22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Msekwa: Tunawatumia vizuri diaspora wetu Sweden

Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, Jacob Msekwa akiwa na mwandishi wa makala hii.
Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, Jacob Msekwa akiwa na mwandishi wa makala hii.

NA SARAH MOSSI, STOCKHOLM

POPOTE pale katika nchi za Ughaibuni walipo Watanzania wataongozwa na ofisi za Ubalozi wa nchi husika kwa lengo la  kuhakikisha wanawahudumia wananchi hao walioamua kuishi huko kwa ajili ya kujitafutia maendeleo.

Jacob Msekwa ni Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, ambao unawakilisha pia nchi za Norway, Denmark, Finland, Iceland, Latvia, Lithuania na Estonia. Mwandishi wetu, SARAH MOSSI amefanya mahojiano na Mtanzania huyo ambaye anaeleza majukumu ya ubalozi wao katika  kuwahudumia Watanzania wanaoishi nchini Sweden (Diaspora). Endelea…

SWALI: Ubalozi wa Tanzania hapa Sweden unafanya kazi gani kuwasaidia hawa Diaspora katika kuishi kwao hapa?

JIBU: Nitazungumzia miaka kumi niliyokuwapo mimi tangu 2006 hadi sasa,  katika kila nchi kumekuwa na utaratibu wa Watanzania kuunda jumuiya zao au umoja wao na hali tuliyoikuta hapa Sweden wakati huo Balozi akiwa Ben Moses kulikuwa hakuna jumuiya inayowaunganisha Watanzania, walikuwa na jumuiya zao ndogo ndogo na mojawapo iliyoonekana inajaribu kuwaunganisha Watanzania ilikuwa inaitwa Kilimanjaro.

Malengo ya Jumuiya hii ilikuwa ni kuwakutanisha Watanzania katika michezo, lakini baadaye wakajaribu kuwakusanya wanachama zaidi na kuwaleta Watanzania pamaoja.

Na sisi Ubalozi tuna majukumu mawili pia, moja ni ya kibalozi ya kuwawakilisha Watanzania, lakini pia sisi ni sehemu ya Diaspora. Mojawapo tulichokifanya akiwamo balozi mwenyewe ni kuwa wanachama wa hiyo Kilimanjaro.

Hapa ubalozini masuala ya Diaspora yanapewa kipaumbele kwa sababu tunaelewa umuhimu wa maendeleo ya nchi yetu. Ingawa hili somo bado huko nyumbani halieleweki, lakini ukikaa nao utajua umuhimu wao na utajua kwamba wengi bado wanaipenda nchi yao na wanataka kusaidia.

Na unajua kuna aina mbili hapa za Diaspora, wapo wale bado ni raia wa Tanzania na wanazo paspoti za Tanzania na kuna Diaspora wale wenye uraia wa Sweden au Denmark lakini wanayo ile nasaba ya Tanzania. Hawa wote hatuwabagui na tunawachukulia kuwa ni sehemu ya Diaspora.

Katika misingi hiyo ubalozi ukaanza kushirikiana na kwa kawaida kuna sikukuu za kitaifa hapa ubalozini kama vile ya Uhuru, Muungano na Mapinduzi Zanzibar ambazo mara nyingine hufanyika hapa ubalozi na wakati mwingine hazifanyiki kutokana na uwezo wa kifedha.

Walipokuja Kilimanjaro tukakaa nao tukazungumza kwanini tusitafute siku ya Watanzania na familia zao kukutana na hiyo siku iitwe Tanzania Day, ni siku ya Watanzania kukutana na kutambuana, wale nyama choma wazungumze bila siasa yoyote. Shughuli hiyo ya kwanza ilifanyika mwaka 2007 hapa katika uwanja wa ofisi za ubalozi.

Shughuli hii ilifanikiwa kutokana na michango yao wenyewe Kilimanjaro pamoja na ubalozi kuchangia baadhi ya vitu vidogo. Hiyo ndiyo shughuli ya kwanza ya kujaribu kuwaleta karibu Watanzania. Na hii inaendelea hadi leo. Hiyo ni hatua ya kwanza.

Hatua ya pili mwaka 2010 tulipopata Balozi mpya, Mohammed Mzale, siku tuliposherehekea Siku ya Uhuru Desemba 9, aliwaeleza Watanzania kuwa angependa sana wawe kitu kimoja na licha ya umoja utawaunganisha Watanzania, lakini pia wanahitaji kiungo kitakachowaunganisha kati yao, ubalozi na Serikali ya Sweden ili kusukuma mambo yao mbele.

Akatoa wazo kwamba anzisheni kamati ya kujadili mchakato wa kuanzishwa umoja wa Watanzania na akawaeleza ubalozi upo na akatoa ofisi ambayo vikao vitakuwa vikifanyika hapa ubalozini.

Ule mchakato ulichukua miaka miwili na ilipofika mwaka 2012 ule mchakato ukakamilika na kupitishwa katiba na ndipo chama kikaanzishwa rasmi na akaendelea  kuwa Mwenyekiti Seynab Haji.

Uchaguzi rasmi ukafanyika mwaka 2014 ambao Tengo Kilumanga akachaguliwa kuwa Mwenyekiti. Lakini cha muhimu hizo process zote ubalozi ulikuwa hauingilii, walikuwa wakiwapa ukumbi na kuhakikisha mambo yote yanakaa sawa hadi kuanzisha umoja wao.

Upande wa pili wa mchango wetu kwa Diaspora, sisi tunaamini kwamba wanao mchango mkubwa sana na kuna wataalamu hapa wa fani mbalimbali na wengine si wataalamu, sisi tunajaribu kuwatumia wataalamu wetu na kuwashirikisha na mfano wakati tunasherekea miaka 50 ya Uhuru na kama unakumbuka Serikali ilitoa maelekezo sherehe zile zisherehekewe kwa aina yake.

Na hapa ubalozini tulipewa maelekezo na tuliandaa semina mbalimbali na tulimwalika mwanamitindo maarufu nyumbani, Mustafa Hassanali na hii yote ilifanywa kwa michango ya Diaspora na baadhi ya mashirika yalijitolea kusponsa yeye na mtu wake na kuhusu malazi Mtanzania mmoja alijitolea na yote ilifanyika kutokana na ushirikiano uliopo.

Siku ya kwanza tukafanya shoo kubwa sana ya Siku ya Utamaduni wa Mtanzania na siku ya pili tukafanya semina ambayo ilishirikisha mashirika makubwa na baadhi ya mabalozi na siku ya mwisho ndio ikawa Siku ya Watanzania wenyewe.

Sasa ile siku ya semina ambayo iliandaliwa na ubalozi mada kubwa ilihusu  “Miaka 50 ya uhusiano kati ya Tanzania na Sweden.” Tukaamua tuwape nafasi Diaspora wetu wataalamu waendeshe ile semina na kweli tukapata wataalamu watatu, mmojawapo ni Profesa Francis Matambalya, mchumi aliyebobea ambaye yuko Uppsala, Joyce Kimwaga, mtaalamu mahiri naye wakaendesha semina vizuri.

Na katika wale watoa mada sehemu yote ya mada zinazohusu Tanzania zilitolewa na Watanzania wasomi wanaoishi hapa.

Semina ilikwenda kwa mafanikio makubwa sana kwa sababu wengi wameishi hapa muda mrefu na wameweza kuielezea Tanzania katika lugha ambayo wenyeji wetu wameweza kuelewa. Hii ni sehemu mojawapo tunayojaribu kuwaweka karibu Diaspora.

Kingine tuko hapa Sweden tunajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kuitangaza nchi yetu kiuchumi. Hasa kiuchumi kuna kitu kinaitwa Economy Diplomacy, tunatangaza fursa za uwekezaji pamoja na fursa za biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles