23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yashiriki kukamilisha ndoto za wanafunzi Kanda ya Kaskazini

Na Mwandishi Wetu

Wanafunzi katika shule za Sekondari imani yao kubwa katika kufaulu na kuhudhuria madarasa kwa furaha ni namna ambavyo mwalimu anatoa ujuzi wake kwa kujiamini, mpangilio wa darasa lakini zaidi ni mazingira na vifaa vya kufundishia.

Kwa kuliona hilo, Benki ya NMB kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii wametenga kiasi cha asilimia moja ya faida ili kusaidia mambo mbalimbali ikiwemo elimu, afya na majanga mengine ya asili mara yatokeapo.

Meneja wa benki ya NMB tawi la Same, mkoa wa Kilimanjaro,Juma Mpimbi akikagua meza na viti vilivyotolewa na benki hiyo katika Shule ya Sekondari Kwakoko wakati wa ziara ya kukagua matumizi ya vifaa hivyo hivi karibuni.
 

Miongoni mwa shule walizosaidia ni Shule ya Sekondari Kibacha na Shule ya Sekondari Kwakoko zilizopo mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same, ambapo wanafunzi wanasema fadhila pekee wanayoweza kuwalipa NMB pamoja na wazazi wao ni kusoma kwa bidii.

NMB imesaidia viti 50 na meza zake katika Shule ya Sekondari Kwakoko ambapo pia wamesaidia viti 50 na meza zake katika Shule ya Sekondari Kibacha pamoja na vifaa vya maabara za sayansi za kujifunzia wanafunzi.

Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakato tofauti wanafunzi wa shule hizo, walisema wanajiona wana bahati kuwa sehemu ya utaratibu huo wa NMB kwa kuwa awali walisoma katika mazingira magumu lakini hawakuwa na namna ya kufanya.

Nasra Selemani mwanafunzi wa Kidato cha Nne A Shule ya Sekondari Kibacha, anasema: “Tulikuwa wanyonge sana wakati tukikaa chini, hasa sisi wasichana kwa kuwa tulichafuka. Hatukuwa na utulivu wakati wa masomo kwa sababu wakati mwingine tulikaa wawili kiti kimoja. Lakini tangu tupokee msaada huu wa viti na meza kutoka NMB hata ufaulu umeongezeka na wanafunzi hawategei masomo.”

Wanafunzi wa kidato cha Nne Shule ya Sekondari Kwakoko wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro wakiwa wamekalia meza na viti zilizotolewa msaada na benki ya NMB ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kurejesha faida kwa jamii. Picha hizo zilipigwa katika ziara ya maafisa kutoka benki ya NMB walipotembelea miradi ambayo wamesaidia na kujionea maendeleo ya vifaa walivyotoa.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibacha, Omary Magongo alisema vifaa vya maabara za sayansi vimekuwa na tija kubwa kwao awali, lakini baadaye walipata changamoto ambayo wakisaidiwa maabara zitarejea katika kutoa mafunzo.

“Naweza kusema tumefaidika kwa kiasi kikubwa na NMB, siwezi kuelezea furaha yangu kwa maneno matupu. Hapa tuna wanafunzi kati ya 700 hadi 800, utaona ni idadi kubwa. Changamoto ya madawati ilitutoa jasho lakini nyinyi mmetusitiri.

“Tatizo kubwa lilikuwa ni hilo la viti, watoto walikaa wawili wawili sasa iliwawia vigumu watoto wa kike, wakiwa katika hedhi wanajisikia unyonge na hata wengine wanafikia kupumzika nyumbani kwakipindi chote cha hedhi,” alisema Mwalimu Magongo.

Akielezea namna msaada huo unavyopatikana Afisa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka NMB, Aloyce Kikois, alisema wengi wanadhani msaada huo unapatikana kwa kuandika barua ndefu au inayohitaji utaalamu mkubwa, lakini yeyote anaweza kuandika.

“Si lazima Mbunge au Mkuu wa Wilaya aandike barua ya maombi, hata mwanafunzi akiona shuleni kwake kuna tatizo la madawati, viti au vifaa vya kuezeka; aandike barua aipeleke kwa Meneja wa Tawi letu lililopo karibu naye, aainishe mahitaji na ina la shule asilikosee pamoja na wilaya na mkoa ilipo shule.

“Huwa tunapokea maombi mengi na yote tunayafanyia kazi, tumekuwa tukisambaza vifaa nchi nzima bila kuangalia ukubwa wa shule au ukubwa wa jina la aliyeandika maombi. Tunatoa kwa haki bila upendeleo, kwetu sisi kila mmoja ni wetu,” alisema Kikois.

Naye mwakiliki wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwakoko, Mwalimu Naiman Kavumo alisema walikuwa na uhaba wa viti kati ya 65 hadi 100, lakini viti na meza 50 walizopokea kutoka NMB vimewapa faraja na hata wanafunzi wameonyesha nia ya dhati ya kufanya vizuri.

“Tunalo ombi moja tu kwenu, hata walimu nao wanaomba vitu na meza kwa ajili ya ofisi, lakini niwahakikishie msaada mliotupatia unatuongezea ari ya kuwa karibu nanyi. NMB wamekuwa kama wafariji wetu na ndiyo maana kila siku tunafuatilia taarifa mpya ya huduma mnazotoa,” alisema Mwalimu Kavumo.

Katika ziara hiyo ya kutembelea vituo vilivyonufaika na mradi wa CSR kutoka NMB, maofisa hao walitembelea shule za msingi, sekondari na chuo kimoja cha Polisi (CCP) pamoja na vituo vya afya ikiwemo Hospitali za Wilaya katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kwa Kanda ya Kaskazini ya NMB.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles