27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Majaji wampinga DPP kwa hoja 9 kukwamisha dhamana ya Mbowe, Matiko

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Rufani imetupilia mbali maombi ya rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, kuhusu kupinga dhamana.

Uamuzi huo umekuja baada ya Mbowe na Matiko kuwasilisha maombi ya kufutiwa dhamana Mahakama Kuu, ambapo upande wa Jamhuri kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ulikata rufaa ya kupinga maombi hayo kwa madai kwamba yalikuwa na upungufu.

Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na jopo la majaji watatu ambao ni Stellah Mugasha, Dk. Gerald Ndika na Jaji Mwanaisha Kualiko.

Majaji hao walisikiliza hoja za rufaa iliyokatwa na Jamhuri dhidi ya wajibu rufani (Mbowe na Matiko).

Akisoma hukumu hiyo katika Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam jana, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Silvester Kaindi, alisema mahakama hiyo imetupilia mbali maombi ya rufaa ya DPP dhidi ya Mbowe na Matiko kwa sababu hoja zilizowasilishwa na upande wa Serikali hazina mashiko.

Aliagiza jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakama Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kuendelea na hatua ya usikilizwaji wa rufani iliyokatwa na viongozi hao wa Chadema ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kuwafutia dhamana zao.

HOJA YA MAHAKAMA YA RUFAA

Kainda alisema rufaa ya DPP haina mashiko kuwepo mahakamani hapo kwa sababu haikuwa sahihi kupeleka mapingamizi huku akijua kuwa alichokuwa anakipinga Mahakama Kuu ilikua imepewa mamlaka.

Alisema ni kweli rufaa iliyokatwa na wajibu rufaa (Mbowe na Matiko), ilikuwa chini ya hati ya dharura na kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo kutoka mahakama ya chini (Kisutu) hazikuwa zimeambatanishwa.

Alisema Jaji Rumanyika wa Mahakama Kuu alitimiza matakwa ya kisheria na si vinginevyo kwa kuelekeza mwenendo wa kesi ulioandikwa kwa mkono pande zote mbili zipewe ili zitumike ambapo walikubaliana pamoja.

Alisema hawawezi kupingana na Jaji Rumanyika kwa uamuzi aliochukua wa kujulisha pande zote tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo na baada ya kubaini kuwa pande zote hazikuwa na mwenendo wa kesi.

 “Kama Jaji asingewaita kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo asingeelewa wana mwenendo wa kesi au la na kwamba kabla ya kuanza kusikiliza rufaa yenyewe alianza kusikiliza mapingamizi ya awali ambao ndio utaratibu wenyewe,” alisema Kainda.

Alisema kwa maoni yao, walalamikaji katika maombi yao ya kudai Jaji alikosea kupanga kusikilizwa kwa rufaa wakati mwenendo haukuambatanishwa, yalijibiwa wakati wa kesi hiyo na wahusika walipewa nakala.

Alisema hoja ya kwamba mahakama itoe mwongozo kabla ya tarehe ya kusikilizwa, msimamo huo si matakwa ya sheria.

Kainda alisema Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuelekeza vinginevyo katika kuharakisha kusikiliza kwa kesi na kwamba hakuna haki zilizoingiliwa kama ilivyodaiwa na upande wa mashtaka na kueleza kuwa si sahihi kusema kuwa walinyimwa haki wakati mahakama iliwasikiliza.

Aliongeza kuwa mahakama hiyo ya Rufaa haiwezi kupingana na Jaji kwa sababu alitekeleza majukumu aliyopewa na sheria na kwamba kesi zote zilizoambatanishwa na rufaa hiyo hazihusiani na shauri hilo.

Mbowe na Matiko wako gerezani kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana jambo lililowafanya wakimbilie Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Wakiwa Mahakama Kuu, kesi hiyo ilikua inasikilizwa na Jaji Sam Rumanyika, lakini upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi ya kupinga maombi ya dhamana ya viongozi hao wa Chadema katika Mahakama ya Rufaa.

Wakimwakilisha DPP, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alipinga kusikilizwa kwa maombi na kutoa sababu tatu ambazo ni pamoja na kudai kuwa Jaji Rumanyika alipotoka kisheria.

Alidai katika kesi hiyo, alikwenda kinyume na kifungu cha sheria namba 362(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachoelekeza kwamba rufaa ikiwasilishwa lazima iwe na viambatanisho ikiwemo nakala ya hukumu.

Alidai baada ya uamuzi wa kufuta dhamana uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutolewa Novemba 23 mwaka jana, mawakili iliwachukua siku nne tu kuwasilisha rufaa bila kusubiri mwenendo wa kesi na nakala ya hukumu.

Alidai kwanini wajibu rufani waliacha kusubiri mwenendo wa kesi na nakala ya uamuzi pamoja na kwamba aliyekuwa Hakimu Mahakama ya Kisutu kuamuru wapewe haraka.

Alidai kushindwa kuwasilisha nyaraka hizo kunaifanya rufaa hiyo kuwa batili na sababu ya mwisho ni kwamba, hawakupata nafasi ya kusikilizwa.

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa mara kwa mara na jopo la majaji ambao walihoji haki waliyonyimwa wakati walisikilizwa.

Nchimbi alidai muda waliopewa kusikiliza rufaa ulikuwa hautoshi kwani uamuzi ulitolewa saa sita kisha wakaambiwa rufaa itasikilizwa saa nane.

Wakili Nchimbi alidai, Jaji Rumanyika, alikuwa na upendeleo wakati wa kuendesha kesi hiyo Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Jaji Mugasha, alihoji kama hiyo hoja iliwahi kuwasilishwa Mahakama Kuu na alipojibiwa kwamba haikuwahi kuwasilishwa alipinga isijadiliwe na Jamhuri waliamua kuiondoa.

Nchimbi aliiomba Mahakama ya Rufaa kuamuru rufaa iliyopo Mahakama Kuu ni batili itupwe ambapo Wakili wa wajibu rufani (Mbowe), Dk. Rugemeleza Nshalla, akijibu hoja za rufaa iliyokatwa na Jamhuri katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikuwa na nia mbaya ya kuwaumiza wateja wao.

Alidai sababu ya kwamba Jamhuri hawakusikilizwa na Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu, haina msingi sababu pande zote mbili zilisikilizwa ambao walitakiwa kulalamika ni wajibu rufani (Mbowe na Matiko) ambao Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikuwasikiliza wala kuwapa haki ya kuwasilisha kiapo kinzani kutokana na kiapo kilichowasilishwa ili wafutiwe dhamana.

Alisema Jamhuri wanadai ilikuwa vigumu kwa muda waliopewa kupitia mwenendo wa kesi kuanzia Machi hadi Novemba, jambo hilo linashangaza kwa sababu waendesha mashtaka walewale waliosababisha wajibu rufani wafutiwe dhamana ndio hao hao waliokuwepo Mahakama Kuu.

Wakili huyo alidai kungekuwa na nia njema warufani wangeruhusu rufaa ya kupinga kufutiwa dhamana isikilizwe Mahakama Kuu, kwa kuwa muda wa mwanadamu duniani una ukomo wake, hakuna mtu wa kumwongezea mwenzake muda wake uliopotea.

Alidai kuwa hauwezi kufidia uhuru wa mtu uliopotea, hali hiyo ya kibinadamu ndiyo iliifanya Mahakama Kuu kuamua kusikiliza rufaa hiyo na kuiomba mahakama hiyo kutupilia mbali rufaa ya Jamhuri kwa madai kuwa haina mashiko na iamuru rufaa ya Mahakama Kuu iendelee kusikilizwa.

Awali, Mbowe na Matiko, walifutiwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya msingi ya kufanya mkusanyiko usio halali na uchochezi.

Tukio hilo lilitokea Februari 16, 2018 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo zilizofanyika Uwanja wa Buibui, Jimbo la Kinondoni.

NJE YA MAHAKAMA

Jana wakati Mahakama ya Rufaa ikitoa hukumu yake, Jeshi la Polisi lilionekana kuimarisha ulinzi nje ya Mahakama kwa ajili ya kuwazuia wafuasi wa Chadema kuingia ndani ya Mahakama wakati kesi hiyo ilipokua inasikilizwa.

Askari wa jeshi hilo walikuwa na silaha mbalimbali pamoja na maji ya kuwasha ili kuhakikisha hakuna vurugu wala madhara yoyote ambayo yangeweza kujitokeza katika maeneo hayo.

Pengine kutokana na hali hiyo, wafuasi wa Chadema walionekana ng’ambo ya barabara katika eneo la Mahakama ya Rufaa wakisubiri kusomwa kwa hukumu hiyo.

Hadi kesi ilipoisha, wafuasi hao waliondoka huku Jeshi la Polisi likiondoka na washtakiwa Mbowe na Matiko na kuwarudisha mahabusu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles