29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAMWEKA MTEGONI MKUU WA GEREZA LA SEGEREA

NA KULWA MZEE  -DAR ES SALAAM

SUALA la Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, Harbinder Sethi  kutibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili limezua sura mpya, baada ya mahakama kutamka kwamba, asipotibiwa mpaka tarehe ya kesi itakapofika, Mkuu wa Gereza la Segerea afike mahakamani kujieleza kwanini hajafanya hivyo.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya Wakili wa utetezi, Joseph Makandege, kulalamika kwa mara nyingine kwamba mteja wake hajapelekwa Muhimbili kwa matibabu.

Makandege amewasilisha malalamiko hayo baada ya Jamhuri kuonesha kukaidi amri ya mahakama iliyotolewa mara kadhaa kwamba mshtakiwa Sethi akatibiwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Wakili huyo aliiomba mahakama itoe adhabu kwa Jamhuri kwa kukaidi amri yake, kwani kitendo hicho kina lengo la kugeuza mashtaka ya jinai na mahakama kuwa vyombo vya utesaji.

Aliiomba Mahakama kufuta kesi inayomkabili mteja wake na Mkurugenzi wa VIP, James Rugemarila, ili Sethi apate nafasi ya kutibiwa.

Alidai mashtaka dhidi ya washtakiwa yalifunguliwa kwa hila na kwamba upande wa Jamhuri umekaidi amri ya mahakama kwa kushindwa kumpeleka mteja wake Hospitali ya Taifa Muhimbili kama mahakama ilivyoamuru zaidi ya mara tatu.

Alidai kushindwa kumpeleka hospitali mteja wake kunahatarisha afya yake,  kwani akikosa kupata matibabu sahihi anaweza kupoteza maisha, kwani ana maputo tumboni.

“Kwa kuwa Jamhuri inakaidi amri ya mahakama, tunaomba wapewe adhabu na mashtaka dhidi ya washtakiwa yaondolewe ili mshtakiwa Sethi apate nafasi ya kutibiwa,” alidai.

Akijibu, Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Leonard Swai, alikiri kuna tatizo limetokea katika kutekeleza amri hiyo.

Swai alidai hawakukaidi amri halali ya mahakama, kilichojitokeza ni utaratibu wa magereza kumpeleka mshitakiwa huyo Muhimbili, lakini wako katika hatua za mwisho za kumpeleka.

“Mheshimiwa hakimu tunaomba muda wa ziada ili tuiwezeshe Magereza kutekeleza azma ya kumpeleka mshtakiwa Sethi Muhimbili, “alidai Swai.

Akitoa uamuzi wa hoja hizo, Hakimu Shaidi alisema amekuwa akitoa amri kwamba mshtakiwa wa kwanza akatibiwe Muhimbili.

Alisema mshtakiwa anatakiwa kupelekwa kwa ajili ya matibabu na endapo hatapelekwa ndani ya siku 14 mpaka siku ya kesi itakapotajwa, Mkuu wa Gereza ambapo mshtakiwa yupo afike mahakamani kujieleza kwanini amri hiyo haijatekelezwa.

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12, yakiwamo ya kutakatisha fedha na wako Gereza la Segerea kwa sababu mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria. Kesi hiyo itatajwa Oktoba 13, mwaka huu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles