24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia itakayosaidia wanawake barani Afrika (AWCCSP) Jumamosi, Desemba 2, 2023 Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Marais wa nchi mbalimbali na viongozi wa ngazi za juu za serikali na mashirika ya kimataifa wamealikwa kuhudhuria uzinduzi wa programu hiyo yenye lengo la kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 900 kwenye nchi hizo hutumia kuni na mkaa kupikia jambo ambalo huathiri zaidi wanawake na watoto kwani ndio watafutaji na watumiaji wakubwa wa nishati hiyo.

Athari za matumizi ya nishati za kupikia zisizo safi ni pamoja na za kiafya, ambapo inaelezwa kuwa watu zaidi ya laki tano kwenye ukanda huo hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa yatokanayo na matumizi ya nishati hizo.

Kwa upande wa athari za kimazingira, takwimu zinaonesha upotevu wa hekta milioni 3.9 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli za ukataji misitu na hivyo kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi

Athari nyingine ni za kijamii ambapo wanawake na watoto hususani maeneo ya vijijini hukumbwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kutokana na kutembea umbali mrefu kutafuta kuni. Aidha, kundi hili hukosa muda wa kutosha kujihusisha na shughuli za maendeleo kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta kuni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, mabalozi na maafisa mbalimbali wa Serikali, Katibu Mkuu wa Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema maandalizi ya uzinduzi yanaendelea na tayari baadhi ya marais na viongozi mbalimbali wamethibitisha ushiriki wao.

Uzinduzi wa program hiyo utafanyika wakati wa Mkutano wa 28 wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP28) utakaofanyika kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 ambapo Marais zaidi ya 140 kutoka mataifa mbalimbali duniani na washiriki takriban 70,000 wanatarajiwa kuhudhuria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles