29.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Muhongo agoma kuzungumzia urais

profesa MuhongoNA EVANS MAGEGE

SIKU chache baada ya wazee wa Wilaya ya Musoma, na jana tena baadhi ya viongozi wa mashina na matawi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dar es Salaam kumtaka aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, achukue fomu ya kuwania urais, mwanasiasa huyo amesema hataki kujisumbua kuzungumzia mambo ya urais kwa sasa.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu katikati ya wiki hii kuhusiana na tamko hilo, Profesa Muhongo, licha ya kukiri wazi kuwa amesikia taarifa hizo kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii, lakini alishindwa kutanabahisha kama anayo nia ya kugombea urais mwaka huu.
“Nimesikia hata wanafunzi wa vyuo vikuu wakitoa tamko la namna hiyo, lakini nyie si mna mtu wenu mnayemjengea hekalu?Kwa hiyo hata nikiwaambia mambo ya urais kwa sasa nitakuwa najisumbua bure, niacheni nipumzike,” alisema Profesa Muhongo.
Hata hivyo, gazeti hili lilidokezwa juu ya kile kinachoitwa mkakati uliokuwa nyuma ya tamko la wazee hao wa Musoma, kwamba liliratibiwa na kijana mmoja aliyetajwa kwa jina la Peter Haule.
Gazeti hili limebaini kuwa mkakati huo ulikuwa ni mpango wa Profesa Muhongo mwenyewe kupima kina kuona kama anaweza kujitosa kwenye siasa kupitia mgongo wa wazee hao wa Musoma.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, mmoja wa wajumbe wanaounda umoja wa wazee wa Musoma (jina tunalo), alidokeza kuwa tamko lao linatokana na msukumo wa Haule, aliyedai kuwa ameagizwa na Profesa Muhongo awaambie wazee hao watoe tamko la kumtaka mwanasiasa huyo achukue fomu ya kuwania urais.
“Sisi wazee tuliitwa na mwenyekiti wetu wa muda, ambaye alituambia kuna ujumbe kutoka kwa Profesa Muhongo, tulipokutana alitutambulisha kwa kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Haule, kijana huyo akatuambia kuwa ujumbe aliotumwa ni kutuomba tumuunge mkono Profesa Muhongo kwenye urais,” alisema.
Alisema kijana huyo ndiye aliyewasaidia kuandika tamko lao ambalo lilisambazwa kwenye vyombo vya habari.
Gazeti hili liliwasiliana na Haule kwa njia ya simu kuhusiana na jina lake kutajwa kuinjinia mkakati huo, lakini katika hali ya kushangaza alishtuka na kukata simu.
Hata hivyo, baada ya dakika chache, Haule alipiga simu mwenyewe na kukana kuhusika kwenye mkakati huo.
“Siku wazee walipotoa tamko nilipigiwa simu na rafiki yangu akiniambia nifuatilie taarifa ya habari ya TV, usiniguse, mimi ni mfanyabiashara, kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi,” alisema Haule.
Alipoulizwa msingi wa kupigiwa simu na rafiki yake huyo kumtaka afuatilie taarifa za wazee hao kutoa tamko la Muhongo, Haule alisema alifanya hivyo kwa sababu yeye ni mtu anayefuatilia siasa.
Jana baadhi ya viongozi wa mashina na matawi wa CCM jijini Dar es Salaam nao wameibuka na kutoa tamko la kumtaka Muhongo achukue fomu ya kugombea urais.
Wamesema, pamoja na kwamba kuna wagombea wengi wa nafasi hiyo kupitia CCM, Profesa Muhongo ndiye chaguo lao kwa kuwa wanaamini anaweza kuiongoza nchi na kuifikisha mahali pazuri.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho katika Kata ya Magomeni, Sadick Kadulo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
“Rais Kikwete alipokuwa akizungumza katika sherehe za CCM za kutimiza miaka 38 mjini Songea hivi karibuni, alisema tuwahamasishe wana CCM wenzetu wenye uwezo wa kugombea urais ili wagombee.
“Kwa hiyo, sisi tumetumia fursa hiyo kumuomba Profesa Muhongo agombee urais kwa sababu uwezo anao na hana woga wala hamung’unyi maneno pindi anapokuwa akitetea haki za wanyonge.
“Narudia tena, tunamuomba Profesa Muhongo popote alipo na kama anatusikia, muda wa kuchukua fomu ukifika, achukue na sisi tutamuunga mkono kwa sababu tunaamini ana uwezo wa kuiongoza nchi hii,” alisema Kadulo.
Kwa mujibu wa Kadulo, uwezo wa uongozi alioonyesha Profesa Muhongo wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini ni kielelezo kingine kitakachowashawishi Watanzania kumpigia kura za ndiyo pindi watakapotakiwa kufanya hivyo.
“Wakati akiwa pale Wizara ya Nishati na Madini alionyesha uwezo wa hali ya juu kwa kupeleka umeme vijijini pamoja na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.
“Kwa mfano, aliruhusu vijana wa Kitanzania kwenda kusomea masuala ya mafuta na gesi na aliwezesha mikataba kati ya wizara yake na wawekezaji isainiwe hapa hapa nchini kwa manufaa ya Watanzania. Haya yote aliyafanya kwa sababu ana uchungu na nchi hii, ingawa baadaye alianza kupigwa vita na baadhi ya watu waliokuwa wakiitumia wizara hiyo kujinufaisha wao,” alisema.
Kabla ya kukumbwa na sakata la Escrow, Profesa Muhongo alihusishwa na mbio za kuwania ubunge katika Jimbo la Musoma Vijijini.
Harakati zake hizo zinadaiwa kusababisha mvutano mkubwa baina yake na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.
Ni mazingira hayo hayo ya kuwania Jimbo la Musoma Vijijini ndiyo yanahusishwa na uamuzi wa Profesa Muhongo wa kuvunja mkataba uliokuwapo baina ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kampuni ya kusimamia masuala ya kisheria ya Mkono & Co Advocates.
Hata hivyo, kufuatia kuwapo kwa mashinikizo ya muda mrefu ya kutaka ajiuzulu baada ya kuhusishwa na sakata la uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Profesa Muhongo aliamua kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa Nishati na Madini na kubaki katika nafasi yake ya ubunge wa kuteuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles