31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

 SHAHIDI AELEZA NYARAKA BANC ABC ZILIVYOGHUSHIWA

Na FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM

SHAHIDI katika kesi ya kughushi nyaraka na kuiba inayowakabili waliokuwa wafanyakazi wa Banc ABC, Paulo Mwakiteleko na Edward Kubagwa, ameieleza mahakama namna watuhumiwa hao walivyoghushi jina na kujipatia Sh milioni 23.6, mali ya Juliana Masanja, kinyume cha sheria.

Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Juma Hassan kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Grace Mwanga, shahidi huyo, Abdalla Kilungi (42) ambaye alikuwa ni Meneja Mwandamizi wa benki hiyo, alisema alibaini wizi huo baada ya kupata taarifa kutoka kwa mteja wao.

Kilungi, ambaye ni shahidi wa tatu kwenye shauri hilo, alisema kati ya Oktoba na Desemba, 2014, alipata taarifa kutoka kwa mteja akilalamika juu ya kuwapo kwa miamala ambayo imefanywa kwenye akaunti yake pasipo yeye kuwa na taarifa.

“Mteja huyo aliniambia miamala hiyo iliyofanyika kwenye akaunti yake hiyo haikuwa yake, baada ya hapo nikakabidhi jukumu hilo kwa ofisa usalama wa benki kwa ajili ya kufanya uchunguzi, wakati huo ikiwa ni kati ya Oktoba na Desemba.

“Baada ya uchunguzi wa ofisa usalama wa benki, ilionyesha kuna miamala ambayo ilikuwa imefanyika kwenye akaunti hiyo bila utaratibu wa benki kufuatwa, ikiwamo kutokuwapo kwa mteja mwenyewe,” alisema.

Shahidi huyo aliendelea kuiambia Mahakama hiyo kuwa, kwa taratibu za benki yao, ilikuwa haimruhusu mfanyakazi wa benki (Tela) kulipa zaidi ya Sh 750,000 kwa mteja na zaidi ya kiwango hicho, lazima kiidhinishwe na msimamizi wa benki (Supervisor), jambo ambalo alisema kuwa halikufuatwa.

“Uchunguzi wetu huo ulionyesha kuwa, aliyekuwa amehusika na mpango huo alikuwa ni mtuhumiwa namba mbili, ambaye ni Edward, kwani kama benki tuliweza kuthibitisha kuwa hakuna mteja aliyekuja kuchukua kiasi hicho cha fedha, badala yake ni mmoja wa wafanyakazi wa benki ndiye aliyehusika kutoa fedha.

“Hivyo miamala yote tulibaini kuwa haikufuata utaratibu na hivyo kuulazima mfumo wa benki kutoa fedha pasipo kumtambua mteja wala kuhitaji uthibitisho,” alisema.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa katika shtaka la kwanza, watuhumiwa wote kwa pamoja kati ya Oktoba na Desemba, 2014, ndani ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam walighushi jina na kuiba.

Katika shtaka la pili, watuhumiwa kati ya Oktoba na Desemba, 2014, wakiwa ndani ya Banc ABC, walighushi sahihi ya Juliana Masanja na kutoa kiasi cha pesa huku ikionyesha kuwa mlalamikaji ndiye aliyetoa kiasi hicho cha pesa.

Na katika shtaka la tatu, watuhumiwa kati ya Oktoba na Desemba, 2014, wakiwa Banc ABC maeneo ya Uhuru Kariakoo, waliiba kiasi cha Sh milioni 23.6 kutoka kwenye akanti ya Juliana Masanja.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Oktoba 23, mwaka huu, kwa ajili ya ushahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles