29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

JAMII YATAKIWA KUWEKEZA ELIMU KWA WALEMAVU

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

JAMII imetakiwa kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu na badala yake kupambana kuhakikisha walemavu wanapata huduma zote muhimu ikiwemo elimu.

Hayo yalielezwa jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika  Mtaa wa Mbalawala Kata ya Mbalawala, mjini hapa ambao uliwakutanisha watu wenye ulemavu na wananchi wa kata hiyo.

Katika mkutano huo jamii ilikuwa ikipewa elimu kuhusiana na haki za watu wenye ulemavu hususani vijana, kupitia mradi wa ‘Kijana paza sauti yako shiriki katika utekelezaji wa sera za umma na  mipango ya maendeleo’.

Mradi huo unadhaminiwa na Foundation for Civil Society kwa kushirikiana na Shirikisho la watu wenye ulemavu (Shivyawata) Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwezeshaji kutoka Shivyawata, Aisha Kayumba, alisema jamii inatakiwa kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu na badala yake inatakiwa kuhakikisha wanapata elimu ili iweze kuwasaidia katika maisha yao.

“Kama kijana anakosa ajira vipi kwa huyu mlemavu, hivyo nawaomba muunde klabu za vijana  mchanganyiko yaani wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu ili kuzikimbilia kwa ukaribu fursa ikiwemo ajira,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kata ya Mbalawala, Musa Matonya, aliishukuru Shivyawata kwa kuwapa elimu hiyo kwani wengi walikuwa hawajua kama haki zao ni zipi.

“Tunashukuru kwani wengi tulikuwa hatujui haki zetu ni zipi, lakini kupitia mradi huu na mkutano huu wa hadhara umetusaidia kutambua haki zetu na tutajiunga kama vikundi ili fursa ziweze kutufikia kirahisi,” alisema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Silvester Mang’ata (CCM), alisema wao wamekuwa nyuma kwenye mambo ya walemavu hivyo akadai mafunzo hayo yamewasaidia vijana kuchangamkia fursa.

“Haya ni mafunzo muhimu sana kwa vijana, tunaomba mafunzo kama haya yaje mara kwa mara ili kuibadilisha jamii ya vijana kwamba wao ndio taifa la leo na si la kesho,” alisema Diwani huyo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles