HAKIELIMU YACHANGIA SHULE MIL 20/-

0
7

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

Shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu limetoa msaada wa Sh milioni 20 kwa ajili ya kuondoa changamoto ya muda mrefu ya tatizo la maji katika Shule ya Sekondari Mukulat, iliyopo wilayani Arumeru, mkoani hapa.

Akikabidhi hundi ya kiasi cha fedha hizo katika mahafali ya 20 ya kidato cha nne shuleni hapo, Mkurugenzi wa Shirika hilo, John Kalaghe, amesema wao kama wadau wa elimu wameguswa kusaidia kuondoa changamoto hiyo huku waathirika wakubwa wa tatizo hilo wakiwa ni wanafunzi wa kike.

Amesema takwimu za serikali za mwaka jana zinaonyesha asilimia 40 ya shule za msingi ndizo zenye miundombinu ya maji huku shule za sekondari asilimia 56 zina miundombinu ya maji.

“Sisi kama marafiki wa Shule ya Muklat na wadau tumeguswa tumeona tuna nafasi ya kuwajibika kutoa  mchango wetu, ili kuboresha elimu.

“Lakini pia watoto wa kike wanakumbana na changamoto nyingi katika kupata elimu ambapo Hakielimu katika mpango mkakati wetu wa miaka mitano, kuanzia mwaka huu, tutalipa kipaumbele suala la elimu ya mtoto wa kike,” amesema.

Aidha, kuhusu maendeleo ya wanafunzi wa kike amesema takwimu za serikali zinaonyesha mwaka 2015 watoto wa kike 69,067 waliachishwa shule na kati yao 3600 waliachishwa kwa sababu ya mimba, wengine utoro na kuwa taifa linapaswa kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wa kike wanaondikishwa kuanza shule wanamaliza.

“Takwimu zinaonyesha asilimia tano hadi sita ya watoto wa kike wanaomaliza kidato cha nne wanaendelea na kidato cha tano, huku watoto wa kiume asilimia 12 hadi 13 wanaomaliza kidato cha nne huendelea na kidato cha tano,” amesema Kallaghe.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here