28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia: Urafiki wetu na Msumbiji umejengwa kwa Msingi wa Kihistoria

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania nDigital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameangazia historia ya urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Msumbiji, akieleza jinsi viongozi waasisi wa mataifa haya mawili walivyoweka msingi imara wa ushirikiano huo.

“Urafiki wetu uliwekwa vizuri zaidi na wababa wa mataifa yetu,” alisema Rais Samia na kuongeza kuwa: “Marehemu Eduardo Mondlane, ambaye ni kama baba wa Taifa la Msumbiji, na Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa letu, ndio walituunganisha vizuri sana wakati ule tunatafuta uhuru kutoka kwa wakoloni,” amesema.

Rais Samia akizungumza Ikulu leo Julai 2,2024 alifafanua kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Msumbiji yalianza rasmi mwaka 1977, pale ambapo nchi hizi mbili zilisaini mkataba wa kuunda Tume ya Pamoja kushughulikia uhusiano wao. Tume hii imekuwa ikishughulikia masuala mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, usafiri, usafirishaji wa watu na bidhaa, na uhamiaji.

“Mahusiano yetu ya kidiplomasia yalianza mwaka 1977 tuliposaini mkataba wa kuunda Tume ya Pamoja kushughulikia uhusiano wetu, ambayo imeshughulikia mambo kadhaa ya kibiashara, uwekezaji, usafiri, usafirishaji wa watu na bidhaa, na uhamiaji,” alieleza Rais Samia. “Kilimo pia kimeshughulikiwa katika Tume hii.”

Rais Samia alibainisha kuwa leo hii Tanzania na Msumbiji zimesaini makubaliano muhimu katika sekta za afya na uwekezaji, yaliyotokana na majadiliano ya Tume hiyo.

“Kama tulivyoona leo hapa, tumesaini makubaliano ya afya na uwekezaji ambayo yalizungumzwa kwenye Tume hii na baada ya makubaliano hayo, ndio leo tumesaini,” alisema Rais Samia.

Huu ni ushahidi wa jinsi uhusiano wa Tanzania na Msumbiji unavyosonga mbele, kwa msingi wa urafiki na ushirikiano uliowekwa na waasisi wa mataifa haya, huku ukijengwa zaidi kupitia juhudi za kisasa za kidiplomasia na ushirikiano wa kibiashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles