24.3 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

KISA CHA MAMA ALIYEISHI CHINI YA MAJI SIKU 32

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


ILI binadamu aweze kuishi, anahitaji kula, kunywa, kupata hewa safi ya oksijeni na vitu vingine vingi.

Ndiyo maana tunashuhudia mara nyingi watu wanapozama ndani ya maji hasa yenye kina kirefu hufariki dunia pale wanapokosa msaada wa kuokolewa.

Hata hivyo, mambo ni tofauti kwake Tausi Waziri maarufu kwa jina la Kagunduka (55), ambaye anasema amewahi kuishi kwa siku 32 akiwa chini ya maji ndani ya ziwa Hengero lililoko katika milima ya Kolelo, Kijiji cha Lumba mkoani Morogoro.

Tausi sasa ni mganga wa tiba asilia, akitumia dawa alizokabidhiwa na mtu anayedai kwamba ni mwema ambaye amekuwa akizungumza naye tangu akiwa na umri wa miaka minane.

Ni simulizi iliyojaa visa na mikasa ambayo Tausi ameisimulia alipozungumza na mwandishi wa makala haya alipomtembelea hivi karibuni nyumbani kwake, Buguruni Malapa jijini hapa.

Katika nyumba yake, kuna ofisi ndogo ambayo anaitumia kutibu watu wanaofika kwake wakiwa wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwamo Ukimwi, saratani, kisukari, shinikizo la damu, matatizo ya uzazi hasa ukosefu wa nguvu za kiume na mengine mengi.

Ndani ya ofisi hiyo kuna kiti kimoja (cha ofisi), meza ambayo juu yake kuna vitabu ambavyo huvitumia kuandika kumbukumbu za wagonjwa wake na kiti kimoja (sofa) kwa ajili ya wateja wake.

Ukutani kumepambwa kwa picha ya Rais Dk. John Magufuli, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na nyaraka nyingine muhimu kikiwamo cheti cha usajili kutoka Chama cha Waganga na Wakunga, Tiba Asilia Tanzania ambapo namba yake ya usajili ni 0161.

Pia kuna cheti cha uthibitisho wa dawa yake iitwayo Mrinorino/ Hengero alichokabidhiwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mei 27, 2011 baada ya kuipima na kuithibitisha dawa hiyo kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Dawa hiyo ndiyo ambayo anaitumia kutibu watu wanaougua ugonjwa wa Ukimwi ambao wengi wanaporudi hospitalini hubainika kuwa hawana tena ugonjwa huo.

 

Mwanzo wa kisa

Tausi anasimulia alianza rasmi kutoa matibabu ya tiba asilia akiwa na umri miaka 10; haikuwa kazi rahisi kwake kwa sababu alipitia misuko suko mingi tangu akiwa na umri wa miaka minane.

“Nakumbuka siku moja Jumamosi nikiwa usingizini nilisikia mtu akiniambia siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wangu wa kuishi kwamba nitapata madhara makubwa na nitapelekwa Hospitali ya Morogoro kutibiwa,” anasema.

Anasema kauli hiyo ilimshtua hali iliyomlazimu kuwaamsha wazazi wake na kuwaeleza juu ya jambo hilo.

“Nilipowaamsha walishangaa, walidhani labda nilikuwa nahitaji kutoka nje kwenda kujisaidia, nikawaambia hapana… nikawasimulia nilichonielezwa na yule mtu nilipokuwa usingizini, wakashangaa!

“Wazazi wangu walishtushwa na jambo hilo, walijikuta wakipiga mayowe…punde watu walikuja nyumbani kwetu, walijaa nje wakakaa kusubiri niwasimulie kuhusu jambo hilo.

“Ilipofika saa tisa usiku, nilishtuka kuona kitu mfano wa mnyama aliyekuwa amejifunika kaniki (nguo nyeusi) akinifuata pale nilipokuwa nimekaa, nikapiga kelele kumuita mama yangu ambaye alikuwa ndani wakati huo na nikamuuliza kama ameona kitu hicho akanijibu hakioni, alikuwa mnyama mkubwa mno, niliogopa,” anasimulia.

Anasema mnyama huyo alipomfikia alimshika katika mguu wake wa kulia na kuuvunja mara mbili hali iliyosababisha avuje damu nyingi (akionesha makovu sehemu alizojeruhiwa),” anasimulia.

Anaendelea:“Mama alifika lakini hakumuona, nikamwambia nimeshaumia… aliponitazama vizuri aliona nilikuwa navuja damu nyingi na zilikuwa zinatoka pia katika sehemu yangu ya haja kubwa na ndogo, alijikuta akipiga mayowe kuomba msaada.”

Anasema watu walijitokeza wengi zaidi kumsaidia na kwamba ndugu wa mama yake walisema hakuna jinsi zaidi ya kumuacha nyumbani wasubiri afariki, wamzike.

“Baba yangu (alikuwa hai wakati huo), alipinga kauli hiyo, akawaambia ataondoka anipeleke hospitalini Morogoro na ikitokea nikafariki atanirudisha na kunizika kijijini hapo,” anasema na kuongeza:

“Wale ndugu wa mama walimbembeleza baba yangu eti wampatie mbuzi ili asinipeleke hospitalini, alikataa basi wakamsaidia kunibeba safari ya kuelekea hospitalini ikaanza.

“Ilikuwa usiku, walinibeba… walitembea hadi umbali mrefu mno, tukafika chini ya mti wa mwembe wakakubaliana wapumzike kidogo kabla ya kuendelea na safari.”

Anasema punde baada ya kumlaza chini, alishangaa kuwaona wale waliokuwa wamembeba akiwamo baba yake wakilia kwa uchungu.

Anasimulia kuwa ghafla wakati huo huo akashangaa akianza kutembea kuelekea asipokujua huku akiwa na majeraha yake.

Anasema akiwa anaendelea kutembea, alishtuka kusikia sauti ya mama mtu mzima ikimuita na kumuuliza alipokuwa akielekea.

“Nilishangaa, nikamjibu sijui ninapokwenda, akaniuliza iwapo nimekula, nikamjibu hapana… akanipatia kitumbua, nikala.

“Yule mama akaniambia mbona unaogopa, nikamjibu kwa sababu nimeota ndoto mbaya, wakati huo niligeuka kuangalia nyuma nikaona nilikuwa mbali mno kutoka pale walipokuwa baba na wenzake.

“Wakati nikiendelea kula kile kitumbua, nilimuuliza yule mama mbona kuna mwanga wa taa akanijibu nilikuwa nimefika kwenye kijiji kingine, akaniambia turudi pale walipokuwa wamekaa baba na wenzake kwani walikuwa wanataka kuanza safari kurudi nyumbani kunizika kwani nimekufa.

“Nilishtuka, ananiambia nimekufa wakati najiona nipo hai! nikamkatalia, tukaanza safari ya kurudi hadi pale kwenye mwembe, tulipofika aliniambia nisimame jirani na baba yangu nilishangaa hakuniona hata nilipomuita baba yangu hakuitika,” anasimulia.

Anaendelea: “Nikamuuliza yule mama mbona baba yangu haitiki, akanijibu kwa sababu nimekufa, akaniambia tena nisimame jirani na dada yangu ambaye naye hakuniona, ndipo yule mama akaniambia sasa nakuamsha, akaniambia ‘zinduka’ ghafla nikaamka kutoka usingizini na kuinuka pale nilipokuwa nimelala.

“Kitendo hicho kiliwashtua baba na wenzake, wakasemezana ‘anatudanganya, atakufa tena’ nikawaambia najua nia yenu mnajua nimekufa, lakini sijafa… nimeenda mbali na nimekula kitumbua hiki nimeshika mkononi mwangu.

“Baba alikiona, akakichukua kile kitumbua na kukila huku akiniambia kama kufa na tufe wote,” anasimulia.

Anasema aliwaeleza hawakuwa porini kama wanavyodhani bali ni kwenye kijiji na punde jogoo aliwika, wakaanza tena safari kuelekea Morogoro.

“Kulikuwa kumekaribia kupambazuka, walinibeba hadi kituo cha mabasi cha Mtamba tukapanda basi kuelekea Hospitali ya Morogoro wakati huo tumbo langu lilikuwa limejaa, damu ilivilia tumboni,” anasema.

Anasema mguu wake wa kulia ambao ulijeruhiwa na mnyama yule nao ulikuwa umepanda kwa juu na kuingia tumboni, ukawa mfupi kama mlemavu.

Anasema walipofika Hospitali ya Morogoro alilazwa katika kitanda namba 17, baba yake alitoka kwenda kupiga simu  wale ndugu wa mama yake waliokuwa wameongozana nao walitumia mwanya huo kuwakimbia na kuwaacha wenyewe.

“Nikabaki mwenyewe na baba yangu, nikafanyiwa upasuaji wakanitoa mifupa iliyokuwa imepasuka, nikawekea chuma ili kuushikilia, nilikamuliwa damu kiasi cha sinia moja, niliendelea kuugulia pale hospitalini na baba alienda kuishi Kiguru-Nyembe kunisubiri nipone.

Anasema alikaa hospitalini hapo kwa muda wa miaka miwili na hiyo ilitokana na kitendo cha yeye kushindwa kuufanyisha mazoezi mguu wake.

“Nilichelewa kupona kwa sababu kila alipokuja daktari kunielekeza jinsi ya kutingisha mguu kuufanyisha mazoezi, sikuweza lakini nilipokuwa usingizi yule mtu alikuwa anakuja na kuniamrisha nitingishe mguu na nilikuwa naweza,” anasimulia.

Anasema usiku mmoja mtu yule alikuja na kumuuliza siku inayofuata ni tarehe ngapi akamjibu tarehe moja baada ya kumjibu aliondoka.

“Asubuhi baba alikuja kunitembelea, aliniletea embe moja na kuniaga kwamba anaelekea kijiji cha Mzinga kutafuta kibarua kwani fedha zote alizokuwa nazo zimekwisha,” anasema.

Anasema punde baada ya baba yake kuondoka daktari alikwenda na kumjulisha kwamba amepewa ruhusa kurudi nyumbani na atapaswa kurudi hospitalini hapo baada ya muda wa mwezi mmoja ili aondolewe chuma alichowekewa katika mguu wake.

“Nikawaambia wamkimbilie baba kwani alikuwa anakwenda mbali, walifanikiwa kumuita… alipokuja alisikitika na kuhoji tutaondokaje kwa sababu hakuwa na fedha za usafiri.

“Nikamwambia asijali, aite gari kwani nilikuwa nimehifadhi fedha ambazo nilikuwa napewa na wasamaria wema waliokuwa wakija kuwajulia ndugu zao walinipatia na mimi fedha kidogo,” anasema.

Anasema walitumia fedha hizo kwa nauli waliita gari ambalo liliwapeleka hadi nyumbani kwa shangazi yake mkubwa eneo la Kihonda huko huko Morogoro.

“Hata hivyo, sikupenda kukaa pale kwa shangazi, nikamwambia baba lazima turudi nyumbani, tukaondoka sikurudi tena hospitalini kuondolewa vile vyuma, nikiwa nyumbani yule mtu aliendelea kunijia na kuniamrisha nifanye mazoezi ya mguu, nilikuwa naweza lakini ndugu zangu wakinielekeza sikuwa naweza kutingisha mguu wangu,” anasema.

Mauza uza chooni

Anasema siku moja (Jumanne) mama na ndugu zake waliondoka kuelekea shambani kwao kupiga maharagwe na yeye alibaki mwenyewe nyumbani.

“Basi nilitoka ndani kwenda chooni kujisaidia lakini nilipofika nilishangaa sikuona shimo la choo… kulikuwa kumefunikwa na jani la mgomba ambalo lilitandikwa katika eneo lote la choo,” anasema.

Anasema aligeuka nyuma ili arudi ndani kwani alishindwa kukitumia choo hicho alichokumbana nacho ni giza nene lililomfanya ashindwe kuona kitu kilichokuwa mbele yake.

“Nilikuwa kipofu, macho yangu yaligoma kabisa kufunguka, nilihangaika kutembea huku na huko kwa lengo la kufika ndani lakini sikufanikiwa, kumbe wakati huo nilikuwa nikitembea, niligundua nilipogeuzwa ghafla na nilipofumbua macho niliona nimetembea umbali mrefu na nyumbani nilipaona ni mbali kutoka pale nilipokuwa,” anasimulia.

Anasema: “Nilikuwa nimepotea na sikuwa najua nilipokuwa naelekea, punde nilijikuta nikiingizwa ndani ya ziwa Hengero, niliteremshwa hadi chini kabisa ya ziwa, kilichonishangaza, nilipofika kule chini maji yalijitenga (yalinizunguka)na pale nilipokuwa sikuwa nimelowana hata kidogo, palikuwa pakavu kabisa.

Anasema aliishi chini ya maji ndani ya ziwa hilo kwa muda wa siku 32 bila kula chakula cha aina yoyote zaidi ya kunywa maji ya ziwa hilo pekee.

“Nilikuwa nikihisi kiu, nanyanyua mikono yangu kuelekea juu kama vile nakinga maji, basi yanatiririka kwenye mikono yangu nakunywa hadi natosheka nikitoa mikono yanakata, nikiwa kule chini ya maji yule mtu alikuwa akiniambia nisijali, ipo siku nitatoka nikiwa mzima ndani ya ziwa hilo,” anasimulia.

 

Msako duniani

Anasema akiwa kule chini ya maji, wazazi wake waliendelea kumtafuta wakiamini amepotea.

“Walinieleza walikwenda hadi kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli, walijua nimechezewa na kuna mganga mmoja aliwaeleza kuna baba mdogo ndiye aliyenichukua, lakini kweli haikuwa ukweli,” anasema.

Anasimulia wakati wazazi wake wakihangaika huku na huko kumtafuta, mzee mmoja aitwaye Kiraka (sasa ni marehemu) ambaye alikuwa akiishi kijijini humo aliwaeleza kuwa wasihangaike kunitafuta kwani nimo ndani ya ziwa hilo.

“Mzee Kiraka alikuwa mlemavu (anaugua ukoma) naye aliwahi kupotea katika mazingira ya kutatanisha akiwa juu ya mlima, kinachoshangaza wengi ni namna gani aliweza kupanda juu ya mlima huo.

“Mzee huyo aliwaeleza kwamba ndani ya ziwa hilo kuna watu wengi wamepelekwa na wanaishi humo, aliwapatia dawa maalumu, aliwaeleza wakifika jirani na ziwa hilo wasigeuke kuangalia upande ambako kumejengwa nyumba iliyo jirani na ziwa hilo bali waende moja kwa moja ziwani na watupe dawa hiyo.

“Kutoka kwa mzee huyo hadi ziwani ni umbali wa saa sita hadi saba, walimuacha nyumbani lakini walipofika ziwani walishangaa kumkuta mzee huyo akiwa amefika, aliwacheka lakini walizingatia yale aliyowaagiza, walitupa dawa ile ziwani na maji yakajitenga.

“Huku juu waliona yamesambaa kuelekea kwenye mawe ya pembezoni mwa ziwa, mimi kule chini nilishangaa kuona mawe yakijitengeneza mfano wa ngazi kiasi cha kuniwezesha kupanda juu, nilipanda nikikanyaga jiwe moja baada ya jingine hadi nikafika juu, nilifurahi kuwaona wazazi wangu.

“Nilikuwa mweupe mfano wa mtu aliyeishiwa damu, nilimsikia mama yangu akiwaambia si yeye (Tausi) kwa jinsi nilivyokuwa nimebadilika aliwaambia wametoa mtu mwingine, nikamwambia ni mimi na nikawaambia wimbo ambao nilikuwa naupenda mno, tukaondoka kurudi nyumbani,” anasimulia.

 

Maisha mapya

Anasema siku tatu tangu alipotolewa kule ziwani alisikia tena sauti ya yule mtu ambaye huzungumza naye ikimueleza kwamba anapaswa kutolewa nje (kuchezwa unyago) kwani amekuwa mwali.

“Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 10 hata maziwa hayakuwa yametoka kifuani, wazazi wangu walitekeleza agizo hilo,” anasema.

Anasema baada ya shughuli hiyo mtu huyo alimjia tena na kumueleza, kwamba kuna ugonjwa unaitwa Juliana ambao upo duniani wanadamu wanakufa kwa mateso kwani hakuna dawa inayoweza kuutibu.

“Wakati ule ugonjwa huo ulijulikana zaidi kwa jina la Juliana ambao ndio Ukimwi, wakati huo hata dawa za kurefusha maisha (ARV’s) zilikuwa hazijagundulika, watu wengi walikuwa wanapoteza maisha, kwa hiyo mtu yule aliniambia atanipa dawa ya kutibu ugonjwa huo.

“Siku moja alikuja na kifurushi (kiroba) ambacho kilikuwa na dawa hizo, basi akaniwekea kichwani kama vile mto, nilikuwa usingizini, niliposhtuka nilimuita mama aje anisaidie kuwasha taa, alipowasha niliona mzigo umewekwa pale nilipokuwa nimelaza kichwa changu.

“Mama aliniuliza ni kitu gani, nilipofungua nilikuta ni dawa, nikawa nazichambua na yule mtu aliniagiza nizishike ili niwasaidie watu, wakati nachambua aliendelea kunipa maelekezo ya kila aina ya dawa kati ya zile alizonipatia,” anasema.

Anasema nilipewa dawa zenye uwezo wa kutibu Ukimwi, matatizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume, kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine mengi.

“Akaaniambia nisiziogope, akanitaka nichukue nile… nikala, mama akaogopa, akaniuliza nani kazileta nikamwambia usiogope, kichwa changu tu,” anasema.

 

Aanza kutoa matibabu

Anasema siku moja mama mmoja ambaye alikuwa na umri wa miaka 50 alifika nyumbani kwao akidai kupata maumivu ya tumbo.

“Nilichukua zile dawa nilizoambiwa ni za uzazi nikampatia, mama yule hakuwahi kupata mtoto, baada ya miezi sita alianza kupata kichefu chefu kumbe alikuwa amepata ujauzito,” anasema.

Anasema ilipofikisha muda wa miezi tisa alisikia sauti ya yule mtu ikimuelekeza akampatie dawa nyingine yule mama.

“Nilipompatia dawa niliyoelekezwa mama yule alijifungua watoto pacha, hapo ndipo nilipoanza safari ya kutibu watu,” anasimulia.

Anasema siku nyingine akiwa nyumbani, kuna watu walipita wakiwa na ndugu yao mgonjwa, alikuwa amefungwa nailoni kumsitiri, alikuwa anaumwa kweli kweli chochote alichokula alikuwa anatapika.

Anasema alipowahoji walisema wametokea mjini na mgonjwa wao alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Ukimwi, akampa dawa.

Anasema baada ya kunywa alitokwa jasho jingi wakampakia uji alipomaliza kunywa alilala usingizi mzito.

“Alipoamka alisema anahisi mwili wake umepata nguvu, wakaenda kumuogesha bafuni, aliporudi nilimpatia tena dawa, nikawaagiza wamnyoe nywele, wakafanya hivyo, afya yake iliimarika na waliondoka kurudi mjini, nikawaomba wanaporudi waninunulie mbuzi 10 ili na mimi nifuge,” anasema na kuongeza:

“Alitumia dawa nilizompatia kama muda wa mwezi mmoja, alipoenda hospitalini walipompima hakuwa tena na Ukimwi, dawa zake zilipoisha alikuja tena kule kijijini na alikuja na mbuzi nikafurahi, nilianza kufuga.

 

Idadi ya waliopona

Anasema wagonjwa wengi ambao huenda kutibiwa kwake ni wale ambao majibu ya vipimo vya hospitalini yanaeleza kwamba haiwezekani tena wao kutibiwa na kupona.

“Mwaka juzi pekee nakumbuka nilitibu wagonjwa 900 kati ya hao wapo waliokuwa wanaugua Ukimwi, matatizo ya uzazi… wengi wamepata watoto kiasi cha kujaza shule mbili za msingi au sekondari,” anasema.

 

Dozi inatolewaje?

