25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

NEC yaanza kujipanga kwa uchaguzi mkuu

Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amekabidhi magari 12 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Magari hayo ni sehemu ya magari 20 ambayo yamenunuliwa na NEC.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi magari hayo, Mhagama alisema Serikali itahakikisha kwamba NEC inawezeshwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa katiba na sheria ili iweze kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki.

“Kwetu sisi Serikali wajibu wetu wa kwanza ni kuhakikisha tume haikwami katika kutekeleza majukumu yake, hata fedha zinazohitajika katika shughuli zote za uchaguzi zinatengwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali,” alisema Mhagama.

Aliipongeza NEC kwa weledi katika utendaji kazi na kusema kwamba msingi wa uhuru wa Tume uliowekwa na Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 utaendelea kuheshimiwa na Serikali.

“Nchi kama Malawi na nyingine zinakuja kujifunza kwenye tume hii, nakupongeza sana mwenyekiti wa tume)na wafanyakazi wote. Rais, Dk. John Pombe Magufuli ametamka kwamba mwaka huu tuna uchaguzi na ametamka kwamba uchaguzi huo lazima uwe huru na haki. 

“Magari haya 12 mmepata, mtapata mengine nane na sio magari tu bali vifaa vyote vya uchaguzi vimeshafikia hatua nzuri ya manunuzi, fedha zimeshatengwa,” alisema Mhagama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NEC Jaji Rufaa mstaafu Semistocles Kaijage, alishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa tume ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuandaa bajeti na kuwasilisha Bungeni na tunalishukuru Bunge kwa kuipitisha bajeti ambayo imeiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupata magari haya, naomba shukrani zetu uzifikishe kwa Serikali na Bunge.

“ Magari haya kwa kuanzia yataanza na shughuli ya uboreshaji wa Dafatri la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili na tuna imani kwamba yatakuwa na msaada katika kuhakikisha kwamba shughuli za Tume zinatekelezwa kwa ufanisi mkubwa” alisema Jaji Kaijage.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk. Wilson Charles, aliishukuru Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) kwa ushirikiano walioutoa katika hatua zote za ununuzi wa magari hayo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles