26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii kunufaika ziara ya Mhubiri Ezekiel nchini, kuponya migogoro ya ndoa, maadili

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAKATI akitarajia kuanza mkutano wa siku tano wa injili uliopewa jina la ‘Miujiza na Ishara’ jijini Mwanza, imeelezwa kuwa jamii itanufaika na ziara ya Mhubiri maarufu kutoka Kenya, Ezekiel Odero ambaye anatarajia kujenga shule, kutoa huduma za matibabu, uponyaji wa familia na ndoa.

Mhubiri huyo atafanya mikutano hiyo katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia Julai 24-28, mwaka huu, huku ukihusisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini, mataifa 10 na viongozi zaidi ya 200 wa madhehebu mbalimbali nchini.

Akizungumza leo Julai 22, 2024 jijini Mwanza, Mratibu wa mikutano hiyo, Nabii Utukufu kwa Bwana Peter, amesema mhubiri huyo wa kanisa la New Life Prayer & Church ameshatoa zaidi ya Sh milioni 100 za ujenzi wa nyumba za waathirika wa maporomoko ya udongo Hanang, na Sh milioni 10 za maendeleo ya timu ya Pamba Jiji, huku akitarajia kujenga shule mpya katika eneo lililoathirika wilayani Hanang.

“Mikutano hii ya injili inakuja na neema nyingi, tunaposema tunagusa maisha ya watu tunagusa kiroho, kimwili na kwenye maisha na tumekuwa tukishiriki kwenye shughuli za kijamii ikiwemo kujenga shule na viwanja,” amesema Nabii Peter na kuongeza;

“Ujenzi huu unatokana na fedha za washirika, sadaka na matoleo zinazopatikana kwa waumini kutoka maeneo mbalimbali. Huduma yetu haina mfadhili kutoka mahali popote, injili ya Pasta Ezekiel haina ufadhili inatoka kwa Mungu na inaleta mabadiliko kwa watu wake,” amesema Nabii Peter

Mratibu huyo ameitaka jamii kuzingatia mahubiri na mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini ili kuwa na familia imara na taifa lenye maadili kwani hivi sasa jamii inashuhudia matukio mengi yasiyofaa ikiwemo wanandoa kuuana huku watoto wakilelewa na mzazi mmoja.

“Kama tunavyojua kwa sasa tuko kwenye wakati ambao maadili yameharibika, tunabaki kwenye jamii ambayo mtoto halelewi na baba na mama kwa sababu familia hazipendani, ndoa hazina amani na furaha. Mtumishi wa Mungu Pastor Ezekiel mahubiri yake huweza kuwapa watu uadilifu na kuwasaidia kuwa na amani kwenye familia na ndoa,”

“Kwahiyo mahubiri yake tunaona watu wengi wanarejea katika matendo yampendezayo Mungu. Familia zetu zikipata mafundisho ya dini ni rahisi sana kupata familia nzuri na taifa lenye maadili. Matukio ya ajabu kama mauaji yanapunguzwa kwa neno la injili linaloleta amani, afya ya akili, maadili na furaha,” amesema Nabii Peter

Kwa upande wake, Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Lazaro Roman, amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa kwani uwanja huo una uwezo wa kubeba watu 35,000, ambapo wakati wa mikutano hiyo mageti sita yatafunguliwa kuanzia saa 1 asubuhi.

“Tunashukuru kupokea ugeni huu mkubwa unaohusisha mataifa zaidi ya 10, tumejipanga vizuri hali ya uwanja iko vizuri. Kanisa hili limekuwa limekuwa likishirikiana nasi katika marekebisho mbalimbali ya uwanja wetu na wametuambia wana mpango wa kutusaidia kuupaka rangi,” amesema Roman

Mmoja wa wafuasi wa mhubiri huyo, Hafsa Sakhi aliyesafiri kutoka mkoani Ruvuma kuhudhuria mkutano huo, amesema anategemea kupata mafanikio yatakayotokana na uponyaji na huduma ya maombezi kutoka kwa Pasta Ezekiel Odero.

“Nimekuwa nikimfuatilia kwa muda mrefu kwenye televisheni niliposikia anakuja nikaona nije naamini nikimuona nitatatua matatizo yangu na kupata uponyaji, nafikiri nitafunguliwa na vingi ikiwemo nyota, afya, kuiombea familia yangu, kazi na kupata uponyaji,” amesema Hafsa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles