24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

MKEMIA MKUU KUPIMA GONGO ILIYOUA WATU

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linapeleka kwa Mkemia Mkuu sampuli za vielelezo, ikiwamo ya miili ya watu waliofariki dunia juzi baada ya kunywa pombe aina ya gongo kwa ajili ya uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Lazaro Mambosasa, alisema katika eneo la tukio ziliokotwa chupa tatu zenye pombe hiyo zenye ujazo wa lita moja kila moja.

Alisema upelelezi wa awali umebaini kuwa, eneo la tukio kulikuwa kunauzwa pombe ya kienyeji na mtu mmoja aliyejulikana kama Mama Anoza.

“Vielelezo vyote pamoja na miili ya waliopoteza maisha vinapelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi ili tuweze kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo,” alisema Kamanda Mambosasa.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Maleo Ramadhani (45), Mohamed Issa (67), Kabugi Rashid (64), Stanslaus Joseph (58) wote wakiwa ni wakazi wa Kimara, Saranga.

“Wengine ni Stephen Isaya (61), Monica Rugaillukamu (42), Alex Madega (41), Hamis Mbala (35), Dikson Nyoni (28) pamoja na mtu aliyejulikana kwa jina moja la Yona, mwenye umri kati ya miaka 20 na 30.

Alisema Jeshi hilo linamtafuta Mama Anoza, aliyekuwa muuzaji wa pombe hiyo.

Kamanda Mambosasa alisema alfajiri ya Oktoba 4, mwaka huu, walipokea taarifa kutoka kwa Matigo Ramadhani kuwa ndugu yake, Maleo, alirudi nyumbani akilalamika kuumwa tumbo, kuishiwa nguvu na kizunguzungu na kumweleza kuwa alikunywa pombe kwa Mama Anoza.

“Walimpeleka Hospitali ya Mwananyamala na kupatiwa matibabu, lakini waliporudi nyumbani alifariki dunia,” alisema Mambosasa.

Alisema baada ya muda alijitokeza Paula Kisangila, akawaeleza kuwa aliporudi nyumbani hakumkuta mlinzi wake anayeitwa Yona.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Stop Over, Godfrey Misana, mmoja wa wapishi wa pombe hiyo (Monika) naye pia alifariki dunia baada ya kuonja kinywaji hicho.

Misana alisema wafiwa wote wameelekezwa na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuchukua miili ya ndugu zao kwa ajili ya maziko.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Daniel  Nkungu, alisema hadi juzi alipokea watu wengine wawili wakiwa wamepatwa na upofu, ambao aliwaandikia rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

DAKTARI

Akizungumzia sumu ya methanol inayopatikana ndani ya sprit ambayo inatajwa kama moja ya chanzo cha vifo vya watu zaidi ya 10 waliokunywa gongo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Tuzo Lyuu, alisema kwa kawaida sumu hiyo haihitajiki katika mwili wa binadamu.

“Mchanganyiko waliouweka hutengeneza vitu vingi ambavyo vina madhara makubwa kwa mwili wa binadamu zaidi kuliko pombe za kawaida ambazo tunazijua.

“Lakini wakati mwingine ni katika hiyo ‘process’ ya kutengeneza hicho kinywaji… tunajua kuna temperature tofauti za utengenezaji na kukusanya zile product ambazo zinatengenezwa.

“Kwa hiyo ukikusanya ile product katika temperature ya tofauti unaweza kupata mchanganyiko mkubwa wa ile alcohol pamoja na kitu kingine ambacho ni methanol,” alisema Dk. Lyuu.

Alisema sumu hiyo ina madhara makubwa katika mwili wa binadamu, kwani huenda kuathiri moja kwa moja baadhi ya viungo, hasa macho na ubongo.

“Yaani sumu hiyo ya methanol pindi tu inapoingia mwilini, mwili hushindwa kabisa kuzihimili na matokeo yake husababisha kifo kwa mhusika,” alisisitiza.

Habari hii imeandaliwa na TUNU NASSOR, ASHA BANI na VERONICA ROMWALD (DAR)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles