Na BENJAMIN MASESE-MAGU
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amekabidhiwa miradi nane iliyokamilika yenye thamani Sh milioni 114.2 iliyotekelezwa naKampuni ya Mbogo Mining & General Supply Ltd, huku akiwagiza wakuu wa wilaya kumlinda na kumpa msaada pale inapohitajika.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa vyoo vya kisasa na vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Bukandwe wilayani Magu jana, ikiwa ni sehemu ya miradi yote, Mongela alisema hajawahi kupokea fedha ama miradi ya wawekezaji kama sehemu ya faida yake kwa wananchi inayofikia Sh milioni 100 ispokuwa Mbogo Mining.
Alisema mara zote kiwango cha fedha zitokanazo na faida ya uwekezaji, huishia Sh milioni 15 au zaidi kidogo, lakini kampuni hiyo meonyesha uzalendo na mfano kwa wengine.
Baadhi ya miradi iliyokabidhiwa, ni vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Msingi Ilendeja na Bukandwe vilivyogharimu Sh milioni 90, matundu 12 ya choo cha kisasa na mfano katika Mkoa wa Mwanza kilicho na kabati yenye vifaa vya taulo za kike kilichogharimu Sh milioni 10.7, ukarabati wa choo cha walimu Shule ya Ilendeja Sh milioni nne.
Mingine ni ujenzi wa uzio na ununuzi wa samani katika kituo cha polisi Kisesa, ununuzi wa sare na vifaa vya michezo shule za msingi mbalimbali ndani ya Wilaya ya Magu, ukarabati wa madarasa shule Ilendeja na Bukandwe, madawati na misaada kwa wananchi pale inapotokea matatizo ya kijamii.
“Sote tumejionea vyoo vya kisasa vyenye makabati ya taulo za kike, hakuna shule ambayo ina vyoo na vifaa vile ispokuwai Bukandwe pekee hivyo naomba miundombinu hii itunzwe na wawekezaji wengine waige kilichofanywa na Mbogo Mining & General Supply Ltd,”alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mbogo Mining & General Supply Ltd, Barnabas Nibengo alisema aliamua kujenga maghala yake ya vilipuzi kwa sababu ya usalama na jiografia ya mikoa anayosambaza vifaa vya shughuli hiyo.
Alisema licha ya shughuli zake kufanyika nje ya mkoa, anajitolea kuisaidia jamii kwa sababu ya ushirikiano mzuri uliopo tangu ujenzi huo ulipofanyika mwaka 2014 ambapo wananchi walimpa ardhi bila masharti magumu na haijawahi kutokea mgogoro baina yake.
“Pamoja na ushirikiano uliopo ngazi ya kitongoji hadi taifa, tunaishauri Serikali kuwapa kipaumbele zaidi wawekezaji katika kutoa kandarasi za miradi mbalimbali kwani kwa kufanya hivyo kunaimarisha uzalendo na kutupatia nguvu na ari ya kufanya kazi,”alisema.
MWISHO