakuwa salama na kwa kweli ni salama hivyo kwa swali lako sina jibu,” alisema

Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama, alisema bado kuna changamoto ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina pamoja na mauaji ya watu wanaojifanya wana hasira kali.

IGP Sirro alisema kwa sasa wana mpango wa kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na imani za kishirikina, huku akiwaomba wanasiasa na viongozi wa dini washiriki katika kuwaelimisha wananchi kuachana na mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.

Aidha, aliwaonya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kwa kukwepa kulipa kodi, ambapo alisema jeshi hilo litawashughulikia kwa mujibu wa sheria ili waweze kulipa kodi halali ya Serikali.

Akizungumzia mapamabano dhidi ya dawa za kulevya, alisema biashara hiyo imepungua kwa kiasi  kikubwa tangu operesheni ya kuwakamata wauzaji na watumiaji ianze nchini.

IGP Sirro aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kuwataja wahusika bila kujali cheo au nafasi ya mtu  na kwamba taarifa hizo watoe kwa mtu wanayemwamini ili sheria ichukue mkondo wake katika kuwashughulikia wahusika wote.

Kadhalika Sirro alisema wahamiaji haramu wengi wamekuwa wakikamatiwa mkoani Mbeya kwa sababu ni sehemu ya kutokea kwenda nchi za kusini.

“Wengi wanapita katika njia zisizo rasmi na si wote wanaosafiri katika mabasi, wapo wanaotumia bodaboda, hivyo ni vigumu kuwakamata,” alisema Sirro.

Dereva wa Lissu

Akizungumzia kauli ya Sirro wiki iliyopita Dar es Salaam, kaka wa Lissu, Alite Mughwai, alisema: “Nimeona kwenye magazeti ya leo yakimnukuu IGP Simon Sirro akizungumzia habari za dereva wa Lissu  aliyeko Nairobi nchini Kenya kwamba arudi nchini ili aje ahojiwe … Ushauri wa familia ni kwamba kwanini Polisi msifuate kule Nairobi?

“Na kama hao watu walivyofyatua risasi zingewapata wote wakafa, je, polisi wasingefanya uchunguzi wao? Na kama ambavyo tunaambiwa hao wahalifu hawajakamatwa, si maisha yake (dereva) yatakuwa hatarini?

“Kuna utaratibu wowote juu ya kuhakikisha usalama wake? Isije ikawa anavuka pale Namanga tukasikia kakatishwa pale njia, kwahiyo kama watahitaji kwenda kumchukua, busara inaelekeza kwamba anapaswa kuhifadhiwa.

“Anapaswa kuhakikishiwa usalama wake kwanza, ndiyo aletwe huku kwa mahojiano na si kumweka mahabusu kwa sababu yeye ni shahidi tu,” alisema Mughwai.

Naye Vincent akimzungumzia dereva huyo, alisema: “Dereva wa Tundu Lissu ni kama mtoto wake kwa sababu alianza kufanya naye kazi akiwa mdogo, kwa hiyo amekulia pale kwa miaka 25, kwa hiyo ni mtoto wake, anakula na kulala kwake, sasa mambo haya yametokea ameathiriwa.

“Na Sirro kusema anasubiri mtu mmoja zoezi limesimama au labda zoezi linaendelea, lakini sisi kama familia tunaona hakuna umakini kwa sababu mtu alitaka kuuawa, mtu mwenye mchango mkubwa nchini hata kama ni upande wa pili jambo hili haliendi kama inavyotakiwa, ndiyo maana tunashauri washirikishwe watu kutoka nje.”

Afya ya Lissu

Akizungumzia hali ya Mbunge huyo, Alute alisema mbunge huyo anaendelea vizuri na afya yake inazidi kuimarika.

“Amefanyiwa upasuaji mara kadhaa na ameanza kula kwa njia ya kawaida, pia anazungumza vizuri,” alisema.

Uchunguzi wa tukio

Akizungumzia uchunguzi wa tukio la Lissu kupigwa risasi Septemba 7, nyumbani kwake Dodoma, Mughwa alisema familia imeshaandika barua serikalini kuomba uchunguzi wa tukio hilo ufanywe kwa kina, haraka na kitaalamu.

Mwisho

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here