23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Nchi yasimama

mtz1*Amani yatawala, Kasoro zaharibu utulivu

* Mamilioni wajitokeza kupiga kura vituoni

*Shughuli mbalimbali zafungwa

 

Na Waandishi Wetu

 

SHUGHULI mbalimbali jana zilisimama katika maeneo mengi ya nchi wakati Watanzania wenye sifa walipopiga kura   kuwachagua madiwani, wabunge na rais.

Watanzania  22,751,292  walitarajiwa  kupiga kura, kwa mujibu wa takwimu zilizokwisha kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wakati shughuli hiyo ikiendelea jana, usafiri wa umma na magari ya watu binafsi viliadimika barabarani huku maduka na migawaha ikiwa imefungwa.

Vilevile  katika maeneo mengine   idadi ndogo ya watu iliweza kuonekana tofauti na siku   za kawaida ambako kunakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

Jijini  Dar es Salaam, eneo la Manzese ambalo ni eneo maarufu kwa wafanyabiashara wadogo (machinga), jana lilikuwa tupu huku meza za wafanyabiashara hao zikiwa zimepinduliwa, ikiwa ni kielelezo kuwa walikuwa wameamua kupiga kura.

 

Taarifa kutoka maeneo mengi ya nchi zilisema watu walidamka saa 11 alfajiri na saa 12 asubuhi kwenda vituoni na kupanga foleni kusubiri saa 1.00 asubuhi vifunguliwe  waanze kupiga kura.

Kabla, wakati na baada ya kupiga kura   amani na utulivu vilitawala katika katika vituo vingi isipokuwa katika maeneo machache ambako zilijitokeza kasoro kadhaa.

Vilevile misururu mirefu iliweza kuonekana katika vituo vingi, hali iliyodaiwa kusababishwa na wasimamizi wa uchaguzi walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchelewesha taratibu za upigaji kura huku baadhi ya watu walionekana kuwasili  na kalamu zao kwa ajili ya kupigia kura.

Pia katika maeneo mengi ya nchi wapiga kura walionekana kutii amri ya mahakama iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopiga marufuku watu kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.

 

WAGOMBEA URAIS WAPIGA KURA

Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa akiwa na mkewe Regina Lowassa, alipiga kura nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha na kusema utaratibu ulikuwa mzuri   kama ilivyoelekezwa na NEC.

“Utaratibu wa upigaji kura ni mzuri, watu wanafuata maelekezo kama inayotakiwa… kama uchaguzi utaendeshwa kwa haki na usawa nitakubali matokeo yatakayotangazwa ila pakiwa na matatizo makubwa sitakubali matokeo, natarajia kushinda na sitegemei kinyume na hapo,” alisema Lowassa.

Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, alipiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Magufuli iliyopo Chato mkoani Geita.

Alipiga kura yake asubuhi na alipomaliza alisema ametimiza wajibu wake.

“Mimi nimetimiza wajibu wangu kama raia wa Tanzania kwa kupiga kura, siku ya uchaguzi ni moja, niwaombe Watanzania tukapige kura kuchagua viongozi watakaoongoza kwa miaka mitano lakini tumtangulize Mungu,” alisema Dk.  Magufuli.

Mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, alisema watu wa Zanzibar wamepiga kura kwa usalama na kwa Tanzania Bara wanawake wamejitokeza kwa wingi kupiga kura.

 

KASORO VITUONI

Katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika baadhi ya maeneo nchini kulikuwa na ucheleweshaji wa vifaa na kusababisha sintofahamu kwa wapiga kura.

Pia Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linawashikilia watu wanane baada ya  kuchoma moto vifaa vya uchaguzi katika eneo la Ilemba mkoani Rukwa wakihofia kuwa vifaa hivyo havikuwa  halali.

 

Inaelezwa kuwa hatua hiyo ilifikiwa  baada ya wananchi wa eneo hilo kusikia kuwa lilikuwapo  gari lililobeba masanduku ambayo tayari yamekwisha kupigiwa kura.

Inadaiwa wananchi hao walifika eneo hilo na kuchoma moto masanduku na vifaa mbalimbali vya uchaguzi.

Msimamizi wa Kituo cha Shule ya Msingi Mkapa kilichopo Busanda mkoani Geita, Salome Rafael, alisema asubuhi kulikuwa na vurugu zilizosababishwa na foleni kutokana na baadhi ya watu waliochelewa kituoni kutaka kuwapita wenzao waliotangulia.

Alisema hali hiyo ilisababisha  vurugu lakini  busara ilitumika na kuwaelekeza na hakuna nguvu ya polisi iliyotumika.  Baadaye  utaratibu uliendelea vizuri.

Katika kituo cha Kimara Temboni,   Dar es Salaam, upigaji kura ulianza saa 7.00 mchana kutokana na kile kilichodaiwa kuwa kituo kimoja cha Shule ya Msingi Temboni kilikuwa feki kwa vile hakikuwa na Daftari la Kudumu la Wapiga kura.

Msimamizi wa Uchaguzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Elizabeth alidai juzi walikabidhiwa vifaa vyote lakini daftari la kudumu la wapiga kura halikuwapo.

Alisema walifika kituoni saa 12 asubuhi  lakini baadhi ya vifaa vya kupigia kura havikuwapo hivyo alilazimika kupiga simu ili apatiwe ufumbuzi lakini alijibiwa kuwa vifaa vingeletwa na kwamba tatizo hilo lilikuwapo katika vituo vingi.

 

Hata hivyo, Mathias Makoye ambaye ni mkaguzi, alisisitiza kituo hicho kilikuwa feki kwa sababu hakikuwa na wasimamizi, karani wala daftari la wapiga kura.

Alisema baada ya kukagua masanduku hayo walikuta ndani kuna karatasi na baadhi ya vifaa vya kupigia kura huku kukiwa na karatasi iliyoandikwa kwa mkono kuwa kura zingepigwa baadaye.

Pia katika Kituo cha Kimara Temboni B wananchi walilazimika kukaa bila kupiga kura kutokana na makaratasi ya kupigia kura kuisha.

Msimamizi wa kituo hicho alisema baada ya karatasi hizo kuisha walifanya mawasiliano   wapelekewe  karatasi nyingine huku wananchi wakiendelea kusubiri.

Katika hatua nyingine, wananchi wa kata tatu za Jimbo la Kibamba walikaa zaidi ya saa nane bila kujua hatima yao ya kupiga kura kwa sababu  karatasi za uchaguzi hazikuwapo vituoni.

Wapiga kura hao wa kata za Kimara Stop Over, Saranga na Kimara B walifika katika vituo vyao kuanzia saa 10 alfajiri lakini walijikuta wakianza kupiga kura saa 9.00 alasiri.

MTANZANIA lilifika katika kata hizo saa 6.00 mchana na kukuta wananchi hao wakiwamo kina mama  wenye watoto wadogo na wajawazito, wakiwa eneo hilo huku wamekata tamaa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema waliamka mapema ili watimize haki yao ya msingi kwa wakati lakini ilikuwa tofauti.

Tito Felix ambaye ni miongoni mwa wananchi wanaoishi kata hizo alisema hadi wakati huo hakuna aliyekuwa amepiga kura na hakuna aliyewaambia chochote.

“Hadi sasa ni saa 6.00 mchana hakuna ambaye amepiga kura tulichosikia ni kwamba vifaa vya kupigia kura havijafika lakini wasimamizi wenyewe hawajatuambia chochote,” alisema Tito.

Eva Clement wa Kituo cha Shule ya Sekondari ya Royal Edp alishangazwa na NEC kushindwa kufanya maandalizi mapema wakati tarehe ya uchaguzi ilijulikana.

“Muda umeenda na hatujanza kupiga kura, naishangaa NEC kwa   miezi yote hii hawajafanya maandalizi ya uhakika,”  alisema.

Mpiga kura mwengine,   James Temba, alisema    wananchi hao hawataondoka katika eneo hilo mpaka karatasi za kura zipelekwe au Tume ikubali kuwa imeshindwa kazi.

NEC YATOA TATHIMINI

Akitoa tathimini ya uchaguzi huo nchi nzima, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima, alisema uchaguzi huo ulifanyika kwa utulivu na amani katika maeneo mengi ya   nchini lakini umeahirishwa katika vituo 29 hadi leo.

 

Akizungumza na waandishi habari Dar es Salaam jana, alisema uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na baadhi ya maeneo kufanya vurugu na kuchana maboksi na vifaa vingine vya kupigia kura.

Alisema hakuna vurugu zilizotokea katika vituo bali zilitokea katika chumba cha makabidhiano ya vifaa vya kupigia kura na baadhi ya vijana walioajiriwa na NEC walidai kuongezewa malipo ya Sh 100,000.

“Baada ya vijana hao kukataliwa walifanya vurugu na kuchana daftari la wapiga kura  pamoja na karatasi za wagombea,” alisema Kailima.

Alisema kutokana na fujo hizo vijana hao ambao sasa wanashikiliwa na jeshi la polisi walivunja masanduku ya kura, kuchana madaftari ya wapiga kura na kuharibu vifaa vinginevyo.

“Hivyo tatizo si la Tume bali la wale tuliowaamini kusimamia wametuangusha lakini watu watapiga kura na tutawapa nafasi hiyo ikiwezekana hadi saa 1.00 usiku,” alisema.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kata ya Saranga iliyopo Jimbo la Ubungo  Dar es Salaam ambako vituo 24 havikupiga kura kutokana na kukosekana kwa karatasi za ubunge, udiwani na urais.

“Maeneo mengine ni Kimara Stop Over vituo 14, Dar es Salaam na Kwera mkoani Sumbawanga ambako vijana walivamia na kulichoma moto gari lililokuwa likisafirisha vifaa vya uchaguzi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya vituo kushindwa kufanikisha upigaji kura kutokana na kukosa vifaa.

“Pia kwa upande wa Zanzibar baadhi ya vituo havikupiga kura za ubunge kwa sababu ya kukosa vifaa vya kupigia kura.

 

“Kutokana na hali hiyo, NEC imeahirisha upigaji kura hadi kesho (leo) kutokana na  baadhi ya vituo kukosa vifaa vya kupigia kura,” alisema.

Kailima alisema kuanzia leo saa 4.00 asubuhi matokeo ya ubunge yataanza kutangazwa katika baadhi ya majimbo ambayo tayari yamekamilisha upigaji kura.

Akizungumzia vituo hewa, alisema taarifa hizo si za kweli kutokana na watu kushindwa kuthibitisha kuwapo   vituo hivyo.

“Huo ni uzushi wa watu, tulitoa vifaa vyote kutokana na idadi ya vituo  na idadi ya watu walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema.

*Imeandaliwa na Grace Shitundu, Ester Mnyika na Veronica Romwald

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,020FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles