25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Aangusha ng’ombe watatu kusherehekea uwaziri

mwijageNa Elizabeth Mjatta
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, anadaiwa kuandaa ng’ombe watatu ambao watachinjwa leo kwa ajili ya kusherehekea kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Mwijage, ambaye ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika nafasi hiyo Januari 24, mwaka huu, baada ya kufanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri baada ya kuibuka sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka eneo la Kamachumu, Muleba ambako mapokezi hayo yatafanyika leo, zinasema kuwa mbali na ng’ombe hao, pia kutakuwa na maakuli ya kila aina.
“Maandalizi yanaendelea, ingawa baadhi ya wananchi wamekataa kushiriki, hali iliyosababisha waandaaji kutumia wanafunzi katika maandalizi hayo, kwa mfano wanafunzi waliotumika kuchagua mchele ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Kamachumu B.
“Lakini pia wamechukua tena wanafunzi wa Sekondari ya Rutabo, ndio walikuwa wanashughulika kufanya usafi na kujenga jukwaa atakalotumia Mwijage kuzungumza na wananchi,” alisema mtoa taarifa wetu huyo kutoka Kamachumu.
Alisema waandaaji wa mapokezi hayo ambao ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Kamachumu, walifikia hatua ya kuwatumia wanafunzi baada ya kukosa ushirikiano sehemu mbalimbali.
“Ilifika mahali hadi wakataka kwenda kutoa mahabusu kinyemela ili wawasaidie kufanya usafi na wananchi wamekataa kushiriki kwasababu Mwijage amefiwa na mama yake mdogo aliyemlea hivi karibuni lakini hajashiriki mazishi, sasa watu wanashangaa anajiandalia sherehe ya mapokezi,” alisema mtoa taarifa huyo.
Katika kunogesha mapokezi hayo, miongoni mwa waratibu katika shughuli hiyo ni yule aliyepewa jukumu la kushughulikia magari ambapo amekuwa akipita kwa baadhi ya watu wenye magari ili kuwashawishi washiriki katika mapokezi ya Naibu Waziri huyo.
Baadhi ya wenye magari wamekuwa wakiambiwa kwamba watawekewa mafuta endapo watashiriki kwenye shughuli hiyo.
MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na Katibu wa CCM Kata ya Kamachumu ambaye simu yake iliita bila kupokelewa.
Ofisa Mtendaji Kata ya Kamachumu, George Rugangila, alithibitisha kuwepo kwa maandalizi hayo, lakini alikataa kuzungumza kwa undani kwasababu yeye siyo mhusika mkuu.
Alipoulizwa kuhusu ushiriki wa wanafunzi katika maandalizi hayo, alikiri kuwaona, lakini alidai walikuwa wanakwenda kucheza shule ya jirani.
“Kweli niliona kundi kubwa la wanafunzi wanapita katika eneo hilo, lakini niliona wanakwenda kwenye shule ya jirani ya Ibuga, siyo kweli kwamba walikuwa wanajenga majukwaa,” alisema Rugangila.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Rutabo alipopigiwa simu kuthibitisha taarifa hizi simu yake haikupatikana.
Kwa upande wake, Waziri Mwijage alipotafutwa kwa njia ya simu kupitia ujumbe mfupi wa maneno alijibu kuwa; “Salaam, nipo kwenye kikao Mwanza”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles