28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, May 12, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAHOJI WANAOVUNJA MAADILI KUPANDA VYEO

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

BAADHI ya wabunge wametaka ufafanuzi  kutoka kwa Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Harold Nsekela  kwa kuhoji hatua ya baadhi ya viongozi wakiwamo wakuu wa wilaya wanaokiuka maadili kupandishwa vyeo.

Wabunge hao walihoji ni kwa nini aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti amepandishwa cheo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, wakati amedaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa kwa kununua madiwani wa Chadema.

Hayo waliyasema jana wakati wa semina ya maadili na udhibiti wa rushwa kwa wabunge iliyoandaliwa na Mtandao wa Wabunge Wanaopambana na Rushwa(APNAC) kwa kushirikiana na  Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Aliyekuwa wa kwanza kurusha kombora alikuwa Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema), ambaye alihoji kuhusu maadili ya viongozi wakiwamo wakuu wa wilaya wanaokiuka kanuni za utumishi na maadili na baada ya muda hupandishwa vyeo.

“Hapa katikati kulitokea purukushani nyingi tu lakini wengine tulikuwa hatuamini lakini huyo aliyekuwa akituhumiwa kwa rushwa ambaye ni kiongozi katika Serikali amesema hadharani na kwenye vyombo vya habari nadhani hata wewe unajua…

“Kwamba yeye anauwezo wa kununua madiwani hata wabunge na atahakikisha ananunua hata wabunge na huyo sio mwingine ni Mnyeti (Alexander) na amepandishwa  cheo wewe ukiwa kama Mwenyekiti wa Maadili  unasemaje kuhusu hilo, tutakuwa na amani gani kwa Tanzania kwa viongozi kama hao?,” alihoji.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema),  alisema Sekretarieti ya Maadili imekuwa ikishughulikia viongozi wadogo wadogo huku wakubwa wakiwaogopa.

Kwa upande wake Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM), alisema licha ya kujaza fomu za maadili lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya viongozi wanaoonekana kwenda kinyume na mahitaji ya fomu hizo.

“Baadhi ya viongozi walikula pesa na wakarudisha sasa  nyinyi viongozi wa maadili mmechukua hatua gani kwa hao viongozi nashangaa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti mmesema nyinyi mnasimamia maadili ya viongozi na kila mwaka tunajaza fomu na viongozi  wana majengo ya ajabu na wanajaza uongo katika hizo fomu.

“Mfano EPA  wengine wamerudisha fedha wengine hawajarejesha wanatanua tu na wengine wapo ndani kwa ushahidi,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Jaji Nsekela, alisema maswali aliyoulizwa sio ya maadili na angependa aulizwe masuala yanahusu maadili.

“Jambo  la kwanza lazima uangalie sheria inasemaje waheshimiwa wabunge tunapozungumzia maadili ni lazima mpate sheria mliyoitunga inasema nini, nadhani kwa hilo nimeeleweka.

Awali akifungua mkutano huo Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema wabunge wanatakiwa kupigwa brashi katika eneo la maadili kutokana na wananchi wengi kulalamika kuhusiana na maadili yao.

“Tutakubaliana na waheshimiwa wabunge katika eneo ambalo tunatakiwa kupigwa brashi ni wabunge wote ni katika eneo la maadili kwani tumenukuliwa na vyombo vya habari na wananchi wametulalamikia kwamba baadhi hatuna maadili,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles