23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Mavunde aitoza Sh mil 1.4 Grumeti Reserve

Mavunde aitoza Sh mil 1.4 Grumeti Reserve

Mwandishi Wetu-Musoma

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde ameitoza faini ya Sh  milioni 1.4 Kampuni ya Grumeti Reserve, baada ya wafanyakazi 28 wa kampuni hiyo kubainika kufanya kazi bila kuwa na vifaa vya usalama kazini.

Waziri Mavunde alitoa adhabu hiyo jana, baada ya kufanya ziara katika kampuni hiyo inayofanya shughuli za utalii katika mapori ya akiba ya Ikorongo wilayani Serengeti.

Pamoja na mambo mengine wafanyakazi wa kampuni hiyo walilalamika kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Mbali na adhabu hiyo, Mavunde pia alitoa siku 14 kuanzia jana kwa kampuni hiyo kuhakikusha vifaa hivyo vinafika na kugawiwa kwa wafanyakazi, huku akiagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi(OSHA)  kufika  eneo hilo ili kufanya ukaguzi juu ya mazingira ya ufanyaji kazi.

Mapema wafanyakazi hao waliwasilisha malalamiko yao kwa njia ya maandishi, wakiogopa kuwajibishwa ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, walisema wafanyakazi wa vitengo vya ufundi na ujenzi kwa muda mrefu wamekuwa wakifanyakazi bila kuwa na mavazi ya usalama kazini jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Walidai  pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwa uongozi wa kampuni hiyo,hakuna hatua zilizochukuliwa huku baadhi yao wakidai hali hiyo imekuwapo kwa zaidi ya miaka minne  na kulazimu wengine kujinunulia mavazi hayo kwa gharama zao jambo ambalo ni kinyume na mikataba yao ya kazi.

Kutokana na malalamimo hayo,Mavunde alilazimika kutembelea idara za ufundi na ujenzi ambazo wafanyakazi wake walidai kufanya kazi bila kuwa na mavazi hayo na kubaini kuwepo kwa hali hiyo.

Alisema suala la usalama na afya mahali pa kazi,lazima lipewe kipaombele kwa maelezo kuwa taifa linaweza kupoteza nguvu kazi kutokana na magonjwa na ajali  ambazo hutokana na mazingira ya kazi hivyo serikali haiwezi kukaa kimya.

Alisema ni wajibu wa muajiri kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama muda wote, ikiwamo wafanyakazi kuapatiwa vifaa vya usalama wawapo kazini.

Katika hatua nyingine, Mavunde alisema Serikali inaanza uchunguzi juu ya vibali vya wafanyakazi wa kigeni wa kampuni hiyo kutokana na madai ya kuwapo wafanyakazi ambao wanafanya kazi ambazo zinapaswa kufanywa na wazawa.

Ofisa Rasilimali Watu wa Kampuni hiyo, Martha Baare alisema tatizo la ukosefu wa mavazi ya usalama kazini tayari limekwishapata ufumbuzi, kwani kampuni hiyo imeagiza mavazi hayo kutoka nchini Afrika Kusini.

Alisema  mavazi hayo yatafika muda wowote kuanzia sasa,baada ya kuagizwa Agosti, mwaka huu.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles