25.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: MAJIZI CCM YANAKIMBILIA CHADEMA

BENJAMIN MASESE NA JUDITH NYANGE – MWANZA

RAIS Dk. John Magufuli amesema yalikuwapo majizi CCM kuliko hata ya Chadema na wengine wametoka kwenye chama hicho tawala na kukimbilia chama hicho cha upinzani.

Alisema pia kuwa wapo waliopo Chama cha Wananchi (CUF) wengine ni wabaya sana.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mkuyuni jijini Mwanza.

“Ndiyo maana tumeamua kuijenga reli ya umeme na sio ya kuendeshwa na dizeli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa fedha za ndani za Watanzania Sh trilioni 7, nataka niwaambie kwamba hata kama itachukua miaka 10 itafika Mwanza na speed (mwendo kasi) yake ni kilomita 160 kwa saa.

“Tunataka Tanzania mpya, hilo ndiyo lengo langu na ndiyo maana nilipofika hapa sikusema CCM oyee kwa sababu yapo yaliyokuwepo CCM yalikuwa majizi sana kuliko hata ya Chadema.

“Ndiyo maana mimi niko hapa sijasema Chadema oyee, kwa sababu yalikuwepo majizi CCM yakakimbilia Chadema, ndiyo maana sijasema CUF oyee, kwa sababu wapo waliopo CUF wengine ni wabaya sana, mimi nataka maendeleo, nasema Tanzania oyee, kwa sababu Tanzania inatakiwa kujengwa na Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

 

AWATAKA WAWEKEZAJI KUJITATHMINI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli wakati akizindua kiwanda cha kuzalisha dawa za binadamu cha Prince Pharmaceutical Ltd kilichopo eneo la Buhongwa mkoani Mwanza, alitoa wiki mbili kwa wawekezaji wa viwanda vya Keko Pharmaceutical Ltd na Tanzania Pharmaceutical Ltd vya Dar es Salaam, ambavyo pia Serikali ni mbia, kujitathmini  juu ya kusuasua kwa uzalishaji wake na wakishindwa watanyang’anywa na kugawiwa kwa wawekezaji wengine.

Agizo la Rais Magufuli lilitokana na kauli ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliyewataka wawekezaji hao kuonana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Elisante ole Gabriel kumweleza mikakati yao kabla ya Serikali kuchukua uamuzi wake.

“Tanzania ina viwanda 13 vya kutengeneza dawa za binadamu, lakini vinavyofanya kazi ni vitano. Kati ya hivyo vitano, viwili vinasuasua, tena ndivyo ambavyo vina ubia na Serikali, hivyo natoa mwezi mmoja kwa mwekezaji kama atashindwa kuchukua hatua, Serikali itavichukua, kama nguo imekubana ni vema ukaivua na kumpa mdogo wako.

“Kabla ya kuchukua hatua hizo, wawekezaji hao nendeni mkaonane na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Elisante ole Gabriel na kumpa mikakati yenu kabla ya Serikali kuchukua uamuzi,” alisema.

Aidha, Mwijage alidokeza kuwa kuna wawekezaji watano wameonyesha nia ya kuwekeza nchini na katika kipindi cha miezi 18, lazima kutakuwa na viwanda vitatu vitakuwa vimejengwa na wawekezaji hao, pia  ndani ya miezi 12 lazima kuwepo na kiwanda cha kuzalisha matone maji (drip) kwani Serikali inatumia Sh bilioni moja kuagiza nchini Uganda.

 

JPM ASHANGAZWA MAJI YA DRIP KUAGIZWA NJE

Akizungumza jana, Rais Magufuli alishangazwa na kutokuwapo na hata kiwanda cha drip, mabomba ya sindano na pampas hapa nchini, huku vyote  vikiagizwa kutoka mataifa mengine.

“Hata mimi mwenyewe najua kutengeneza maji ya drip, wanafunzi wa chuo waliosoma kemia kwa kidato cha nne na sita wanajua kutengeneza, kwanini tusitengeneze maji ya drip badala yake tunanunua Uganda? Tunashindwaje kuwatumia wanafunzi au wahitimu wa kemia kutengeneza?” alihoji.

Pia alitoa angalizo kwa mwekezaji wa Kiwanda cha nguo cha Mwatex kilichopo Mwanza, kuhakikisha kinaongeza uzalishaji na kuacha visingizio na kama ameshindwa ni vema kukiachia ili kukabidhiwa mtu mwingine.

Rais Magufuli alionyesha pia kushangazwa na mwekezaji wa kiwanda hicho, kupewa kingine Mbeya na sasa hakifanyi kazi ipasavyo.

 

UJUMBE KWA WAFANYABIASHARA

Pia Rais Magufuli aliwatumia ujumbe wafanyabiashara, kwamba wasilalamike pesa kukosekana mifukoni badala yake watumie fursa ya Tanzania ya viwanda kuwekeza ili Serikali iweze kuwapatia zabuni na hatimaye watapata fedha kwa urahisi.

“Pesa zipo nyingi, lakini za bure hazipo na hazitakuja kamwe, lazima mzitafute kwa kufuata mkondo mzuri ambao ni kuwekeza kwenye viwanda na masoko yapo likiwamo la Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki lenye watu  milioni 165, pia kuna soko la nchi za Jumuiya ya Nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), ambalo lina watu milioni 400, hivyo ukiwekeza kwenye viwanda utapata wateja wengi huko,” alisema.

Rais Magufuli aliwaonya wafanyabiashara wa dawa kutotumia fursa ya soko la ndani kupandisha bei ya bidhaa hizo, badala yake ziwe nafuu ili Serikali iweze kuangalia kuongezea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa zile zinazotoka nje ya nchi na kuwaondolea wazalishaji wa ndani.

 

WAZIRI UMMY

Kwa upande wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Kiwanda cha Prince Pharmaceutical kitaokoa zaidi ya asilimia 80 ya dawa zilizokuwa zikiagizwa nje ya nchi.

Alisema Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD), wameanzisha mpango wa kununua dawa kutoka kwa wazalishaji wa ndani.

Waziri Ummy alisema tayari zabuni imetangazwa na mikataba 10 kwa wazawa imetolewa yenye thamani ya Sh bilini 20.6 hadi Oktoba mwaka huu.

“Kwa bahati nzuri, MSD imeteuliwa na SADC kuwa mnunuzi wa dawa za nchi 15 ambazo zitanunuliwa katika viwanda vya hapa Tanzania, kikiwamo hiki cha Prince, pia tuna mpango wa kujenga kiwanda kinachozalisha bidhaa za pamba mkoani Simiyu.

“Pia Global Fund wameahidi kutusaidia magari 190 ya kusambaza dawa nchi nzima na yatakuwa yakionekana mara kwa mara kama ilivyo magari ya Coca Cola, vile vile si kwamba tunaendelea kununua drip nje ya nchi, mpango wetu ni kujenga hapa hapa,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Prince Pharmaceutical, Hetal Vetalan, alisema kiwanda hicho kinazalisha aina 26 za dawa na moja ya glucose na wamepata zaidi ya Sh bilioni 222.5 kutoka serikalini baada ya kuanza kununua dawa kiwandani hapo.

Awali, Rais Magufuli alifungua kiwanda cha kutengeneza bidhaa za plastiki cha Victoria Moulders & Polybags kilichopo Igogo, ambako alimpongeza mwekezaji kwa kuzalisha bidhaa ambazo zinauzwa hapa nchini na nje ya nchi.

Pia alimtaka mwekezaji huyo kukitanua kiwanda hicho ili kuboresha masilahi kwa wafanyakazi.

 

AUNGA MKONO JUHUDI ZA WANANCHI

Akiwa kiwandani hapo, alitoa Sh milioni tatu kwa lengo la kununulia mifuko 100 ya saruji kwa shule mbili zilizopo ndani ya kata hiyo.

Rais Magufuli alimkabidhi fedha Diwani wa Kata ya Igogo, John Minja, akiunga mkono juhudi za wananchi wa kata hiyo katika kuboresha miundombinu.

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, alimweleza Rais Magufuli kuwa wananchi wa kata hiyo wamechanga Sh milioni 15.8 kujenga matundu ya vyoo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwa aliwahi kuishi ndani ya kata hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Victoria Moulders & Polybags, Manjist Singh, alisema bidhaa zinazozalishwa hapo zinauzwa Uganda, Rwanda, Burundi na ndani ya nchi na kuongeza kuwa alikianzisha kutokana na uwepo wa shughuli za kilimo na madini.

Hata hivyo, aliomba Serikali kupunguza matatizo yaliyopo soko la ndani kwa kuondoa utegemezi wa bidhaa za nje kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji wa ndani.

 

Meya aibuka kwa JPM

Katika hali isiyotarajiwa baada ya jana kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa saa sita, Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, alipongeza jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli na kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.

Hata hivyo, wakati akizungumza, minong’ono na vicheko vya chini chini vilitawala, hasa kwa madiwani wenzake, huku wananchi wakimshangilia.

Bwire alimweleza Rais Magufuli kwamba amepokea maelekezo yake ya kuwataka kukaa meza moja na kutatua matatizo yao ya ndani.

Alisema binafsi ameridhia kukaa na anaamini wenzake wamemwelewa Rais Magufuli.

Hata hivyo, alimwomba Rais Magufuli pale atakapopata muda kama itampendeza, kumpa nafasi ya kumwona kwani ana jambo binafsi la kumsimulia na asingeweza kuliongea hadharani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles