29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko atoa maagizo TPDC

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kutengeneza mpango wa muda mrefu utakaowezesha uwepo wa hazina ya kutosha ya gesi asilia.

Dk. Biteko ameyasema hayo leo  Novemba  21, 2023  katika kikao chake na Bodi na Menejimenti ya TPDC ambacho kililenga kufahamiana, kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi na kuelekeza matarajio  ya nchi  kwa shirika hilo.

“Tutambue kuwa mahitaji ya gesi asilia ni makubwa kwa sasa kwani dunia inahama kutoka matumizi ya mafuta na kwenda kwenye gesi, hivyo lazima tujipange, pia tukumbuke tumesaini makubaliano ya kusafirisha nishati hii kwenda Uganda, Zambia na Kenya hivyo lazima tuwe na gesi ya kutosha,”amesisitiza Dk. Biteko.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame

Pia amewataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa mafuta na gesi ili sekta hiyo isirudi nyuma.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake, katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati mkoani Mtwara, amesisitiza kuwa, maisha ya wananchi katika maeneo hayo ambayo kuna visima na mitambo ya gesi asilia lazima yabadilike kwa kupewa huduma bora ikiwemo maji, umeme, afya na usafiri.

Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue

“Nashukuru mmeanza kufanyia kazi maagizo niliyoyatoa kwa haraka, ikiwemo ya kuweka taa za barabarani Kijiji cha Msimbati, kupeleka umeme wa uhakika Madimba na Msimbati unaotoka kwenye mitambo ya gesi asilia.

 “Kupeleka kivuko kisiwa cha Songosongo na malipo ya mafao kwa wastaafu wa ambao walikuwa wakilinda mitambo na visima vya gesi ambao hawakulipwa muda mrefu,” amesema.

Katika hatua nyingine, ameiagiza shirika hilo kupita kwenye halmashauri zote nchini zinazopokea ushuru wa huduma kutokana na shughuli za mafuta na gesi ili TDPC ijihakikishie kwamba, fedha hizo zinakwenda  pia kwenye  maeneo ambayo shughuli za uzalishaji  wa nishati hiyo zinafanyika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, amemueleza Waziri kuwa  wanandaa  mpango mkakati wa shirika wa miaka 10 ili kuwezesha upatikanaji wa gesi ya kutosha na kuchochea biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, ameeleza mipango ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania, Mradi wa Gesi ya Kusindika (LNG) ambapo majadiliano yamekamilika na mikataba ipo kwenye hatua za kuidhinishwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu kwa maelekezo yake ambayo yamewapa hamasa ya kufanya kazi kuahidi kwenda mbali kiutendaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles