DC ATUPWA NJE UJUMBE MKUTANO MKUU CCM TAIFA

0
1

Na ABDALLAH AMIRI-IGUNGA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, kimewapata viongozi wapya akiwemo mwenyekiti mwanamke na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano, huku Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, akishindwa kuchaguliwa kwenye nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho Taifa.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika Jimbo la Manonga wilayani hapa, ukihudhuriwa na wajumbe 1,174 lakini ni kura 1,169 za wajumbe zilizokuwa halali huku tano zikiharibika, ambapo Regina Thadeo, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Ally Mnyimvuwa, alimtangaza Regina, kuwa mshindi wa uchaguzi huo baada ya kupata kura 661 dhidi ya wapinzani wake, Idd Moshi aliyepata kura 441 na Daniel Bugota aliyepata kura 67.

Kashaga Anwar, alichaguliwa kuwa Katibu wa Siasa na Uenezi baada ya kupata kura 98 kati ya kura 156 zilizopigwa akiwabwaga washindani wake, Makongoro Ramadhani, aliyeambulia kura 31 na Majilanga Selemani, aliyepata kura 27.

Kwa upande wa nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho Taifa, jumla ya wagombea 10 walijitokeza akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, lakini hakufanikiwa kuchaguliwa baada ya wapiga kura kuwachagua Abubakar Shaban, Kwandu Chugu na Kapaya Hilda.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Costa Olomi, alisema  amekiacha chama hicho kikiwa safi na salama ambapo alitoa wito kwa viongozi waliochaguliwa kumpa ushirikiano mwenyekiti mpya ili ifikapo mwaka 2020 chama kiweze kushinda kwa kishindo kwa kuwa wananchi bado wanakiamini kutokana na utendaji wake mzuri.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here