“Kwa kawaida huwa mgonjwa ananunua kikopo kimoja cha dawa na atapaswa kutumia dozi mara tatu kwa siku, kwa kutumia kijiko kidogo ambacho mara nyingi hutumika kuweka sukari kwenye chai.

“Mgonjwa huchota dawa kiasi kwa kutumia kijiko hicho bila kukijaza na kuweka kwenye uji kisha kunywa uji huo asubuhi, mchana na jioni.

“Kinachoumiza watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Ukimwi ni kule kushuka kwa kiwango cha kinga za mwili (CD4) kwa hiyo anapotumia dawa ninayompatia huenda kusaidia mwili wake kupandisha  CD4 zake.

 

Gharama za matibabu

Anasema si kubwa kama ambavyo wengi hudhani, kwa dozi moja ya kutibu ugonjwa wa Ukimwi humtoza mgonjwa kiasi cha Sh 250,000.

“Nalazimika kuwatoza gharama kidogo kwa sababu ili nipate dawa hizo inanibidi kufunga safari kwenda mkoani Morogoro hivyo huwa natumia nauli na kuwalipa vijana wanaonisindikiza kwenda msituni.

“Huwa naambatana na vijana watatu na nikishavuna dawa huwa kuna gharama za kuisaga kuziweka katika vifungashio ndipo niwapatie wagonjwa,” anabainisha.

Imethibitishwa ubora

Cheti cha uthibitisho ambacho MTANZANIA imekiona ofisini kwa mama huyo kinaonesha sampuli za dawa hiyo Mrinorino/ Hengero zilichukuliwa Mei 26, 2011 na ilifanyiwa uchunguzi Mei 26, mwaka huo.

Matokeo ya uchunguzi huo ambayo yameandikwa katika cheti hicho yanaeleza, ndani ya sampuli hiyo kulikutwa ‘alkalids’ na kwamba ni dawa zitokanazo na mimea au kutengenezwa (synthesized) na hutumika kutibu magonjwa ya binadamu.

Tausi anasema alikuwa apewe kitengo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) lakini ameshindwa kukaa huko kwani kila anaposikia ndugu wa mgonjwa wakilia na yeye machozi huwa yanamtoka.

“Siwezi kuvumilia ninapoona mtu analia, huwa napatwa na uchungu na mimi najikuta nikilia pamoja naye,” anabainisha.

 

Simulizi ya mgonjwa

Nikiwa naendelea kufanya mahojiano na Tausi, anaingia mama mmoja ambaye ananieleza kuwa ni miongoni mwa wagonjwa ambao anaowatibia.

Mama huyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, anasema Tausi amemsaidia kutibu tatizo la uzazi ambalo lilikuwa likimsumbua kwa miaka mingi.

“Nilikuwa sipati ujauzito, mume wangu alitaka kuniacha, rafiki yangu mmoja akanileta kwa huyu mama, akanipatia dawa nikaanza kutumia hadi sasa nimebahatika kupata watoto wawili na sasa kama unavyoniona nina ujauzito mwingine natarajia kupata mtoto wa tatu,” anasema kwa furaha.

Je, anapiga ramli

MTANZANIA lilimuuliza mama huyo iwapo hao aliokuwa akiwasiliana nao ambao walimkabidhi dawa hizo ni wachawi au mizimu ya kwao! na iwapo anapiga ramli anapotibu wagonjwa wake.

Anasema: “Hapana siamini kwamba dawa hizi nilikabidhiwa na wachawi au mizimu na wala sipigi ramli ninapokuwa namtibu mgonjwa.

Anasema haamini kabisa katika kupiga ramli na huwa hapendi waganga wanaotibu watu kwa kutumia njia ya kupiga ramli.

“Wale wanaopiga ramli mara nyingi ni waongo, awali nimeeleza wazazi wangu walienda kwao na walidanganywa na ndio hao ambao huelekeza kuua watu wenye ulemavu wa ngozi ili wapate utajiri jambo ambalo si kweli,” anasema.

Mipango yake

Anataja mipango yake ya baadaye kuwa ni kuendelea kusaidia watu wanaougua magonjwa mbalimbali kwa kutumia dawa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles