25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda sasa kufikishwa mahakamani

makondaNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, ametangaza kumfikisha mahakamani Mkuu mpya wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, baada ya kushindwa kuomba radhi kutokana na kashfa alizozitoa dhidi yao.
Guninita alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wake na waandishi wa habari,uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Makonda kuandikiwa barua Februari 12 mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine ilimpa wiki mbili kuomba radhi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutokana na kauli yake ya kuwaita Guninita na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai kuwa ni“vibaraka”wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Zaidi Guninita alimtaka Rais Jakaya Kikwete kumuengua Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Kinondoni kwasababu ya kukosa uadilifu.
Kwa mujibu wa Guninita, uadilifu ambao Makonda ameukosa na unamuondolea sifa ya kuwa kiongozi, ni tabia yake ya kutukana na kupiga viongozi jambo alilosema kuwa linakibomoa chama.
Guninita ambaye alikuwa ameambatana na mwanasheria ambaye atasimamia kesi hiyo, Benjamin Mwakagamba kutoka katika Kampuni ya BM Attorneys, alisema kutokana na kuwapo kwa utawala wa sheria nchini, hivyo ni wajibu wa viongozi na wananchi kuheshimu na kutii sheria.
“Hakuna mtu ndani ya nchi hii yuko juu ya sheria anayeweza kumtukana mwenzake au kumpiga ngumi bila ya sababu yoyote asichukuliwe hatua za kisheria eti kwasababu yeye ni kiongozi na anafanya hivyo kwa kutumiwa na chama,”alisema Guninita.
“Tulimtaka aombe radhi baada ya kupata barua cha kushangaza Makonda alitujibu kuwa ametumwa na chama na alikuwa anafanya kazi ya chama na yuko katika kazi ya kulinda na kujenga Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo hawezi kuomba radhi wala kufuta maneno yake.
“Makonda hawezi kulinda chama kwa matusi na mangumi, hivyo anapaswa kukumbuka kuwa hata Jaji Joseph Warioba ni mwana CCM kwasababu hiyo alipaswa kumheshimu na kutambua kuwa wapo waliowekeza jasho lao kwenye chama kwa zaidi ya miaka 40 si yeye ambaye bado ni mchanga,”alisema.
Alisema siasa ya karne hii hoja humalizwa kwa hoja si matumizi ya ngumi,hivyo inashangaza kumuona Makonda akijenga chama kwa ngumi alizompiga Warioba, utaratibu ambao alisema hauwezi kujenga chama bali kukibomoa.
Kutokana na mwenendo huo, alisema Makonda amebadili Umoja wa Vijana wa CCM kuwa ulingo wa ngumi na si chuo cha maadili.
Alisema kama suala hilo halitaangaliwa linaweza kuwa ni chanzo cha kupata viongozi wa aina ya Makonda ambao hawawezi kuienzi misingi ya siasa alizoziacha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alisema nchi nyingi duniani zinazoingia katika machafuko ya kisiasa ya wenyewe kwa wenyewe viashiria vyake huanzishwa na viongozi wanaofanana na Makonda.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mwakagamba ambaye ni miongoni mwa watakaofungua kesi hiyo Machi 2 mwaka huu, alisema sababu ya kufikia hatua hiyo inatokana na kuwapo kwa udhalilishaji.
“Kutokana na kauli yake iliyokuwa ikisema kwamba yupo mtu anayewatuma watu na kasha kuwataja majina watu hao kisheria ni maneno yanayodhalilisha,”alisema.
Makonda ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya, mbali na kuingia kwenye mgogoro na wanasiasa wenzake hao, pia amejikuta katika upinzani mkali kutoka kwa watu wanaopinga uteuzi wake.
Baadhi ya watu wanaompinga wanamshutumu Makonda kwa kukejeli, kuwatusi na hata kudaiwa kuwapiga viongozi wa chama hicho.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema kiongozi huyo licha ya kushutumiwa kwa utovu wa nidhamu ni kijana mzuri anayefaa kushika ukuu wa wilaya.
Sambamba na hilo, pia alisema wale wote wanaohoji na kupinga busara iliyotumika kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni wanapiga porojo hivyo wasubiri siku watakapobahatika kuingia Ikulu nao wateue watu wanaowataka kushika nafasi ya uongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles