29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

Mgomi: TAKUKURU Ileje chunguzeni milioni 25 za ujenzi wa madarasa

Na Denis Sinkonde, Songwe

Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imeagizwa kufanya uchunguzi haraka wa matumizi ya Sh milioni 25 zilizotolewa na Serikali mwaka 2022 kwa ajili ya ukamilishaji vyumba viwili vya madarasa na ofisi katika shule ya msingi Chibila kata ya Luswisi.

Agizo hilo limetolewa juzi, na Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara wakupokea kero kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Mgomi ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamemlalamikia Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Anna Mwaipopo kutoshirikisha kamati za ujenzi ambapo hadi sasa ujenzi umesimama.

Mgomi amesema viongozi wanatakiwa kushirikisha kamati za ujenzi zinazochaguliwa na wananchi kusimamia miradi pindi serikali inapopeleka fedha za maendeleo kwenye taasisi na kujenga mahusiano mazuri ili miradi ikamilike kwa viwango na huduma ipatikane kwa ubora.

Amesema kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya wananchi juu ya mradi huo ameiagiza TAKUKURU wilayani humo kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha Sh milioni 25 kwenye mradi wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na atakayebainika hatua kali zichukuliwe kwa kukwamisha ukamilishaji wa mradi huo toka mwaka 2022.

“Tuziheshimu hizi kamati ambazo zilianzishwa kwa lengo la kusaidia usimamizi wa miradi, tuache kufanya manunuzi, mapokezi bila kushirikisha wajumbe wa hizi kamati kwani kufanya hivyo kunasababisha kuwa na mashaka ya matumizi ya fedha na ndiyo maana kuanzia leo TAKUKURU wanaingia kazini kufuatilia matumizi ya fedha hizi,” amesema Mgomi.

Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Stephano Konga amesema manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa madarasa umefanyika bila fundi hivyo kuwa na mashaka juu ya manunuzi na kwamba yote hayo yamefanyika kutokana na mwalimu mkuu huyo kutowashirikisha wajumbe wa kamati ya ujenzi na kupelekea mradi kukwama.

Mjumbe wa kamati ya ujenzi, Elieza Mtafya amesema kamati hizo ziliundwa kama pambo maana tangu fedha kutolewa na serikali hawajawahishirikishwa kujadili namna ya kufanya manunuzi, hivyo wanashangaa vifaa kufika kijijini hapo bila wao kujua na wameiomba serikali kufuatilia kwa kina kujua nani aliyehusika kutumia fedha hizo na mwalimu huyo.

Upande wake mwalimu Anna Mwaipopo amesema kuchelewa umaliziaji wa jengo hilo ni changamoto ya fundi hivyo tuhuma ya kutoshirikisha mafundi amesema ni uongo kwani kila mchakato wa manunuzi kamati zilihusika.

Serikali ilitoa fedha hizo Sh milioni 25 kwa ajili ya kusaidia nguvu ya wananchi ambao wamejenga vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi ya mwalimu mpaka eneo la linta lakini mpaka sasa tangu serikali itoe fedha hizo mwaka 2022 bado ujenzi umesimama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles