24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

‘Tunataka mataifa yetu yakue kiuchumi kwa manufaa ya watu wetu’

*Ubalozi wa Kenya nchi Tanzania waadhimisha miaka 60 ya Uhuru

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imebainisha kuwa nchi ya Kenya ndiye mshirika mkubwa wa kibiashara na kwamba inatarajia kuona uchumi ukiimarika zaidi siku za usoni.

Aidha, imesisitiza kuwa itaendelea kuwa na ushirikiano na nchi hiyo katika kuhakikisha wanatengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa pande zote kufanya shughuli zao bila vikwazo hatua ambayo itachochea Afrika kuwa huru kiuchumi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Kenya katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam Desemba 13, 2023.

Hayo yamebinishwa Desemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo katika hafla ya Maadhimisho miaka 60 ya Uhuru wa Kenya.

Prof. Mkumbo ambaye alimuwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema kuwa serikali ya Tanzania na Kenya ni marafiki wa asili ambao wamekuwa wakishirikiana katika nyanja tofauti tofauti ikiwamo biashara.

“Nimefurahi sana kuhudhuria siku ya Uhuru wa Kenya ambao unafikisha miaka 60. Imekuwa ni siku muhimu ya kukumbusha mambo muhimu mawili, kwanza mapambano ambayo ilifanya katika kujikomboa kutoka katika mikono ya Wakoloni, pili kukumbusha safari kubwa ambayo wamepiga katika maendeleo wakiwa na kauli mbiu ya “Tumetoka mbali, Tunakwenda mbali”.

“Naweza kusema kwamba uhusiano mzuri na mwema kati ya Tanzania na Kenya umekuwa wa asili na unakwenda zaidi ya serikali na serikali na nimesisitiza umuhimu wa kuendelea kuliweka Bara la Afrika kuwa huru kiuchumi kwa sasa biashara kati ya nchi zetu mbili tumefikia biashara zenye thamani ya Shilling trillioni 1.8.

“Hivyo, kwa Afrika Kenya ndiye mshirika wetu mkubwa wa kibiashara, matarajio yetu ni kuona kwamba mataifa yetu yanakua zaidi kiuchumi ili watu wetu waweze kufaidi matunda ya uhuru wa nchi zetu,” amesema Prof. Mkumbo.

Upande wake Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isack Njenga, amesema katika kipindi hiki cha miaka 60 ya uhuru, yapo mengi waliyofanikisha kama nchi na kikanda katika nyanja za uchumi na nyingine.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isack Njenga akizungumza na wageni waalikwa katika hafla ya kusherehekea Miaka 60 ya Uhuru wa Kenya iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam Desemba 13, 2023.

“Tumekuwa na uhuru wa kufanya mipango na mikakati ikiwemo kuwa na dira ya maendeleo katika kufikia malengo ikiwamo kushirikiana na nchi mbalimbali duniani ikiwemo majirani zetu Tanzania kwani tumekuwa na urafiki wa jadi ambao umetuwezesha kufikia malengo makubwa.

“Sisi waafrika ni watu wenye uwezo mkubwa na ubunifu wa hali ya juu, mfano ukiangalia huduma kama ya M-Pesa ilianza Kenya na kisha ndiyo ikasambaa kote duniani, hivyo tumepiga hatua kubwa kwa kushirikiana na majirani zetu Tanzania.

“Hivyo, kama waasisi wa ushirikiano huu wa Afrika Mashariki tunaamini kwa fikra za viongozi wetu waliopita tunaona tunapiga hatua kubwa na tutafikia mafakio ambayo kila mwanachama anayakusudia,” amesema Balozi Njenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles