27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ushindi Miss Tanzania yavuja

DIANA akiwa na mshindi wa pili Merry Peter 26 kutoka Mwenza na mshindi wa tatu Grece Malikita 7 kutoka Ilala.
DIANA akiwa na mshindi wa pili Merry Peter 26 kutoka Mwenza na mshindi wa tatu Grece Malikita 7 kutoka Ilala.

Na JOSEPH SHALUWA, MWANZA

MLIMBWENDE mpya wa Tanzania mwaka huu 2016 amepatikana usiku wa kuamkia jana katika Fainali ya Miss Tanzania iliyofanyika kwa mara ya kwanza jijini hapa, huku siri ya ushindi wake ikivuja.

Kwa sasa siyo siri tena kuwa Diana Edward kutoka Kanda ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam ndiye Miss Tanzania mwaka 2016, baada ya kuwaangusha wenzake 29 waliopanda jukwaani katika Viwanja vya Rocky City Mall, jijini hapa.

Miongoni mwa siri kuu iliyomfanya Diana aibuke na ushindi huo ni uwezo wake wa kujieleza kwa kujiamini akiwa na hoja katika maelezo aliyotoa wakati akijibu swali alilochagua.

Siri nyingine ni kuchagua kusaidia jamii ya kabila la Wamasai ili waepukane na mila ya kukeketa watoto wa kike, akitumia msemo wa ‘Masai dondosha wembe’.

“Nia yake ya kutetea wasichana wa jamii ya Kimasai bila shaka ndiyo iliyowavuta majaji na kuamua kumtazawa kuwa mshindi. Lakini namna anavyojieleza kwa kujiachia na kujiamini, ni kati ya sifa kuu zinazoangaliwa na majaji,” alieza Julie Magesa, mmoja wa wahudhuriaji wa shindano hilo.

Magesa anaongeza: “Amekuja na kitu cha tofauti… angalia hata namna alivyozungumza, amechagua lugha ya Kiingereza, lakini amejibu vizuri, hana papara na ana pointi zinaoeleweka. Ni haki yake kuibuka mshindi.”

Mbali na ushindi wa Diana, warembo waliomfuata walikuwa ni Merry Peter kutoka Kanda ya Mwanza aliyechukua nafasi ya pili akifuatiwa na Grace Malikita wa Kanda ya Ilala aliyetwaa namba tatu.

MISS TANZANIA 2016

Shindano la Miss Tanzania 2016, lililofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu tangu kufufuliwa kwake, miaka 22 iliyopita na kufanyika Dar es Salaam pekee, limekuwa na msisimko wa aina yake na kuhudhuriwa na watu wanaokadiriwa kufikia 3000 waliojaza uwanja mzima.

Pazia rasmi la ufunguzi wa shughuli hiyo, lilifunguliwa mishale ya saa 5:30 usiku ambapo warembo walifungua fainali hizo kwa kupiga shoo matata kwa kupishana, wakiwa warembo 10 kila kundi.

WASANII WA KANDA YA ZIWA

Baada ya ufunguzi wa shoo hiyo, wasanii wa jijini hapa walipata kupitisha fagio la burudani kwa ajili ya kumsafishia njia, mkali wa Bongo Dansi, Christian Bella aliyepanda mwishoni.

Msanii wa kwanza kutoka hapa Mwanza aliyepata nafasi ya kuonyesha makali yake ni mwanamuziki wa Dancehall   akifuatiwa na msanii wa RnB, Cool Chata aliyeibua shangwe kubwa.

MAMISI WACHUJWA

Baada ya shoo iliyochukua takribani dakika 30, warembo walipanda jukwaani na mavazi ya ufukweni, kisha baadaye wakapita na ya ubunifu kabla ya kuhitimisha katika mavazi ya jioni.

Onyesho hilo lilivyokamilika, mmoja wa washereheshaji wa onyesho hilo, Jokate Mwegelo aliye Miss Tanzania 02 mwaka 2006, alimuita mmoja wa majaji kwa ajili ya kuwataja warembo walioingia 15 Bora.

Baada ya mchujo wa kwanza, ilifuata mchujo wa pili ambao uliwabakiza warembo watano jukwaani.

MREMBO NUSURA AZIMIE

Mrembo aliyekuwa na namba 07 aitwaye Grace Malikita aliyeingia 5 Bora, kutokea Kanda ya Ilala, Dar es Salaam, alikatisha kujieleza na kuonekana akibabaika kwa muda jukwaani kabla ya kumfuata Jokate na kumnong’oneza kitu.

Kwa namna alivyoonekana ni kama alihisi kizunguzungu na kutaka kuzimia, hivyo ilibidi asaidiwe na mmoja wa wahusika kutoka nje ya jukwaa.

Awali wakati akijibu swali namba tatu, lililomtaka aeleze ni wakati gani au jambo gani linalompa furaha, alijieleza vizuri kwa Lugha ya Kiingereza fasaha, lakini ghafla alisita na kushindwa.

Pamoja na Jokate kumshawishi ajitahidi kumalizia kujibu swali lake, bado mlimbwende huyo alisisitiza ashuke jukwaani.

NYUMA YA JUKWAA

Wanakamati wa Miss Tanzania wakiongozwa na Hashim Lundenga walimshusha Grace jukwaani na kumpeka kwenye chumba cha mapumziko ambapo alipewa muda wa kupumzika na kupatiwa ushauri wa kumtuliza.

Robo saa baadaye, hali ya mrembo huyo iliimarika na kuungana na wenzake kwa ajili ya kusubiri mzunguko wa mwisho uliomtoa mshindi na wawili waliomfuata kwa nyuma.

HISTORIA YAANDIKWA

Kwa miaka 22 mfululizo (tangu mwaka 1994) shindano hili lilifanyika jijini Dar es Salaam, lakini kwa mara ya kwanza limefanyika jijini hapa kwa mafanikio makubwa.

Umati mkubwa wa watu ni kielelezo tosha kuwa, wana-Mwanza walicheleweshewa heshima hii kwa muda mrefu.

Akizungumza jukwaani kabla ya washindi wa juu kutangazwa, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, alisema mwitikio mkubwa unatoa taswira kuwa Watanzania wanaunga mkono mashindano hayo.

“Tumefurahi kuona Miss Tanzania hii mpya nzuri. Maadili kwakweli yamezingatiwa na wote tumeona. Sisi kama Serikali tunaungana nanyi na tunatambua mafanikio yanayotokana na watoto wa kike wanaoshinda katika mashindano haya.

“Tumeridhika na tumefurahishwa sana na mchakato wa shughuli nzima, lakini pia mahudhurio mazuri yenye kudhihirisha kuwa mashindano haya yanapendwa, kukubalika na kuheshimiwa na Watanzania.

“Tunakumbuka vizuri mchango wa Hoyce Temu, namuona yupo hapa ukumbini. Yeye anaendesha kipindi Channel Ten ambacho kinasaidia sana jamii… hata Wema Sepetu naye anafanya vizuri kwenye kazi zake.

“Lakini pia tunaheshimu sana jitihada za Miss Tanzania 2005, Nancy Sumari ambaye alishinda taji la Miss World Afrika mwaka ule. Humu ukumbini yumo pia Genevieve Mpangala ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2010, huyu amesaidia sana watoto wanaoishi na Ualbino lakini pia Lilian Kamanzima ambaye anamaliza muda wake leo, yeye amesaidia wanawake wenye matatizo ya Fistula.

“Yote hayo ni mafanikio makubwa ya Miss Tanzania ambayo sisi kama Serikali tunakubaliana nanyi na kwakweli tunawashukuru sana kutuwakilisha vizuri huku mkoani. Ni lengo letu pia kama wizara, kuhamisha wizara yetu katika moja ya mikoa yetu. Hivyo huu ni mwanzo mzuri.

“Mwisho, nawaomba sana waandaaji muwe makini sana na mikataba. Naomba sana, mikataba mliyoingia na hawa warembo wetu, iheshimiwe,” alisema naibu waziri huyo.

BELLA SHANGWE

Shoo ya Christian Bella iliyokuwa na uzani wa juu ndiyo iliyofunga burudani ukumbini hapo, muda mfupi kabla ya washindi kutangazwa.

Bella alipagawisha na vibao vyake Nashindwa, Ameondoka, Amerudi, Nani Kama Mama na vingine vilivyompa heshima na kuinua ukumbi mzima muda wote aliokuwa jukwaani.

Akiwa jukwaani, Bella alituzwa noti za kutosha kutoka kwa mashabiki mbalimbali wakiwemo Wema Sepetu, Sebastian Maganga na mapedeshee wengine wa jijini hapa.

Pazia la shughuli lilifungwa rasmi saa 9:30 usiku, ikiwa ni shoo iliyochukua saa nne isiyochosha na jambo la kufurahisha ni kwamba hakuna hata mmoja aliyesinzia!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles