Askofu Bagonza aonya wanaotesa watu

0
555
  • Akemea tabia ya kugeuza wengine watumwa

WAANDISHI WETU -DAR, SOGEA

VIONGOZI wa dini katika makanisa mbalimbali nchini jana walitumia ibada ya Ijumaa Kuu kutoa ujumbe mzito, wakikemea utesaji, utumwa, matumizi yasiyofaa ya simu ambayo yameziweka ndoa nyingi shakani na kuhubiri amani, uhuru, upendo na kujitoa kwa ajili ya wengine.

Akitoa salamu za Ijumaa Kuu katika Ibada ya Kitaifa iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT) Usharika wa Lukajange, Karagwe mkoani Kagera, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Karagwe, Dk. Benson Bagonza, alisema siku ya jana ni ya kukumbuka mateso na kifo cha Yesu, ambayo ndiyo msingi wa dini ya Kikristu.

Alisema binadamu huwa hawapendi mateso kama ya Yesu, lakini wakilazimika sana huwa wanapenda kuwatesa wengine na si kuteswa.

“Sisi binadamu hatupendi   mateso, kama tukilazimika sana tunapenda kuwatesa wengine, lakini si kuteswa, kukwepa mateso ni ishara ya ushupavu na ushujaa, usimtese mtu kwa sababu Bwana Yesu aliteswa, ukifanya hivyo unamgeuza mtu huyo kuwa Bwana Yesu, kwa hiyo si sawa, mara nyingi watesaji jambo hili hawalijui,” alisema Askofu Bagonza.

Alisema utesaji ni kama bangi, ikishaingia mwilini unajenga mazoea ya kupenda kutesatesa  watu na usipowatesa unajisikia kuwashwa washwa na kwamba ndivyo ilivyokuwa kwa watu wa Kiyahudi.

Akitoa mafundisho ya upendo na upatanisho, aliwataka watu kuwa na tabia ya kujitoa kwa ajili ya wengine, kuanzia kanisani hadi  katika ngazi ya Taifa.

“Tujitoe kwa ajili ya wengine, kujitoa na kujitolea ni mambo ambayo yanazidi kupotea katika kanisa letu na hata ndani ya Taifa letu, siku hizi kila kitu ni fedha, nawasihi ndugu zangu tujitoe, tujitoe muda wetu na mali zetu  katika kulitumikia kanisa na Taifa.

“Kutoa na kujitoa ni ibada kamili, ikifanyika kwa usahihi na mwongozo kwa kufuata Biblia vinaongeza thamani yetu kwa Mungu, Bwana Yesu alitoa damu yake isiyo na hatia ili kutukomboa sisi.

“Nakumbuka nikiwa kijana wakati nasoma shule ya msingi hapa Karagwe tulihamasishwa kutoa damu kwenda Msumbiji  tuliambiwa inaenda Msumbiji kumkomboa ndugu yangu, sijasahu hadi leo thamani ya damu katika uhusiano na upatanisho, ni kubwa sana kuliko unavyodhani,” alisema Askofu Bagonza.

Mbali na hilo, Dk. Bagonza pia aliwataka waumini wa Kikristu kuonyesha tofauti ya watumwa waliokombolewa na waliopo utumwani.

Alisema watumwa waliokombolewa huwa ni watu huru wenye shukurani, wana furaha, wanajiamini, wanachukia utumwa hata wakiwa huru hawafurahi kuwaona wengine wakiwa bado utumwani.

“Kukombolewa halafu wewe ukawa mfuga watumwa ni jambo la aibu mno, kuna tabia moja ya kuzoea utumwa, tabia mojawapo ya mtu kuzoea utumwa ni kupenda kubaki utumwani, ya pili kupenda kumiliki watumwa, ndugu zangu nayasema haya kuwaeleza kuwa ukombozi unaotokana na kifo cha Bwana Yesu pale msalabani unatutaka sisi sote tuwe chachu ya kupenda uhuru sisi wenyewe na kwa wengine pia.

“Hapa kwakuwa naongea na Watanzania wote niseme tu kwa ufahari tunu moja tuliyobarikiwa kuwa nayo katika Taifa hili chini ya uongozi wa Baba wa Taifa ni pale tulipotangaza kuwa uhuru wetu hauna maana kama bado kuna nchi nyingine zipo utumwani, tukaona uhuru si kamili, tukatumia rasilimali nyingi kuwasaidia jirani zetu waondokane na ukandamizaji, ukoloni na utumwa, sisi wa Mkoa wa Kagera,” alisema Askofu Bagonza.

Alisema anakumbuka jinsi Taifa lilivyoingia gharama kubwa kuingia vita kupinga udikteta katika nchi ya jirani.

“Ulituhusu nini ule udikteta, sisi hatukuwa na dikteta hapa, tulikuwa tunaishi vizuri, lakini kwa sababu tuliona jirani kuwa katika shida si sawa na sisi tukaingia katika gharama, hii ni sawa na kuteseka kwa Yesu, tumtii aliyetukomboa.

“Anatuagiza tushike amri zake ambazo zinatuweka salama kwa kutokomboa sisi, si yeye, wapo watu wanaodhani kwa kukataa kukombolewa wanamkomoa anayemkomboa.

“Katika somo la leo, cha kwanza tupendane kwa sababu ni watumwa tuliokombolewa, wewe na mimi wote ni watumwa waliokombolewa, tufurahie ukombozi, tuuchukie utumwa,  tusitamani kurudi huko, tuishi maisha ya shukurani kwa mkombozi wetu, ndugu zangu mfano wewe umeiba unakimbia na kupepea kakamatwa mtu mwingine ambaye hajaiba  anahukumiwa kuuawa, wewe unaangalia tu na kuchekelea unaona inakuja, unafikiri ni ujanja?” alisema Bagonza.

Mbali na hilo, Askofu Bagonza pia alizungumzia kuhusu umwagaji damu, akisema damu ya mwenye haki haimwagiki bure  na kwamba isipokomboa itaangamiza.

“Damu yenye haki kama ya Yesu ikishamwagika kwa sababu ni damu ya mwenye haki  isipokomboa inaangamiza, tuwe macho sana kwa sababu  kutukuza, kushabikia, kukalia kimya au kukumbatia umwagaji wa damu usio na hatia kuna madhara kwetu sisi na kwa vizazi vijavyo, kazi ya damu ya mwenye hatia ni kukomboa na kutakasa, isipofanya hivyo inaangamiza, waweza usiangamie wewe uliyeshiriki, unayeshabikia, unayekaa kimya wakaja kuangamia uzao wako au Taifa lako na hao hawana hatia kwa sababu hawakuwepo wakati unashabikia umwagaji damu usio na hatia,” alisema Askofu Bagonza.

Wakati Askofu Bagonza akisema hayo, kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea, Damian Dallu, amewataka waumini wa kanisa hilo kuendelea kuilinda imani kwa kuyahubiri mema na si kufanya kama walivyofanya Petro na Yuda.

Akihubiri kwenye ibada ya Ijumaa Kuu, Askofu Dallu alisema kipindi cha miaka ya karibuni Wakristu walipita katika wakati mgumu wa kiimani, lakini waliyashinda majaribu kwa kuendelea kuhubiri amani na kumtangaza Kristo.

“Katika kipindi hicho kigumu baadhi yao walimkumbuka Petro na kusema tuchomoe na sisi upanga uliorudishwa alani mwa Petro, lakini wengine walisema hapana, bali tusimame katika imani,” alisema Askofu Damian Dallu.

Alifafanua kuwa baadhi ya wanafunzi wa Yesu, akiwamo Petro, hawakutambua kuwa Yesu Kristo hulindwa kwa imani na ndiyo maana alichomoa upanga alani mwake na kumkata sikio mmoja wa maadui, huku Yuda akipokea vipande vya fedha kutoka kwa makuhani kwa maslahi yake, jambo ambalo kiimani haikutakiwa.

 “Ni mambo ya ajabu kwa Mkristo wa Kanisa la Katoliki kuwa waoga kuhubiri ukweli uliopo kwa kuogopa kufanyiwa vibaya na baadhi ya watu wenye nia mbaya, hali hiyo haitakiwi kwa kuwa mbaya yeyote akimzuru kiongozi wa dini siyo kwamba ameliuwa kanisa au Ukristo, bali Kanisa litazidi kusonga mbele,” alisema Askofu Dallu.

Naye Mkurugenzi wa Utume na Familia, Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Padri Novatus Mbaula, ameishauri jamii kupunguza matumizi ya simu za mikononi ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia mafarakano kwa wanandoa na jamii kwa ujumla.

Akitoa mahubiri ya Ijumaa Kuu katika ibada iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Jijini jana iliyohudhuriwa pia na Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, Padri Mbaula alisema binadamu wamekuwa na kiburi na majivuno kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii na kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo, hali ambayo inamchukiza Mungu.

“Wanadamu wamejaa viburi kiasi ambacho kimesababisha mifarakano kwa baadhi ya wanandoa, huku muda mwingi wakitumia kwenye mitandao ya jamii kupitia simu za mikononi bila kuwaza athari ambazo zinaweza kutokea, hali ambayo imesababisha kuongezeka kwa migongano na mifarakano baina yao,” alisema Padri Mbaula.

Alisema kiburi na majivuno, hayawasaidii chochote katika maisha, zaidi ya kujitenganisha na upendo wa Mungu.

Zaidi alionya vitendo vya imani za ushirikina, dhuluma kwa mazao ya wakulima, wastaafu na watu wanaotengwa na kukandamizwa katika jamii ya sasa, ambavyo kwa sasa alidai  vimeongezeka.

Alisema kitendo cha kukumbatia mambo ya ulimwengu bila ya kuwa na hofu ya Mungu kunasababisha jamii nyingi kuporomoka.

Zaidi alizungumzia hulka ya kujikweza na kujitukuza kuliko kujishusha na kujiona dhaifu mbele za watu, kunachangia kuongezeka kwa chuki.

“Binadamu wameacha kumtolea Mungu sadaka, badala yake wanaishi maisha ya kujikweza na kujitukuza bila kuwa na hofu, wakati umefika wa kila mmoja kujifikiria na kutafakari yupo kwenye kundi gani ili aweze kurudi na kutubu, jambo ambalo linampendeza Mungu,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, waamini wanapaswa kukumbatia haki na mapatano katika jamii wanazoishi ili waweze kuongeza wema na amani, huku wakiwa na upendo ambao utasaidia kuboresha amani kati yao.

Katika mwelekeo huo huo, naye Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Chediel Luiza, alisisitiza upendo pamoja na kusamehe.

Akitoa mahubiri hayo katika Kanisa la Azania Front, Jijini Dar es Salaam, Mchungaji Luiza mbali na hilo, alisisitiza kuwa kuna wakati viongozi wanachonganishwa, raia wanachonganishwa, lakini msamaha ndio unaotakiwa.

“Viongozi wakichonganishwa wakashindwa kutenda haki wanakosea,” alisema Mchungaji Luiza.

Pia Mchungaji Luiza alisema  thamani ya mtu inapaswa kutunzwa kama maandiko yanavyosisitiza, watu wasiteswe, wasiuliwe, bali utu utunzwe.

“Unaangalia taarifa ya habari watu wanateswa huko nje ya nchi, wamechoshwa na viongozi,  lakini Yesu anatufundisha kusamehe,” alisema Mchungaji Luiza.

Alisema mateso ya Yesu Msalabani yasitumike kama kigezo cha watu kuteswa, kwasababu ya imani zao na misimamo, ni ishara ya ukombozi.

Alisema mateso hayo yanakumbusha pia kutimiza wajibu kama Yesu alivyomkabidhi mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda ambaye naye alitii.

Alisema haijalishi unazungumzwa vibaya, unasemwa, lakini ibada ya misa ya Ijumaa Kuu inakumbusha kuwa upendo hushinda hayo.

Habari hii imeandaliwa na AZIZA MASOUD, PATRICIA KIMELEMETA Na AGATHA CHARLES

(DAR), AMON MTEGA(SONGEA)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here