Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara ni salama.
Hatua hiyo inafuatia baada ya kuwepo kwa taarifa kuhusu dawa aina ya paracetamol iliyoandikwa ‘P 500’ inayodaiwa kubabua ngozi.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo, imesema hakuna virusi vinavyojulikana kwa jina la Machupo na kwamba virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge.
“Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zimesajiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa hivyo ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa,” amesema.
Mamlaka hiyo imewahakikishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda afya ya jamii kwa kuhakikisha bidhaa tiba zinazotumika nchini zinakidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.
Kulingana na TMDA, taarifa kama hiyo iliwahi kutolewa Mei 10,2023 na kushauri wananchi kupata ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki.