24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

STAA WA MBAO NI KOCHA

Na ABDUL MKEYENGE

MWISHONI mwa miaka 80 na mwanzoni mwa miaka 90 kulikuwa na timu ya Reli ya Morogoro iliyoitwa jina la utani Kiboko ya Vigogo kutokana na upinzani iliyokuwa ikiutoa kwa Simba na Yanga.

Timu hiyo ilikuwa ikitumia fedha kiduchu kwenye usajili wake tofauti na timu hizo kongwe zilizokuwa zikitumia gharama kubwa kununua wachezaji, lakini ndani ya uwanja Reli ilionekana moto wa kuotea mbali.

Wachezaji Boniface Njohole, David Mihambo, Duncan Butinini, Juma Salum, Madundo Mtambo, Abdallah Mkali (Hayati) James Charles (Hayati), Mbuyi Yondani, Gasper Lukindo ni miongoni mwa nyota waliokuwa wakiunda kikosi hicho kwa miaka tofauti wakiwa na makocha wao, Thabit Mgalula na John Simkoko.

Baada ya timu hiyo kushuka daraja kwa sababu nyingi tofauti, muda mrefu Ligi Kuu Tanzania Bara ilikosa timu ya namna hiyo inayoweza kutumia bajeti finyu kufanya mambo makubwa na kuwaacha watu midomo wazi.

Baada ya anguko la Reli ya Morogoro zikaja timu za aina ya Moro United ‘Chelsea ya Bongo’, Mbeya City, lakini zote hizo zikawa na sura ya tofauti kwa Moro United kuteremka daraja na Mbeya City kuwa na kiwango cha kusuasua tofauti na ilivyopanda daraja katika msimu wake wa kwanza.

Muda huu ambao Reli ya Morogoro imejifia na haijulikani lini itarudi Ligi Kuu Bara, Moro United wakipoteza dira na Mbeya City wakizidi kujishangaa, imeibuka timu ya Mbao FC inayofanya vyema.

Mbao FC ya jijini Mwanza ni moja ya timu inayofanya vyema katika msimu wake wa pili wa mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara, bila kutumia gharama kubwa ya usajili.

Timu hiyo inayotumia jina la Chama la Wana kama jina lake la utani, imekuwa ikizisumbua Simba na Yanga na kuonekana kikwazo kwa vigogo hao.

Msimu uliopita ambao ulikuwa msimu wao wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, walifika hatua ya fainali michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kufungwa na Simba.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Mbao FC walionyesha kiwango kizuri na kufanya wapoteze mchezo huo kwenye dakika 120 baada ya dakika 90 kumaliza kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Msimu huo ambao ulikuwa msimu wa kwanza kwa timu hiyo waliweza kuzibana vyema timu za Simba, Yanga katika michezo yao ya nyumbani na ugenini.

Katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini iliyokutana na Simba, Mbao walipoteza michezo yote, lakini walionyesha umahiri wa kucheza soka safi.

Mazingira ya mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Mbao FC walipoteza kwa kufungwa bao 1-0, bao lililofungwa dakika ya 87 na kiungo mshambuliaji wa Simba, Mzamiru Yassin.

Mchezo wa marudiano uliofanyika Mwanza kwenye dimba la CCM Kirumba, Simba walishinda mabao 3-2, lakini mpaka mchezo huo unakwenda mapumziko Mbao walikuwa mbele kwa mabao 2-0 na Simba iliporudi kipindi cha pili ikaweza kushinda mabao 3, mabao mawili yakifungwa na Yassin na lingine Fredrick Blagnon.

Baada ya mchezo huo kumalizika viongozi wa Mbao FC, walimuweka kitimoto mlinda mlango wao, Erick Ngwengwe, baada ya kuona amefungwa mabao ya kizembe.

Katika michezo ya Mbao FC dhidi ya Yanga msimu huo, timu hizo ziligawana pointi tatu kwa kila timu kushinda kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Yanga iliwafunga Mbao FC mabao 3-0 katika pambano lililofanyika Uwanja wa Uhuru, huku Mbao FC wakiwafunga Yanga bao 1-0. Yanga iliutumia mchezo huo uliokuwa wa mwisho kupewa kombe lao, huku wakiwa na maumivu ya kupoteza mchezo huo.

Msimu huo ulipomalizika timu za Simba na Yanga na timu nyingine zilipiga hodi ndani ya kikosi hicho na kusajili baadhi ya mastaa wake.

Katika kikosi cha kwanza cha Mbao FC msimu uliopita waliondoka wachezaji saba waliokuwa wakitegemewa.

Nyota hao ni Kwessi Asante (Lipuli FC), Jamal Mwambeleko, Emmanuel Mseja (Simba), Pius Buswita (Yanga), Salimin Hoza na Benedict Haule (Azam), Evarist Vedartus (Mwadui FC).

Kuondoka kwa nyota hao kulimwaminisha kila mpenda soka kuwa anguko la kikosi hicho limewadia, lakini kumbe mambo ni tofauti na alivyokuwa akifikiri kocha wa kikosi hicho, Ettiene Ndayiragije.

Ndayiragije ndiye staa wa Mbao FC. Ni yeye mwenye ujasiri wa kuwaamini vijana wengi wasiokuwa na majina na kuwafungulia dunia kuwa wanachokitaka.

Kocha huyo raia wa Burundi ni miongoni mwa makocha wenye wasifu wa juu kwenye soka la Afrika Mashariki.

Ndayiragije, aliwahi kuchukua kozi ya ukocha nchini Ufaransa kwenye klabu ya Nantes na amewahi kufundisha timu kadhaa nchini kwao.

Umahiri wa kocha huyo hauko kwenye kutoa mbinu bali uko hadi kumtazama mchezaji na kumwona anafaa kucheza nafasi gani.

Kocha huyo amembadilisha nafasi mchezaji Boniface Maganga ambaye awali alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji, lakini Ndayiragije amembadilisha na kuwa mlinzi king’ang’anizi wa kulia na kumvutia hadi kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ amjumuishe  katika kikosi chake kila mara hivi sasa.

Ndani ya msimu huu, Ndayiragije ameonyesha moto baada ya kuondokewa na baadhi ya mastaa wake, lakini amesajili vijana wengine na kukipa heshima kikosi chake.

James Msuva mdogo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simon Msuva, Faraji Kabali, Kelvin Ingendelezi, Abubakar Ngalema, Yusuph, Sadallah Lipangile, Emmanuel Mvuyekire, Habibu Kiyombo wamekifanya kikosi hicho bado kiwe moto.

Nyota hao pamoja na wakongwe wa timu nahodha Yusuph Ndikumana, Maganga na wengineo wameifanya timu hiyo ivune pointi 4 katika michezo minne waliyocheza mpaka sasa msimu huu.

Katika michezo hiyo Mbao FC wamepoteza michezo miwili, wameshinda mchezo mmoja na wamepata sare mchezo mmoja.

Sare hiyo ilikuwa ni kwenye mchezo wa katikati ya wiki dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba. Ilikuwa sare ya kufungana mabao 2-2.

Katika pambano hilo kocha wa Mbao FC alionyesha umahiri wa kufahamu mianya yote ambayo Simba wangepita na kwenda kuidhuru timu yake.

Mfumo alioingia nao katika mchezo huo ulikuwa wa kujilinda na ulikuwa na faida kwa maana kipindi cha pili alirudi uwanjani kwa lengo la kutafuta goli kwa mashambulizi ya kushtukiza (counter attacks) na alifanikiwa kwa mbinu hiyo.

Katika kila wanachokifanya Mbao FC kuanzia msimu uliopita mpaka msimu huu, jina la kocha wao ndiyo linasimama kama staa wa timu tofauti na timu nyingine ambazo wachezaji ndio wanakuwa mastaa wa timu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles