31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI AWALILIA WATU 15 WALIOKUFA KWA AJALI NKASI

Rais Dk. John Magufuli

Na GURIAN ADOLF -NKASI

RAIS John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 15 waliofariki dunia, huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kugonga mwamba na kisha kupinduka.

Ajali hiyo ilitokea juzi katika Tarafa ya Wampembe wilayani Nkasi, wakati gari aina ya Fuso lililokuwa likitokea katika Kijiji cha Wampembe kuelekea mjini Sumbawanga kupinduka.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, ajali hiyo ilitokea majira ya saa tisa alasiri katika eneo la Mbuga Nyeupe baada ya gari hilo kugonga mwamba na kupinduka.

Alisema baada ya gari hilo kupinduka, watu 12 walikufa papo hapo na wengine watatu walifariki baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa kupatiwa matibabu.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, alisema dereva wa gari hilo alikuwa ni mgeni na hajawahi kupita katika njia hiyo na baada ya kufika katika eneo hilo ambalo lina kona kali, alishindwa kumudu gari na kugonga mwamba na hatimaye gari kupinduka kisha dereva kukimbia kusikojulikana.

“Baada ya tukio hilo waliwakimbiza majeruhi katika hospitali ya mkoa huku maiti zote zikihifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Mvimwa kwa ajili ya utambuzi wa ndugu zao.

“Jana asubuhi tumeketi kikao cha kamati ya ulinzi na usalama na kuteua gari moja la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo litatumika kusafirisha maiti zote zitakazotambuliwa na ndugu zao hadi katika maeneo yao kwa ajili ya mazishi,” alisema Mtanda.

Aliwataka wananchi kujitokeza katika Kituo cha Afya cha Mvimwa kwenda kuzitambua maiti na kwamba gharama zote za usafirishaji wa maiti hizo zitabebwa na Serikali.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, George Kyando, alitoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani ili kuepuka ajali zinazokatisha maisha ya wananchi.

JPM AWALILIA

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli alipokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo hivyo.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna mstaafu Zelothe Stephen, familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na vifo hivyo.

 “Natambua hiki ni kipindi kigumu kwa wanafamilia wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii, natambua kuwa wamepoteza wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea, nawapa pole sana kwa kufiwa na naungana nao katika maombi ili roho za marehemu zipumzishwe mahali pema peponi. Amina,” alisema Rais Magufuli.

Mkuu huyo wa nchi, pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hiyo wapone haraka na kurejea katika afya njema.

Pia alizitaka mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama barabarani kuongeza juhudi zitakazowezesha kukabiliana zaidi na matukio ya ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles