24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi la Polisi Tanzania laanza kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Jinai

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi (DCP), Mwamini Rwantale, ametangaza kuwa Tanzania inajiunga na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Jinai, ambapo sayansi hiyo inatoa mchango mkubwa katika kutoa haki na kubaini wahalifu.

Rwantale alisema kuwa kila mwaka ifikapo Septemba 20, dunia inaadhimisha siku hiyo ili kuwakutanisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi katika juhudi za kutatua uhalifu. Hata hivyo, kwa Tanzania, ni mara ya kwanza kuadhimisha siku hii muhimu tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi mwaka 1955.

Akizungumza leo kwa niaba ya Kamishna wa Polisi wa Uchunguzi wa Kisayansi, katika hafla iliyofanyika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini, DCP Rwantale alieleza kuwa uchunguzi wa kisayansi umeleta mafanikio makubwa katika kuhakikisha haki inatendeka. Alisema uchunguzi huo umesaidia kubaini wahalifu kwa urahisi na kuwafungulia mashitaka ipasavyo, huku wasio na hatia wakiwekwa huru.

“Uchunguzi wa sayansi ya jinai umesaidia kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa umekuwa chombo cha kubaini wahalifu bila shaka yoyote, na pia kusaidia kuwaachia huru wasio na hatia,” alisema DCP Rwantale.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, DCP Dk. Lazaro Mambosasa, alisema uchunguzi wa kisayansi hauruhusu mtu asiye na hatia kuadhibiwa, na unaleta taswira njema kwa Jeshi la Polisi na Serikali katika kutenda haki.

Ofisa kutoka Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Fidelis Sekumba, alisema uchunguzi wa kisayansi unatoa ushahidi wa uhakika zaidi, na hivyo kurahisisha maamuzi ya kisheria katika mihimili inayohusika na utoaji wa haki.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, George Kyando, alisisitiza kuwa uchunguzi wa kisayansi unategemea uzalendo, uaminifu, weledi, na uadilifu. Aliongeza kuwa wahitimu wa kozi mbalimbali za uchunguzi chuoni hapo watakuwa mabalozi wa teknolojia ya kisayansi nchini, huku akibainisha kuwa kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Forensic for Justice.”

Maadhimisho hayo yanaonyesha jinsi teknolojia ya uchunguzi wa kisayansi inavyoendelea kuimarisha mifumo ya utoaji haki nchini Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles