Imechapishwa: Sat, Oct 7th, 2017

BANDA: SOKA LA NJE LIMENIPA UJUZI ZAIDI

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

BEKI wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Abdi Banda, anayecheza soka la kulipwa Afrika Kusini kwenye klabu inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, Baroka FC, amesema kucheza nje ya nchi kumemsaidia kukuza kiwango chake.

Banda alisajiliwa na Baroka msimu huu baada ya kufuzu majaribio akitokea klabu ya Simba, mara baada ya kumaliza mkataba wake.

Tangu mchezaji huyo asajiliwe na klabu hiyo licha ya kuchezea nafasi ya beki, amefanikiwa kufunga bao moja kati ya michezo mitano waliyocheza, ambapo timu yake inaongoza ligi kwenye msimamo ikiwa na pointi 15.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Banda alisema tangu ameanza kucheza nje ya nchi ameweza kujifunza mambo mengi kutoka huko, hali iliyopelekea kiwango chake kuongezeka tofauti na alivyokuwa Tanzania.

“Mpira wa Afrika Kusini upo juu tofauti na Tanzania hivyo imenisaidia kipaji changu kukua zaidi tofauti na nilivyokuwa nikicheza timu ya Simba,” alisema Banda.

Alisema anajitahidi kutumia nafasi yake vizuri ili azidi kung’ara kwenye timu yake ya Baroka na Taifa Stars ili azidi kuitangaza vema Tanzania.

“Timu za nje hakuna kulala, unatakiwa kupambana na kujituma ili kiwango kizidi kuongezeka na mimi nitajitahidi kupambana kila nitakapopata nafasi ya kucheza ili kumshawishi kocha azidi kuniamini,” alisema.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

BANDA: SOKA LA NJE LIMENIPA UJUZI ZAIDI