Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mama wa marehemu Steven Kanumba, Frola Mtegoa, amesema kwamba hajawahi kuangalia filamu ya mwanae tangu alipofariki kwa sababu zinamletea maumivu ya kihisia. Alieleza hisia zake kwenye Tamasha la Faraja ya Tasnia 2024 lililofanyika Septemba 7, 2024, jijini Dar es Salaam. Tamasha hili lina lengo la kuwaenzi wasanii na wanahabari waliotangulia mbele ya haki, akiwemo Steven Kanumba.
Frola alieleza kuwa tamasha kama hilo ni muhimu kwa sababu linasaidia kuwakumbuka wapendwa waliotangulia. Alifurahia kuwa mwanae bado anakumbukwa miaka 12 tangu kifo chake, kilichotokea Aprili 7, 2012. Alipongeza waandaji wa tamasha kwa juhudi zao za kuwaenzi wasanii na wanahabari waliotangulia.
Kwa upande mwingine, msanii wa maigizo Vaileth Malle, maarufu kama Mama Afrika, alisisitiza kuwa kumbukumbu hizi zina umuhimu mkubwa kwao kama wanatasnia kwani zinawawezesha kuendelea kuyaenzi yale mazuri yaliyofanywa na marehemu.
Tamasha la Faraja ya Tasnia 2024 limeudhuriwa na wasanii na viongozi mbalimbali, likiwa ni tukio muhimu la kuwaenzi zaidi ya wasanii 230 waliotangulia mbele ya haki, wakiwemo marehemu kama Albert Mangwair, Amina Chifupa, Ruge Mutahaba, na wengineo.