24.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

Waganga wakuu kikaangoni vifo vya uzembe

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imesema kuanzia sasa waganga wakuu wa mikoa na wilaya watakuwa ni watuhumiwa pindi itakapotokea vifo vya uzembe kwa wajawazito, watoto au mtu yeyote yule.

Maelekezo hayo yametolewa Novemba 20,2023 na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipofanya ziara katika Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Temeke na Mwananyamala.

Dk. Mollel ametoa maelekezo hayo ikiwa ni wiki moja imepita tangu kilipotokea kifo cha mjamzito Mariam Zahoro jijini Tanga kwa madai ya kukosa Sh 150,000 ili afanyiwe upasuaji.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, akikagua miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke. Kulia ni Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Joseph Kimaro.

“Rais ameshafanya kazi yake ya kuleta rasilimali kazi ni kwetu sisi kuzingatia ubora wa huduma, yanapotokea matatizo kwenye vituo vya afya halafu sisi tunatoka tunakwenda kule wanatakiwa wajitafakari.

“Tumechoka kubeba mizigo ya watu, kuanzia sasa DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya), RMO (Mganga Mkuu wa Mkoa) likitokea tatizo mama amefariki au mtoto amefariki na nyie ni watuhumiwa pamoja na aliyefanya kosa kwa sababu walitakiwa wawasimamie,” amesema Dk. Mollel.

Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajo, amesema wanaboresha mifumo iweze kusomana ili kuwapunguzia adha wananchi na kuhakikisha mgonjwa anahudumiwa ndani ya saa tatu tangu anapofika hospitali.

“Rais ameshawekeza vya kutosha deni tunalo sisi watumishi kuhakikisha tunatoa huduma bora, hospitali inahusu maisha ya watu hatutaki utani.

“Tunaamini mgonjwa akifika hospitali kuna mlinzi getini, walinzi wapewe mafunzo ya namna ya kupokea wateja…tunataka mgonjwa akiingia hospitali aanze kuona matumaini kuanzia getini,” amesema Profesa Rugajo.

Kwa mujibu wa Profesa Rugajo, uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya afya ambao unahusisha ujenzi wa miundombinu, kuongeza bajeti ya dawa na kufikia Sh bilioni 20 kila mwezi, kuendeleza watumishi katika ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi ambapo bajeti imeongezwa kutoka Sh bilioni 5 hadi 9.

Waganga Wafawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke (Dk. Joseph Kimaro), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyama (Dk. Zavery Benela) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana (Dk. Bryson Kiwelu), wamesema watazingatia maelekezo hayo na kuhakikisha ubora wa huduma unakuwa kipaumbele chao.

Dk. Kimaro amesema tayari wamejenga uwezo kwa watumishi wote 600 wa Temeke kwenye eneo la huduma kwa wateja na kwamba wanafanya mpango waweze kuwapatia mafunzo hayo watumishi wapya walioajiriwa karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles