*Zitto, Lipumba wakwepa mtego, wautosa
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkutano ulioandaliwa leo Julai 23, 2023 na Chama cha Upinzani cha CHADEMA na kada wake wa zamani, Wilbrod Slaa, kwenye viwanja vya Bulyaga, Temeke, jijini Dar es Salaam, umepooza baada ya kususiwa na viongozi wa vyama vikubwa vya siasa nchini na wananchi.
Ingawa makada wa CHADEMA walisambaza mabango mengi kwenye mitandao ya jamii kuonesha viongozi wakubwa wa vyama vya siasa na makanisa kuwa watahudhuria mkutano huo, hali halisi iliyotokea leo ni kuwa mkutano huo umehudhuriwa na viongozi na wananchi wachache kuliko matarajio ya waandaaji wake.
Viongozi wachache wa makanisa ambao wanaegemea CHADEMA walihudhuria mkutano huo, huku wananchi wengi wakiamua kususia mkutano huo wa hadhara.
Slaa amekuwa akihangaika takribani kwa wiki nzima sasa kuandika barua kwa viongozi kadhaa wa vyama vya siasa, maaskofu wa makanisa na viongozi wastaafu wa serikali kuwaomba wahudhurie mkutano huo.
Lakini vyama vikubwa vya siasa, ikiwemo ACT-Wazalendo na CUF wameamua kutohudhuria mkutano huo baada ya kubaini nia ovu ya Slaa na CHADEMA ya kufanya upotoshaji mkubwa kwenye suala la uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam na kuchochea nyufa za dini kwa kutumia baadhi ya maaskofu.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, ni miongoni mwa viongozi wa vyama vikubwa vya siasa ambao walikwepa mtego wa kuhudhuria mkutano huo wa CHADEMA na Slaa.
Video na picha kutoka viwanja vya Bulyaga, Temeke, zimeonesha wananchi wachache kuhudhuria mkutano huo, huku wengi wakiamua kupuuzia hadhara hiyo.
Wahudhuriaji wa mkutano huo waliojitokeza ni makada wa CHADEMA kutoka Temeka na makao makuu, pamoja na viongozi wao, huku wananchi wa kawaida wachache sana wakijitokeza.
“Wananchi tumechoshwa na siasa za udini na ubaguzi wa Zanzibar na Tanganyika zinazoenezwa na viongozi wa CHADEMA kwa kisingizio cha kupinga mkataba wa bandari,” Shomari Mzee, mkazi wa Temeke stendi alisema.
“Nawashangaa sana pia hawa maaskofu kuamua kupanda jukwaani na wanasiasa wa CHADEMA kujihusisha na siasa za uchonganishi.”
Licha ya kuwa Slaa amejiweka mbele kama muandaaji wa mkutano huo, mkutano huo umetawaliwa na viongozi wa CHADEMA, huku ikiwekwa nembo ya chama hicho na picha kubwa ya Mbowe kwenye bango nyuma ya meza kuu.
Makada wa CHADEMA pia wamekuwa wakiupigia debe mkutano huo kupitia mitandao ya jamii kama mkutano wa chama chao.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ilitoa onyo kwa CHADEMA kabla ya mkutano kuwa kuwahusisha maaskofu kwenye mikutano yao ya siasa siyo sawa kwani ni ukiukwaji wa sheria za nchi ambazo zinakataza vyama vya siasa kutumia udini kufikia malengo yao.
Hata hivyo, CHADEMA wamekaidi onyo la Msajili wa Vyama vya Siasa na kuwapandisha maaskofu kwenye jukwaa katika mkutano wao wa leo wa Temeke, kinyume na sheria za nchi.
Kitendo cha CHADEMA kuwatumia maaskofu kwenye majukwaa yake ya kisiasa kinaweza kusababisha mpasuko mkubwa wa kidini nchini, na kuhatarisha tunu ya umoja na uvumiliaji wa tofauti za dini ambao umeasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.