24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

MTAFITI WA TEMBO NCHINI DK. KIKOTI AFARIKI

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

MTAFITI wa tembo nchini kutoka Shirika la World Elephant Centre (WEC), Dk. Alfred Kikoti, amefariki katika Hospitali ya Rufaa ya Selian, mjini Arusha.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu jana mjini hapa, mke wa marehemu, Mariamu Kikoti, alisema mumewe alianza kujisikia vibaya juzi.

“Alikwenda Hospitali ya Selian juzi Ijumaa baada ya kuanza kujisikia miguu ikimuuma, alilazwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo walibaini kuwa figo zake zilikuwa zimeshindwa kufanya kazi. Na ilipofika saa 6 usiku alipoteza uhai akiwa hospitalini.

“Kabla ya kwenda hospitali juzi, hakuwahi kulalamika kuwa alikuwa amezidiwa sana, aliendelea na shughuli zake kama kawaida ninachofahamu tatizo hilo la figo lilimuanza tangu Juni, mwaka huu,” alisema Mariamu.

Alisema taratibu za mazishi bado hazijapangwa ambapo kwa sasa msiba huo upo nyumbani kwa marehemu eneo la Sakina, mjini Arusha.

Kifo cha Dk. Kikoti kimewashtua wengi, hasa ikizingatiwa kuwa ni miezi michache tu tangu mwanaharakati mwingine wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo wa Taasisi ya Pams Foundation, Wayne Lotter (51), kuuawa kwa kupigwa risasi na watu waliovalia kininja katika eneo la Masaki, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), Paschal Shelutete, akimzungumzia mtafiti huyo alisema, sekta ya utalii na uhifadhi imepata pigo kubwa la kuondokewa na mtu aliyetoa maisha yake kwa mnyama tembo.

“Hili ni pigo kubwa, Dk. Kikoti alitoa sehemu kubwa ya maisha yake porini kufanya utafiti wa mnyama tembo. Alishirikiana na wadau ndani na nje ya nchi kuhakikisha tembo wanaishi na kuzalisha, amekuwa na miradi mingi katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuhusu tembo.

“Sisi wahifadhi tutahakikisha tunasimamia na kuendeleza juhudi zake za kuhakikisha tembo wanaendelea kuhifadhiwa na kuongezeka kwenye hifadhi zetu nchini,” alisema Shelutete.

Hata hivyo, kupitia mitandao ya kijamii Shelutete alimzungumzia tena Dk. Kikoti akisema; “Ni hasara kubwa kwa uhifadhi wa tembo Tanzania. Nina uhakika tembo waliopo porini leo watakuwa wakilia.

“Vyombo vya habari Tanzania vitakukosa, ulikuwa chanzo cha uhakika cha habari za tembo, ulitoa maisha yako kwa ajili ya kuwalinda tembo Tanzania,” alisema Shelutete.

Dk. Kikoti msomi na mtafiti aliyejikita kwenye utafiti wa tembo na hivyo kumtambulisha kama mwanaharakati aliyekuwa akipinga kwa nguvu zote vitendo vya ujangili wa tembo ndani na nje ya nchi.

Mbali na ushiriki katika masuala ya utafiti wa tembo nchini, Dk. Kikoti alishiriki kwa karibu zaidi maadhimisho ya Siku ya Tembo Duniani na kutoa mada mbalimbali juu ya umuhimu na ulazima wa kuwalinda wanyama hao katika mikutano tofauti tofauti.

Awali kazi hiyo aliifanya kupitia Mradi wa Utafiti na Uhifadhi wa Tembo Mlima Kilimanjaro (KERP) na baadaye kuihamishia katika Shirika la Wolrd Elephant Centre (WEC).

Moja ya kauli alizowahi kuzitoa kwenye maadhimisho ya Siku ya Tembo Duniani, ni pale aliposema; “Siku hii ni siku ya wanyama wote. Lakini kwa kuwa kitaalamu tembo ndiye mlezi wa wanyama wengine, hivyo kutoweka kwake ni ishara ya uhifadhi kutoweka nchini.”

“Moja ya sifa za tembo ni kuwa na huruma na kutoa msaada kwa wanyama wengine wanapoonewa, kusaidia kufungua vichaka kwa ajili ya malisho na usalama wao.

“Tembo anatajwa kama mhifadhi mzuri wa miti kwa kuwa hula miti mbalimbali na kinyesi chake, hurutubisha ardhi na husaidia kuotesha mimea mingine.

“Tunaadhimisha Jubilei ya miaka 15, wakati tumepoteza asilimia 67 ya tembo kwa kipindi cha miaka minne tangu mwaka 2011 kutokana na ujangili.

“Hali hiyo inaashiria kuna hatari kwa wanyama hao kutoweka kutokana na kasi ya ujangili unaoendelea maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa,” alisema katika moja ya machapisho alipohojiwa na vyombo vya habari nchini.

Mbali ya kuwa mtafiti aliyebobea katika eneo hilo la tembo, kutokana na umahiri wake wa kuwasilisha mada zilitokana na tafiti zake, Dk. Kikoti alikuwa mdau wa karibu zaidi na vyombo vya habari hususan habari za utalii.

Mapambano dhidi ya ujangili kwa tembo, lugha ya kitaalamu aliyokuwa akiitumia na kuitafsiri kwa wepesi, vyote hivyo vilimfanya Dk. Kikoti kuitwa na wanahabari kwa jina la utani la Mzee wa Shoroba.

Akitoa mada katika moja ya mikutano ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Shirika la Taifa la Hifadhi (TANAPA), Dk. Kikoti alilitambulisha jina la shoroba akisema maana yake ni mapito ya wanyama.

Alikuwa akikerwa na namna baadhi ya jamii kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi kwenye shoroba za wanyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles