28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia, Nyusi wakubaliana kuimarisha ushirikiano wa Kibiashara na Uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, wamekutana na kufanya mazungumzo mbalimbali, ikiwemo namna ya kushirikiana katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Akizungumza leo, Julai 2, 2024, Ikulu jijini Dar es Salaam, na waandishi wa habari mara baada ya kumkaribisha Rais Nyusi ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu, Rais Samia alisema kuwa Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuongeza uhusiano wa kibiashara hasa katika kuhamasisha ufanyikaji wa biashara baina ya nchi hizo mbili.

“Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuongeza uhusiano wa kibiashara. Mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili bado yapo chini hivyo tunapaswa kuongeza mahusiano hayo pamoja na uwekezaji,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alifafanua kuwa mwaka 2022, mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili yalikuwa Dola Milioni 57.8 lakini mwaka jana yalishuka hadi kufikia Dola Milioni 20.1. Hali hii imesababisha wasiwasi na hivyo wameamua kuchunguza sababu za kushuka kwa biashara.

“Imetushtua wote hivyo tumesema tutalichunguza vizuri eneo hili, tumekubaliana kuangalia ni sababu gani zilisababisha jambo hili,” alieleza Rais Samia.

Rais Samia pia alisema kuwa nchini Tanzania kuna wawekezaji wawili tu kutoka Msumbiji ambao wametengeneza ajira, wakati Watanzania 16 ndio waliowekeza Msumbiji. Alisema namba hii ni ndogo na inapaswa kuongezwa.

“Wapo wawekezaji wawili tu kutoka Msumbiji ambao wametengeneza ajira hapa nchini, na Watanzania 16 ndio waliowekeza kule Msumbiji. Namba hii tumeona kuwa ni ndogo hivyo inapaswa kuongezwa,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alisema wamekubaliana pia kuongeza ushirikiano wa kuziunganisha nchi hizo mbili na nyingine za Afrika katika masuala ya usafiri, usafirishaji, na nguvu ya umeme.

Kwa upande wake, Rais Nyusi alisema wamekutana na Rais Samia na kufanya mazungumzo mbalimbali, ikiwemo kupitia upya suala la ushirikiano wao na kwamba wanahitaji kufanya juhudi zaidi katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

“Mahusiano yetu yanahitaji juhudi zaidi katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu,” alisema Rais Nyusi. “Nchi hizi mbili zinahitaji kufanya kazi kwa pamoja na wakati mwingine kuwa na mkutano wa pamoja na kuzungumzia namna gani wanaweza kukuza uchumi wa nchi zao.”

Rais Nyusi alieleza kuwa mazungumzo yao pia yalihusisha ziara ya Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embaló, ambaye alitembelea Msumbiji na baadaye Tanzania, na kuzungumzia namna ya kukuza uzalishaji wa zao la korosho.

“Bidhaa hizi zikichukuliwa na wenzetu, sisi hatunufaiki ipasavyo. Hivyo ni vema kuwepo kwa utafiti unaoweza kutafuta namna bora ya zao hili kuleta manufaa kwa nchi zetu,” alisema Rais Nyusi. “Ni muhimu kuwa na umoja wa nchi zinazozalisha korosho ambapo zao hili linaweza kuwa na tija zaidi hapo baadaye.”

Mazungumzo haya yanaonyesha nia thabiti ya Tanzania na Msumbiji katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, huku wakilenga kuinua uchumi wa nchi zao kwa pamoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles