Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Tanzania imeanza utekelezaji wa makubaliano ya kuuza mahindi tani 650,000 kwa Zambia, kufuatia mazungumzo kati ya Rais Samia Suluhu na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema yaliyofanyika Aprili 26, mwaka huu. Mazungumzo hayo yalifuatwa na mikutano kati ya wizara za kisekta na balozi za nchi hizi mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.), kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuwa msaada kwa washirika wake wakati wa uhitaji. Zambia imehitaji msaada huu wa chakula ili kusaidia zaidi ya wananchi milioni 7 wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame uliolikumba taifa hilo.
Makubaliano haya, ambayo yanatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane, yatasaidia kuimarisha uhusiano, udugu na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Aidha, Tanzania itaingiza Sh bilioni 650 kupitia makubaliano haya.
Ukame uliosababishwa na mvua za El Nino umeathiri zaidi ya hekari milioni 1 nchini Zambia, na hivyo kuiweka nchi hiyo katika uhitaji mkubwa wa chakula ili kunusuru maisha ya wananchi wake.
Tanzania na Zambia zimekuwa marafiki wa muda mrefu katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika. Ushirikiano wao ulianza wakati wa harakati za kupigania uhuru chini ya waasisi wa mataifa haya, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda. Udugu huu wa miaka na mikaka unathibitishwa na miradi mbalimbali kama Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) na Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).