31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaunda tume kuchunguza maghorofa Kariakoo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imeunda tume ya watu 19 kufanya uchunguzi wa maghorofa yote yaliyoko katika Soko la Kariakoo.

Kuundwa kwa tume hiyo kunafuatia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa tatu katika Soko la Kariakoo Novemba 16,2024.

Juzi wakati akihutubia wananchi Rais Samia alimwekeleza Waziri Mkuu kuongoza timu ya uchunguzi wa majengo hayo.

Akizungumza leo Novemba 18,2024 wakati wa ibada ya kuaga miili ya marehemu katika uwanja wa Mnazi Mmoja, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema hadi sasa vifo vimefikia 16 na majeruhi ni 86 na kati yao watano bado wanaendelea na matibabu.

Amesema tume hiyo itafanya kazi ya kuyapitia maghorofa yote ya eneo la Kariakoo ili kujua ubora wake na kuishauri Serikali hatua za kuchukua.

“Tume hii itasaidia kujua na kuishauri Serikali nini ifanye baada ya uchunguzi kwa sababu mahitaji ya Soko la Kariakoo bado yako palepale. Soko la Kariakoo ni la kimataifa linategemewa na nchi zote zinazotuzunguka.

“Kwahiyo tunayo sababu ya kuliimarisha na kutambua ubora wa majengo tuliyonayo ili wajasiriamali waendelee kufanya biashara kwa miongozo mipya itakayotolewa na Serikali,” amesema.

Tume hiyo itaongozwa na Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Jenerali, Hosea Ndagala wakati katibu atakuwa Mhandisi Meleki Mwano kutoka Bodi ya Usajili wa Makandarasi.

Waziri Mkuu pia ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta mwenye jengo popote pale alipo ili aendelee kulisaidia kujua kwanini jengo limeanguka.

Aidha ameonya watu wanaotumia fursa ya ajali hiyo kuwachangisha Watanzania na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta walioanza kuchangisha fedha bila kuwa na kibali.

“Shughuli yoyote ya maafa ina utaratibu na huwa inatolewa maelekezo, iko namba maalumu ya Benki Kuu ambayo inapokea michango yote,” amesema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles