23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mapenzi kwa nchi yetu ni sawa na alivyoghani marehemu Shakila

marehemu Shakila
marehemu Shakila

NIMEKAA hapa jikoni kwa rafiki yangu na naangalia nje naona hali ya hewa si nzuri leo, mawingu na baridi kidogo. Mawingu yamekusanyika na hamna hata dalili ya jua. Kwa wenyeji wetu hii hali kwao si mbaya, wengi wao wanataka ubaridi kidogo baada ya muda kadhaa wa jua kali. Sidhani kama tunatofautiana sana binadamu, kila mtu katika mazingira yake anapenda yale aliyozoea. Ndio hivyo maumbile yetu.

Nimekaa hapa jikoni namsikiliza marehemu Shakila anaimba kuhusu mahaba yaliyopita, mapenzi yasiyojibiwa na maumivu ya kwenye nafsi ambayo yamekaa kama donda sugu. Sauti yake inanipeleka mbali na maneno yake yana mengi ambayo yanatugusa kimaisha.

Tamaduni yetu inabebwa na hii sauti inayolia kutakwa kupendwa, kuelewa na kuheshimiwa kama mke, mpenzi. Sauti ya kutoka kwenye jangwa la maisha na msitu wa maumivu. Sauti inaomba ukweli tu ili iweze kuendelea na maisha hata kama mwendo ni mgumu na wa kukatisha tamaa. Lakini kama jumuiya tunakwenda wapi wakati ni kudanganyana kila kona.

Roho inabaki nzito kama mawingu ambayo yanakusanyika nje ya dirisha la rafiki yangu. Ukweli uliobakia ni sauti ya marehemu Shakila ambayo inanibeba katika pori la huzuni na bahari ya majonzi.

Najiuliza utu wetu umekwenda wapi na ule ukarimu tuliokuwa nao umekwenda wapi? Mali zilikuwa si sehemu kubwa ya maisha yetu kuliko utu, utulivu, ukarimu, hekima na amani. Haya yote yamekwenda wapi?

Wakati wote mimi husema maendeleo ni mchakato wa mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kuwa ni msingi wa mambo tata ya utamaduni na mazingira na mwingiliano wao. Hapa tunachotafuta hali halisi ya wananchi je, ni maendeleo ambayo yako pia ndani ya nafsi zetu?

Maendelo yanaanza kwenye roho yako. Wanaughaibuni kuhamasishwa kuwekeza nyumbani ni jambo la msingi sana na inakuwa ni rahisi kwetu kama mapenzi ya nchi yetu yapo pale pale, hata kama umebadilisha sura ya kitabu unachoshika mkononi cha kukusaidia kupita mipakani. Shakila anaimba, “Macho yanacheka moyo unalia,” unaelezea penzi ambalo wengi wetu tunalo kwa nchi mama. Milima ya Udzungwa, Usambaa na Oldonyo Lengai inatuita na kutusuta,…..haraka haraka, mrudi nyumbani siye tupo lakini wengi wanawaacha..”

Nakaa hapa nasikiliza taarab kwenye nyumba ya rafiki yangu, kwenye mazingira mageni, mbali na hali halisi. Kwenye mazingira ambayo kila mahitaji yako ya kimwili utayapata. Lakini nafsi yako itaridhika? Maendeleo si yale ambayo unayakuta kwa mfano majumba makubwa ambayo unayasikia kwenye midomo ya watu. Maendeleo ni yale ambayo unayasikia mpaka rohoni mwako. Unaweza kutoka hatua mia moja tu, kutoka kwenye majumba yako na ukakutana na umasikini wa hali ya juu. Nyumba nzuri lakini barabara bado haijakamilika na pembeni yako kuna watu wana hali mbaya. Sasa hayo ni maendeleo ya namna gani? Lakini hii ndio hali halisi.

Kukaa Ughaibuni na kuona maendeleo ya wenyeji wako wakati hali ya nyumbani kwenu si nzuri. Utawezaje kuishi na raha moyoni wakati wenzako wana hali duni? Ndio maana tunahangaika sana huku Ughaibuni, nafsi zetu zinatusuta na zinataka tusaidie kwetu kwa nguvu zote, kile ninacho na kile ninachokiona nataka na wewe uwe nacho na pia uwe na uzoefu nacho. Kusaidia kwetu nyumbani kwa ndugu na jamaa kunawezesha wao pia waweze kubadilisha hali halisi. Lakini bado njia ni ndefu. Inafurahisha sana kuona kwamba baadhi ya wenzetu wameweza kuanzisha shule, zahanati na maduka ya dawa na wengine hata kuleta miradi mikubwa.

Juzi juzi hapa nilimtembelea Mtanzania mwenzangu ambaye sasa amelazwa, hali yake ni mbaya sana. Amefanya kazi sana miaka mingi, kusomesha wanawe na kjitengenezea mazingira mazuri nyumbani. Mara tu akapigwa na bao kubwa sana. Sasa ni mlemavu na amewekwa kwenye nyumba ya wazee na walemavu, hawezi kufanya au kwenda popote bila ya msaada wa wengine. Amejitoa sadaka kubwa sana kwa ndugu zake ambao wamebaki nyumbani. Si wengi ambao wanamkumbuka huku, amebaki na huzuni na maumivu.

Kuja kwetu Ughaibuni sababu kubwa ni kutafuta maisha na pia kuwekeza nyumbani. Wengi wetu ni kwa sababu penzi lilikuwa kubwa kuliko mvuto mwingine wowote, baada ya hapo ni watoto. Lakini moyoni mwetu nyumbani ilibaki kama jiwe zito katika nafsi zetu. Shakila anatukumbusha penzi letu kwa Tanzania ni kama …nimezama kwa mapenzi.

Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga..

Tengo Kilumanga Email: [email protected] Tel: +467051263303 Twitter: @tengo_k

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles