24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 13, 2024

Contact us: [email protected]

Kuwa mtoto wa Rais hakuondoi haki za uraia

Na Mwandishi Maalum, Mtanzania Digital

HISTORIA ya Tanzania tangu ikiitwa Tanganyika, imepata kutambulishwa watoto wamarais au familia za marais wote sita kwa mitindo tofauti kulingana na nyakati.

Ilianza familia ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ikafuata familia ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, kisha Hayati Mzee Benjamin Mkapa, ikafuata ya Mzee Jakaya Kikwete na kufuatia ya Hayati Dk. John Magufuli na sasa ni familia ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kama ambavyo ni utaratibu, watoto wa marais wanakuwa na utajo tofauti kwa nyakati tofauti kulingana na maslahi ya wale wanaowataja iwe kwa kheri au kwa shari.

Hata hivyo, kulingana na utamaduni wa Kitanzania, hakuna mahali viongozi hawa waliwatukuza watoto wao na kuwafanya wa kipekee. Wamewapa nafasi za kusoma, kuchanganyika na zaidi ya yote kufanya shughuli za kujitafutia kipato cha halali kwa ajili ya kuendesha familia zao.

Wengine walioamua kuchagua siasa, waliendelea hadi kufikia ngazi mbalimbali ikiwemo ubunge, uwaziri na hata urais wa nchi kama tulivyoona kwa mtoto Mzee Ali Hassan Mwinyi, Dk. Hussein Mwinyi ambaye alishika nafasi mbalimbali za uwaziri na sasa ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Makongoro Nyerere wakati Tanzania ikiwa katika vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa, kutoka chama kimoja na kuingia vyama vingi vya siasa, alichagua kuwa mwanachama wa chama cha upinzani, (NCCR-Mageuzi).

Wananchi walishindwa kuelewa inakuwaje mtoto wa muasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anakuwaje mwanachama wa chama cha upinzani.

Mwalimu Nyerere kwa nafasi yake kama baba, alipoulizwa swali hili aliwaambia waiomuuliza kuwa mtoto anayo haki ya kuchagua wapi pa kwenda na nini chakufanya, madhali havunji sharia za nchi.

Sababu ya maelezo hayo ni vuguvugu lililogubika mitandao ya kijamii kwa sasa juu ya mtoto wa Rais Samia Suluhu Hassan, ndugu Abdulhalim Hafidh Ameir kuonekana akiwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda wakijadiliana kuhusu uwekezaji kwenye sekta ya nishati.

Moja kwa moja swali linalozunguka mitandaoni ni nafasi aliyo nayo Abdul, kanakwamba amefanya kosa kubwa la jinai kutafuta wasaa wa kukutana na Rais Museveni kujadiliana naye masuala hayo ambayo kimsingi yeye hatakuwa wa kwanza wala wa mwisho kufanya hivyo si tu nchini Uganda bali mahali popote duniani.

Kwanza kuna upotoshwaji mkubwa unafanyika, watu wenye nia ovu wanataka kuudanganya umma wa Watanzania kuwa mtoto wa Rais Samia amekwenda Uganda kama mwakilishi wa Rais wa nchi au waziri. Hilo halina ukweli.

Alichoandika Rais Museveni, kwa faida ya wengi ni kushukuru ujio wa kijana huyo akiwa na ujumbe wake. Labda hili neno ‘na ujumbe wake’ ndilo linalowatatiza watu na kuona labda linabeba taswira ya nchi.
 
Rais Museveni aliandika hivi: “Nimekutana na Bwana Abdul Halim Hafidh Ameir na ujumbe wake kutoka Tanzania. Tumejadiliana mustakabali wa kushirikiana katika eneo la nishati, hasa usambazaji umeme kutoka Mutukula kwenda Mwanza, itakayosaidia kusambaza katika eneo hili, itasaidia maendeleo kwa Uganda na Tanzania.
 
“Nipo sawa na ombi kutoka kwa Bwana Abdul na kikundi chake kuendelea mtambo wa kuzalisha umeme wa jua wa Megawati 20 katika Wilaya ya Nwoya, karibu na kituo kidogo cha Olwiyo. Umeme huu utaingizwa katika Gridi kuu na hakutakuwa na tatizo la umeme katika eneo hilio.”
 
Labda ni tatizo la lugha ndilo lililomfanya hata ‘Wakili Msomi’ Tundu Lissu kusambaza maneno ya kejeli dhidi ya mtoto wa rais, Abdul ameir.
 
Lissu akiwa katika mkutano wa hadhara ameonekana akimkebehi ndugu Abdul na kusema huenda huu ndio mwanzo wa kutengeneza familia ya kifalme akikumbushia baadhi ya marais waliopata kuwa na watoto waliokuwa marais wan chi, utadhani jambo hili ni geni kwa dunia ya demokrasia.
 
Ni ajabu sana kwa kiongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuminya uhuru wa rais wa nchi, mzalendo, msomi na mwenye ujuzi katika masuala ya nishati kujadiliana na taifa jirani juu ya kuendeleza nishati kwenye taifa hilo kupitia ujuzi alio nao kwa faida ya nchi na wengine, eti kwa sababu tu ni mtoto wa kiongozi.
 
Anachotaka kuwaaminisha wananchi ndugu Lissu ni kuwa siku tu mzazi anaposhika madaraka basi watoto wanapoteza hadhi ya kuwa wananchi, wanapoteza haki ya kufanya kazi, wanapoteza haki ya kutafuta maisha kwa ajili ya familia zao.
 
Kataika hali ya kushangaza, watu hao wenye nia ovu walikwenda mbali zaidi na kumhusisha ndugu Abdul na hali iliyopo sasa juu ya uwekezaji wa kampuni kutoka Falme za Kiarabu (UAE), yaani DP World.

Wakisema ndugu Abdul anamiliki ofisi nchini Dubai lakini pia amehusika kwa kiasi kikubwa kuwaleta hao wawekezaji kutoka Dubai kuja kuwekeza kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa mikataba isiyoinufaisha nchi.
 
Huu ni uonevu wa kiwango cha juu, kuendeshwa kwa dhana na kuunganisha matukio bila kutumia vielelezo vya kweli na haki,   
 
Tumeshuhudia kampuni na watu wengi wakija Tanzania kwa sura ya uwekezaji, wanapata wasaa wa kuzungumza na rais wa nchi juu ya kuendeleza mambo mbalimbali kwenye Nyanja tofauti kuanzia teknolijia, kilimo, nishati na mengine mengi.

Hatukuwahi kuwasikia hawa wanaolalamika kuonekana kijana wa Kitanzania mwenye kiu ya kujikomboa kiuchumi kupitia ujuzi alio nao kwenye sekta ya nishati, kwamba hao waliokuja kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan tena ndani ya Ikulu ya nchi, kwamba wamefanya kosa kubwa kwa sababu tu wao si viongozi wa nchi.

Kwamba ni kosa la jinai kwa raia wa Tanzania kuomba fursa ya kukutana na rais wa nchi nyingine yoyote ili kupata fursa ya kuwekeza katika nchi hiyo. Sidhani kama hili lipo kwenye katiba yetu au kwenye sheria yoyote inayoiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tumepata kuwaona wafanyabiashara aina ya Rostam Aziz akizindua biashara ya gesi nchini Kenya tena mgeni rasmi wa uzinduzi huo ni Rais Samuel Ruto. Inamana pale Rostam amefanya kosa kwa kukutana na Rais Ruto wa Kenya kwa kuwa yeye si Rais wa Tanzania wala si waziri wala mbunge?

Vijana tunahitaji kuoneana wivu wa kimaendeleo na wala si wivu wa kurudishana nyuma kwa mambo yasiyo na msingi. Mambo yanayihitajika kufanywa na washindani wetu kiuchumi yanafanywa na Watanzania wenyewe kwa kuombeana dua mbaya kwa sababu ya chuki tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles