Ofisa JWTZ,polisi mbaroni kwa tuhuma za rushwa

0
676

Na Nyemo Malecela Kagera

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera, inawashikiria askari kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), polisi, ofisa afya wa Kijiji na mwajiriwa Idara ya Misitu kwa kujihusisha na matukio ya kuomba na kupokea rushwa katika matukio matatu tofauti katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera, John Joseph aliwataja watumishi hao, kuwa ni Koplo Nyambita Magoma (JWTZ), Koplo Nassoro Maulidy Mirambo (polisi), Asaph Manya Manya (misitu) na Audastus Rwegoshora Norbert (ofisa afya).

Alisema Nyambita ambaye alikuwa mmoja kati ya wakufunzi wa ofisi ya mshauri wa mgambo wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, akiwa  Kijiji cha Nemba aliomba rushwa ya Sh 3,000,000 ili asimchukulie hatua za kisheria mfugaji wa ng’ombe kwa  kosa la kuingiza mifugo yake  ndani ya hifadhi ya taifa.

“Nyambita alikamata ng’ombe wa mkazi mmoja wa wilaya hiyo kwa madai wameingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Biharamulo Forest Reserve,kisha kuomba kupatiwa kiasi hicho cha fedha ili asimchukulie hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kumfikisha katika mamlaka husika.

Askari huyo alishikilia mifugo hiyo mpaka alipopatiwa Sh 400,000, kisha kumwachia mwananchi huyo ambaye alilazimika kutoa taarifa Takukuru Oktoba 12, mwaka huu,” alisema.

Kwa upande wa Mirambo ambaye ni askari polisi wa kituo cha Runazi, humo anatuhumiwa kushirikiana na Manya (misitu) kuomba na kupokea rushwa ya Sh  700,000 Agosti 23, mwaka huu kutoka kwa mfanyabiashara wa mkaa (jina limehifadhiwa),baada ya kumkamata akiwa na magunia 50.

“Uchunguzi wa Takukuru ulibaini fedha hizo zilipokelewa na Mirambo siku hiyo hiyo kwa mikupuo miwili ambapo awamu ya kwanza alipokea Sh 250,000, Sh  148,000.

“Ilibainika baada ya kupokea fedha hizo walimrudishia mlalamiiaji mkaa waliokuwa wanashikiliwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema.

Alisema kwa upande wa Rwegoshora ambaye ni Ofisa Afya wa Kijiji cha Nyakanazi, anashikiliwa kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh 200,000,kisha kupokea Sh 50,000 kutoka kwa mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa ili asimfungie bucha yake ya kuuza nyama.

“Mwananchi huyo ambaye anauza nyama buchani aliombwa rushwa na Rwegoshora baada ya kumkuta na makosa akiwa katika shughuli za ukaguzi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Uchunguzi wa tuhuma hizi unakaribia kukamilika na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili mara tu baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Joseph alitoa rai kwa watumishi wa umma na Watanzania kujiepushe na vitendo vya rushwa.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here