‘BIRTHDAY’ YA MAJAY YAMRUDISHA LULU INSTAGRAM

0
1919

Bethsheba Wambura na Elizabeth Joachim, Dar es Salaam


Muigizaji maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, ametupia kwa mara ya kwanza katika ukurasa wake wa Instagram ujumbe wa kumtakia heri ya kuzaliwa mpenzi wake Francis Shiza ‘Majizo’ tangu atoke gerezani.

Lulu alitoka gerezani kwa msamaha wa Rais Mei 14, mwaka huu kwa kubadilishiwa kifungo kutoka cha miaka miwili na kuwa kifungo cha nje ambapo alitakiwa kufanya kazi za kijamii kifungo kinachomalizika Novemba 18, mwaka huu, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Steven Kanumba.

Katika ujumbe wake Instagram, Lulu aliambatanisha picha mbili moja ikimuonesha akiwa na Majizo wakiwa wamevaa suti na nyingine iliyounganishwa picha mbili ambayo moja ilimuonyesha Majay au Majizzo akiwa mvulana mdogo ameinama kwenye maua na nyingine inaonekana imepigwa si siku nyingi.

Ujumbe wa Lulu uliandikwa maneno ya Kiswahili na Kiingereza ukisema; “Mpenzi, rafiki, mfanyabiashara mwenza, wa kufa na kuzikana na sehemu pekee ya kuegemea siku zote, ahsante kwa kunionesha upendo wa Agape (Kiungu), baraka zikufuate siku zote za maisha yako, heri ya kuzaliwa Baba G… Nakupenda,” amendika Lulu.

Baada ya kutupia ujumbe huo, watu wengi ‘walicomment’ walifurahia Lulu kuandika tena ujumbe kwenye ukurasa wake huo ambapo miongoni mwa watu waliocomment alikuwa muigizaji Wema Sepetu ambaye alimtakia heri Majizo huku akimuita shemela (shemeji).

“Heri ya kuzaliwa kwako shemela, kasi naomba iendelee na vile vipande vyetu pambe vya video viendee na natumai hutalegeza kamba,” ameandika Wema.

Lulu amekuwa kimya tangu Oktoba 22, mwaka jana kabla hajakwenda gerezani, ambapo ujumbe wake wa mwisho kutuma aliweka picha aliyovaa kitenge chenye rangi ya njano na maua meusi na meupe, viatu vyeusi na kichwani akiwa amesuka mtindo wa ‘yeboyebo’.

Katika ujumbe wake siku hiyo aliandika maneno machache akimtambulisha mwanamitindo aliyembunia nguo yake hiyo, Saleh Hamimu.

“Dressed by Talented @officialsalehhamimu,” aliandika kwa kifupi Lulu pia akimtambulisha aliyemsuka nywele zake.

Lulu amejizolea umaarufu katika mtandao wa Instagram, kutokana na mara nyingi kutupia picha au video akiwa amependeza.

Lulu ni miongoni mwa wasanii wachache wanaojua kupangilia mavazi yao, lakini pia kutokana na uhusiano wake na Majay ambao huwavutia wengi.

Aidha, Lulu pia amejizolea umaarufu katika tasnia ya filamu tangu akiwa na umri mdogo ambapo alianza kuigiza akiwa katika Kundi la Kaole (Kaole Sanaa Group) na ndipo jina la Lulu lilikozaliwa na kuzoeleka hadi leo kuliko jina lake halisi.

Novemba mwaka jana alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia Kanumba, Aprili 12, mwaka 2012, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here